|
RAIS JAKAYA KIKWETE |
IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. Jakaya Kikwete
amemtumia Salamu za Rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu, Abdulrahaman Kinana kufuatia kifo cha Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali hapa nchini, Ndugu
Deusdedith Makandila Mtambalike aliyefariki dunia tarehe 16 Januari, 2014
nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Enzi za Uhai
wake, Marehemu Deusdedith Mtambalike, licha ya kuwa Kada hodari wa CCM, aliwahi
kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya za Ngara na Muleba Mkoani
Kagera, Wilaya ya Igunga katika Mkoa wa Tabora, Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa
Iringa na katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.
“Nimepokea
kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Deusdedith
Makandila Mtambalike, Kada makini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mmoja wa
Viongozi makini katika Utumishi wa Umma aliyewahi kushika wadhifa wa Mkuu wa
Wilaya katika Wilaya mbalimbali hapa nchini”, amesema Rais Kikwete
katika Salamu zake za Rambirambi zilizosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo.
Taarifa imesema, Rais Kikwete
amesema alimfahamu Marehemu Desudedith Mtambalike, enzi za uhai wake, kama Kada
Hodari, Mwaminifu na Mchapakazi wa Chama Cha Mapinduzi, na mmoja wa Wakuu wa
Wilaya aliyekuwa makini katika kazi zake ambaye aliutumikia wadhifa huo kwa
umakini na uaminifu mkubwa, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo
ya Wananchi katika sehemu zote alizofanya kazi.
“Kuondoka kwa Mheshimiwa
Deusdedith Mtambalike ni pigo kubwa kwa Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambako mchango wa mawazo na ushauri wa Marehemu ulikuwa bado unahitajika sana
kwetu sote”,
ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
“Kutokana na
msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahaman
Kinana Salamu zangu za Rambirambi kutokana na kifo cha Kada huyu wa CCM, na
kupitia kwako kwa Wanachama na wapenzi wote wa Chama Cha mapinduzi kwa kuondokewa
na mwenzao, Bwana Deusdedith Makandila Mtambalike”, amesema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete
amemuomba Mheshimiwa Kinana kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi
kwa Familia ya Mtambalike kwa kuondokewa na Baba, Kiongozi na Mhimili wa Familia.
Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha
maombolezo ya mpendwa wao, huku akiwahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika
kuomboleza msiba huu mkubwa.
Amesema
anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema
Peponi, Roho ya Marehemu Deusdedith Makandila Mtambalike, Amina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇