*Awataka
kutoa michango ya maendeleo kwa jamii inayowazunguka
KATIBU Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewataka wawekezaji nchi
kujenga tabia ya kutoa michango ya maendeleo kwenye maeneo ambayo wamewekeza na
si kutoa michango ili kumfurahisha Rais
au Waziri Mkuu.
Kinana
alitoa kauli hiyo jana katika Kijiji cha Mwendakulima katika Wilaya ya Kahama
mkoani Shinyanga ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake ambayo itakuwa kwa
Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara ambapo akiwa eneo hilo alizungumzia umuhimu
wa wawezaji kujitahidi kufanya maendeleo kwa wananchi ambao wamewekeza kwenye
maeneo yao.
“Wawekezaji
wapo tayari kutoa hadi sh.milioni 200 wakiwa Dar es Salaam, Mwanza au Arusha,
lakini ushauri wangu kwao, ni vema wakachangia kwenye maeneo ambayo wamewekeza
kwani hiyo itasaidia kuondoa malalamiko lakini pia itakuwa ni jambo jema
wananchi kunufaika kutokana na uwekezaji huo.
Alisisitiza
kuwa anatambua umuhimu wa wawekezaji kuchangia maendeleo lakini inapendeza
zaidi inapofika mahali wananchi wakawa
na maendeleo kutokana na wawekezaji.
Kinana
alifafanua hayo zaidi wakati akizindua kituo cha afya kwenye kijiji hicho
ambacho kimejengwa na kampuni ya madini ya Buzwagyi ambapo alisema kampuni hiyo
imeanza na eneo la afya lakini mwaka mwingine wanaweza kujenga miundombinu ya
barabara na mwaka unaofuata kufanya jambo lingine la maendeleo.
Wakati huo
huo Katibu Mkuu huyo , alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kushiriki kikamilifu
kwenye mchakato wa Katiba mpya na kwamba msimamo wa chama chake ni Serikali
mbili lakini wapo tayari kwa uamuzi ambao utafanywa na wananchi kwa kuamua aina
ya katiba ambayo wanahitaji.
Pia alisema
wananchi wafahamu kuwa licha ya umuhimu wa kuwa na Katiba mpya lakini hiyo
haitakuwa mbadala wa kuwa na mabadiliko ya maisha baada ya kupatikana kwake
ambapo alitoa mifano ya nchi kadhaa Afrika na Asia ambazo zilipata katiba mpya
lakini hali ya uchumi kwa watu wake imebaki kuwa ile ile.
Akifafanua
kuhusu msimamo wa CCM wa kutaka muundo wa Serikali mbili, Kinana alisema hakuna
sababu ya kuwa na Serikali ya tatu kwani kuwanayo ni kuongeza mizigo kwa
Mtanzania kwani ni gharama kuindesha kwake lakini pia haitakuwa na kazi.
Pia Kinana
akiwa Kahama alizindua Saccos ya Mkombozi katika eneo la Isaka ambapo alitumia
nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kubuni miradi ya maendeleo lakini pia kwa
vijana kujiendeleza kielimu hasa kusoma masomo ya ufundi yakiwamo ya ujenzi,
ufundi mchundo na aina nyingine nyingine ya taaluma ya ufundi ambayo
itawawezesha kupaa kipato.
Katika
kuhakikisha hilo la masomo ya ufundi linafanikiwa,Kinana aliweza kutoa ahadi ya
kusomesha vijana 10 wa eneo la Kahama na kwamba kama gharama itakuwa nafuu
ataongeza idadi ya vijana ikiwa ni sehemu ya kufanikisha malengo ya vijana.
Wakati huo
huo akiwa katika Uwanja wa CDT Kinana aliwataka Watanzania kuwa makini na
wapinzani kwani nia yao si kuwaisaidia Watanzania bali n kutafuta maslahi yao
na ndio maana wapo tayari kufanya lolote kufanikisha kile wanachokitaka.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana akikata utepe kuashiria kukamilika kwa awamu ya kwanza ya jengo la kituo cha afya cha kijiji cha Mwendakulima ambalo limedhaminiwa na Mgodi wa Buzwagi.


No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇