Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dr Shein,Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Ndg Sadifah Juma wakiongoza matembezi ya Vijana. |
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema, katika kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi, vijana hawana budi
kuzingatia mafunzo ya msingi ya mwenendo wa waasisi wa Mapinduzi hayo.
Dk.
Shein amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa
matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya
mwaka 1964 huko Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dk.
Shein amebainisha kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 ambao yaliwakomboa
wananchi wa Zanzibar yaliwezekana tu kutokana na ujasiri, mshikamano,
moyo wa kujitolea na uzalendo pamoja na ukweli miongoni mwa waasisi wa
Mapindhzi hayo.
Aliwaeleza
mamia ya vijana kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wanaoshiriki matembezi
hayo kuwa katika hali ya unyonge waliyokuwa nayo wananchi wa Zanzibar
na uwezo mkubwa wa utawala wa kikoloni uamuzi wa kufanya Mapinduzi
ulikuwa mgumu lakini waasisi hao hawazingatia hayo kutokana na ujasiri
waliokuwa nao na umadhubuti wa mshikamano wao.
Aliwakumbusha
vijana hao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni jambo la lazima
kutokana na ukandamizaji waliokuwa wakifanyiwa wa nanchi huku wakifanyiwa kila aina ya njama na misukosuko wasiweze kujitawala.
“Chama
cha ASP katika kipindi cha miaka 7 tangu kuanzishwa mwaka 1957
kulipitia misukosuko mingi, viongozi na wanachama wake walikabiliana na
vitisho, mbuni za kuwagawa na vitendo vya hila katika uchaguzi wa mwaka
1957, Januari 1961, Juni 1961 na uchaguzi wa mwaka 1963” Dk. Shein
alieleza baadhi ya visa hivyo.
Kwa
hiyo alisisitiza kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa halali kwa kuwa
ndio yaliyowapa wananchi wote wa Zanzibar haki ya kujitawala na
kuwaondoshea kila aina ya ubaguzi.
“Ni Mapinduzi yaliyowaondoshea wananchi wa Zanzibar unyonge wa kutawaliwa kwa karibu karne na
nusu, ndio yaliyowaondoshea ubaguzi katika elimu, afya, ardhi na
unyonyaji kwa kutangaza huduma hizo bila ya malipo” Dk. Shein alieleza.
Alifafanua kuwa kuweka hali za wananchi sawa kwa kuondosha ubaguzi na malipo katika huduma kama afya na elimu ni miongoni mwa ahadi za chama cha ASP na ndio maana, hatua kwa hatua, tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Kwanza hadi sasa zimekuwa zikitekeleza ahadi hizo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameutaka Umoja wa
Vijana wa CCM kuendelea kuyalinda Mapinduzi na Muungano vitu
alivyovieleza kuwa ndio nguzo mbili kuu za msingi wa uhuru, amani na
maendeleo yaliyopatikana katika miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
ifikapo Aprili, 2014.
Akizungumza
katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Sadifa Juma
Khamis alieleza kuwa madhumuni ya matembezi hayo ni kupeleka ujumbe wa
Mapinduzi kwa jamii ili kuleta hamasa kukumbuka mchango wa vijana katika
Mapinduzi hayo ambayo hayawezi kufutika katika historia ya nchi yetu.
Alisema
kuwa UVCCM inathamini sana mchango wa vijana wenzao waliofanya
Mapinduzi wakiwa chini ya uongozi wa Jemedari Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume.
Mwenyekiti
huyo wa UVCCM aliongeza kuwa Mapinduzi ni tukio la kihistoria katika
maendeleo ya Zanzibar hivyo vijana hawana budi kufanya tathmini ya nchi
ilikotoka, ilipo na inakokwenda na kuchukua nafasi yao katika kuleta
maendeleo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇