Meza Kuu kutoka kulia Katibu Mkuu wa UVCCM Martine Shigela, M/kiti wa UVCCM Taifa Sadifah Juma, Naibu Katibu Mkuu Znz Ally Vuai na M/kiti wa Mkoa wa Magharib Yusuph M. yusuph. |
Naibu Kaibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi upande wa Zanzibar, ndugu Vuai Ally Vuai
ameeleza kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kudumisha muungano ulioasisiwa na
muasisi wa Serikali ya mapinduzi na Chama cha ASP Marehemu Abeid Amani Karume.
Mheshimiwa Vuai ameyaeleza hayo katika Kongamano la kumuenzi
muasisi wa Mapinduzi-marehemu Mzee Abeid Amani karume lililoandaliwa na Jumuiya
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) chini ya mwenyekiti wake
Ndugu Sadifah Juma, lililofanyika katika Ukumbi wa chuo cha Ufundi Karume,
Mbweni Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Umoja huo akiwemo
Katibu Mkuu wa UVCCM, ndugu Martine Shigela, Makatibu wa Idara za UVCCM na
maafisa wengine wa Makao Makuu Bara na Zanzibar, na wajumbe wengine 600 kutoka
katika Mikoa mbalimbali ya Zanzibar, pamoja na wawakilishi kutoka vyuo vikuu.
Katika Nasaha zake na salamu za ufunguzi wa Kongamano hilo,
Mheshimiwa Vuai alifafanua umuhimu wa kuwaenzi waasisi wa muungano na kusema kuwa
vijana wana wajibu wa kutafakari na kujifunza kutokana na viongozi wao
waliopita, wajifunze ujasiri, uzalendo na kusimamia misingi ya umoja na utaifa.
Alisema kuwa Mapinduzi yalikuwa ni halali
kwa kuwa Serikali iliyopinduliwa ilikuwa ni Serikali chini ya Sultan
ikinufaisha wachache, hivyo Mapinduzi yalilenga kuleta utawala ulio huru wa
watu wa Zanzibar, yalilenga kutetea Uafrika yakiongozwa na mioyo ya kizalendo
na nia ya kuijenga Zanzibar na kunufaisha wengi katika wazanzibar wenyewe.
Alisisitiza kuwa muungano una manufaa makubwa kwa
wanzanzibar akitolea mifano ya manufaa yanayopatikana katika sekta mbalimbali
za kimaendeleo na kijamii ambapo alianza kwa kutaja manufaa yanayopatikana
katika sekta ya Elimu ambapo alitaja kuwa kupitia muungano , wanafunzi takribani
1251 waliweza kupatiwa mikopo ya elimu ya juu chini ya bodi ya mikopo ya wanafunzi
(HESLB) ikiwa ni wanafunzi si zaidi ya mia nane na sitini (860) ndio ambao
waliweza kupatiwa mikopo na Serikali ya Mapinduzi hii ni kulingana na bajeti na
uwezo wa Serikali ya mapinduzi.
Lakini pia, Mheshimiwa Vuai alitaja fursa katika sekta ya
afya, ambapo akasema kuwa wagonjwa mbalimbali ambao wamekuwa na matatizo makubwa
na yanayohitajia utaalamu zaidi wamekuwa wakipelekwa katika Hospitali Kuu ya rufaa ya Muhimbili
kama walivyo watanzania wengine kwa gharama ya chini sawa na watanzania
wengine, na akasisitiza haya yanapatikana chini ya kivuli cha muungano. Akaeleza
pamoja na fursa hii kuwepo kwa fursa nyingine za makazi, biashara n.k
Pamoja na kufafanua juu ya faida na manufaa hayo Mheshimiwa
vuai alisema kuwa ni kweli kuwa zipo kero mbalimbali katika muungano, ambapo
akasisitiza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC)
imejadili na kutoa fursa kwa kero hizo kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Mheshimiwa
Vuai alisema kama tatizo ni kujiunga na OIC, NEC ya CCM imetoa fursa ya
kulijadli hilo na kuruhusiwa ikionekana inafaa, ama ikiwa kero ni mapato ya
Bandari, ama mafuta ama takwimu basi NEC imetoa fursa ya kuyajadili haya na
ikionekana inafaa yatolewe katika muungano, na pia kulibainisha suala la
mahusiano ya kimataifa na suala la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Visiwa Duniani.
Akasisitiza kuwa vijana wasiwe tayari kufuata mawazo ya
wapinga mapinduzi na wapinga muungano kwani hao ni watu wanaotaka kurudisha
ukoloni kwa mlango wa nyuma, kwa kuwa wanapinga muungano bila ya kuwa na sababu
za msingi wala hoja.
“..wakiulizwa kwanini
hamtaki muungano hali ya kuwa imetolewa nafasi ya kujadili kero na kasoro
zilizopo katika muungano ili uwe bora zaidi na wenye manufaa zaidi, wapinga
muungano husema tu kuwa hatutaki muungano, lakini sisi wanaotuita wahafidhina
tunajua kuwa wao ni mawakala wa ukoloni na wapinga mapinduzi..” alisema
Mheshimiwa Vuai.
Pamoja na kuelezea kwa kina suala la muungano, Mheshimiwa Vuai
aliwakumbusha Vijana juu wajibu na jukumu lao la kushiriki katika uchaguzi wa
wajumbe wa mabazara ya katiba na kutumia haki yao hiyo ya kidemokrasia.
Kongamano hilo la siku moja lilimalizika saa 12: 15 jioni,
ambapo mada mbalimbali kama Mchango wa Marehemu Karume katika Ukombozi wa
Zanzibar iliyofikishwa na Ndugu Haji Machano Haji pamoja na mada ya Fursa za
Kielimu, Kiuchumi na Kijamii, zilizopatikana baada ya Mapinduzi Matukufu ya
January 12, 1964 iliyowasilishwa na Haroun Suleiman (MNEC) na Mada ya Mwisho
kuwasilishwa ikiwa ni DHANA YA MAPINDUZI YA JANUARY 12, 1964 na kwanini
yalifanyika ikiwasilishwa na Ramadhan A. Ramadhani (MNEC).
Wajumbe wa Kongamano hilo wanategemea kuhudhuria shughuli ya
Kumbukumbu ya Marehemu Mzee Karume zitakazofanyika kesho Jumapili tarehe 07
April 2013, katika Afisi kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyopo kisiwandui Zanzibar.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇