Rais Kikwete |
Mwenyekiti wa CCM, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Abdulrahaman Kinana kufuatia
kifo cha ghafla cha Diwani wa Kata ya Njombe Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Mkoa wa Njombe, Ndugu Lupyana Fute.
Ndugu Fute alifariki ghafla tarehe 19 Oktoba, 2013 nyumbani kwake Mtaa wa Mgendela
katika Kata ya Njombe Mjini kutokana na shinikizo la damu.
“Nimepokea kwa
mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Diwani wa Kata ya
Njombe Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mheshimiwa Lupyana Fute ambaye, enzi za uhai wake, nilimfahamu kama
Kiongozi Mchapakazi na Mwanachama Mwaminifu na Mwadilifu wa CCM aliyekisaidia
sana Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa majukumu yake”, amesema kwa
masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete
amesema anaelewa fika kuwa kuondoka kwa ghafla kwa Mheshimiwa Fute kumeleta
simanzi na majonzi makubwa siyo tu kwa Familia yake, bali pia kwa Wananchi
aliokuwa akiwaongoza katika Wadhifa wake wa Udiwani, Wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi katika Mkoa wa Njombe, na kwa kweli kwa Wanachama wengine wa CCM kote
nchini ambao wataukosa mchango wa Mwanachama huyu muhimu.
“Kutokana na
Msiba huu Mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahaman
Kinana Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Viongozi muhimu katika
Chama chetu. Vilevile kupitia kwako
naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi zifike kwa Familia ya Marehemu
Lupyana Fute kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia”, amesema Rais
Kikwete na kuongeza,
“Ninawahakikishia
kuwa niko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha Maombolezo ya Mpendwa wao,
na namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi
Roho ya Marehemu Lupyana Fute, Amina”.
Vilevile Rais
Kikwete amemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahaman Kinana kumfikishia
Salamu zake za Rambirambi kwa Wana-CCM kote nchini hususan wa Mkoa Mpya wa
Njombe ambao Marehemu alikuwa
akiwawakilisha katika Wadhifa wake wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Amewaomba wafuate mfano mzuri wa uchapakazi, uaminifu
na uadilifu wa Marehemu katika utendaji wa kazi zao.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22
Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇