Kikwete akizungumza kwenye kilele cha miaka 37 ya CCM leo |
NA BASHIR NKOROMO, MBEYA
MWENYEKITI wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete leo amevunja ukimya na kuzungumzia suala la mawaziri waliotuhumiwa na wananchi kuwa mizigo wakati wa ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti katika mikoa kadhaa nchini mwishoni mwa mwaka jana.
"Najua wapo baadhi ya watanzania, walitaka
Mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo wafukuzwe kazi, na kwa vile
halikufanyika basi suala hilo limegeuzwa kuwa la malumbano,
ni vyema ieleweke kuwa kuitwa kwa Mawaziri hao na Kamati Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), hakuna maana ya kuishia kufukuzwa", alisema, Kikwete leo akihutubia maelfu ya watu katika sherehe za kilele cha miaka 37 ya CCM, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Alisema
Mawaziri hao waliitwa kwa sababu ya kuwepo matatizo yaliyoonekana
yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi, matatizo hayo yamezungumzwa na maelekezo
kutolewa kuhusu cha kufanya.
"Kamati
Kuu ya CCM imetimiza wajibu wake uliobaki ni wa serikali.Kamati Kuu
itaendelea kufuatilia na kama hakuna maendeleo ndipo inapoweza kuamua
kuomba mamlaka ya uteuzi ichukue hatua zipasazo dhidi ya mhusika.Huko
hatujafika" alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alimpongeza
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akisema, ziara ambazo amekuwa akifanya ni mfano unaopaswa kuigwa na viongozi wengine hasa wa CCM kwa sababu ndio hasa unaotakiwa.
Alisema ziara za Kinana zinakijenga Chama na kutoa taswira nzuri ya CCM katika jamii kwani zinahuisha uhai wa CCM kwa kuwa Katibu Mkuu huyo katika ziara hizo huenda hadi kwa wanachama waliopo ngazi za chini.
"Katibu
Mkuu Kinana amekuwa anafanya mambo ambayo baadhi ya watu wanadhani kuwa ni mageni, lakini katika kufanya hayo amekuwa pia akionyesha umahiri na ujasiri mkubwa kwa kwenda maeneo ambayo ni magumu kufikika" alisema Rais
Kikwete na kuongeza;
"Katika ziara hizo
wakati mwingine amekuwa anatumia njia za usafiri zinazoogopesha, amewahi kutumia meli ya MV Songea kutoka
mkoani Ruvuma hadi Mbeya, amepanda milima na mabonde kwa magari katika maeneo ambayo ni hatari, lakini lengo likiwa ni kuhakikisha anawafikia wanachama wa ngazi za chini kabisa".
Rais
Kikwete alisema mambo mengine yalivyomvutia katika ziara za Kinana, ni hatua ya Katibu mkuu huyo kwenda kukaa na kula na wananchi katika ngazi za chini na kisha kufanya nao kazi za maendeleo na zaidi kutoa fursa kwa wananchi kueleza matatizo
na manung'uniko yanayowasibu.
Mwenyekiti
huyo wa CCM Taifa alisema Katibu mkuu wa Chama amekuwa anashiriki
katika kutafuta majawabu na matatizo anayoambiwa hali ambayo imesaidia
sana kumaliza baadhi ya matatizo kulekule mikoani.
"Pale
ambapo pamekuwa panahitaji hatua zaidi za serikali hakusita kutoa
taarifa kwa Waziri Mkuu, vile vile amekuwa anatoa taarifa ya ziara zake
kwenye Kamati Kuu ya CCM" alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇