Mhe. Rais Jakaya M. Kikwete. |
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA
WANANCHI, 28 FEBRUARI, 2013
Utangulizi
Ndugu
wananchi;
Namshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea
wa kufanya hivyo kila mwisho wa mwezi.
Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa Amani, Usalama na
Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu na
Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne.
Mpango wa Amani, Usalama na
Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe.
Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na
Kusini kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake. Pamoja
na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda, Uganda,
Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola, Zambia na
Tanzania ambazo ni jirani ya Kongo. Nchi
za Ethiopia, Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja
wa Afrika zilitia saini kama wadhamini.
Ethiopia kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika
na Msumbiji kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC). Nchi wanachama wa Mkutano wa
Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti wake wa
sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa
kwa kuwa taifa kubwa na linalotegemewa katika
ukanda wetu.
Mpango
huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ipate
amani ya kudumu. Kama tujuavyo, tangu
mwaka 1997 wakati wa vita vilivyosababisha kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko
mpaka sasa nchi hiyo rafiki na jirani haijapata amani na utulivu wa
kudumu. Kumekuwepo jitihada na mipango
kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea
tena na mipango hiyo kuvurugika.
Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni
5.4 wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi
yao. Pia kumekuwepo na vitendo vya
ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi kuharibiwa au
kuporwa.
Ndugu
Wananchi;
Machafuko
yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo sababu ya
kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa, Ethiopia tarehe
8 Februari, 2013. Katika Mpango huo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana
kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi zetu. Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja
kama nchi au kwa kutumia watu wengine.
Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu kutumia nchi
zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine.
Kimsingi tumekubaliana kuwa majirani wema. Katika Mkataba huo, majukumu ya kila nchi
yameainishwa vizuri pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na
Mashirika ya Kikanda hususan SADC na ICGLR.
Ndugu
Wananchi;
Niliamua
kukubali kushiriki na kutia saini Mpango ule kwa kutambua ukweli kwamba sisi
majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia kwa kile tunachoweza. Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu
mno hivyo kama Mpango huu utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi
kuunga mkono. Ni kwa misingi hiyo hiyo,
tulikubali kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi la Kimataifa la kulinda amani
huko Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu
mwezi Julai, 2012. Uamuzi huo umeungwa
mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika. Umoja wa Mataifa umeamua
Jeshi hilo liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani nchini
Kongo (MONUSCO) jambo ambalo sote tumeliafiki.
Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini
tusipeleke Kingo. Miaka ya nyuma
tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera Leon na Eritrea.
Ni
matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa matunda
yaliyokusudiwa. Kama nchi jirani,
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye
maslahi makubwa kwetu. Ina maana ya
kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika
kutokuwepo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu na
wao. Ni chachu muhimu ya maendeleo ya
Mikoa ya pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano
wa Waislamu na Wakristo
Ndugu
wananchi;
Jambo la pili ninalopanga
kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini. Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana
kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki
baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini
za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za
ibada na mzozo kuhusu nani achinje. Kumekuwepo na matumizi mabaya ya radio na simu za
mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano
iliyoeneza maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini
zetu hizi kubwa hapa nchini. Kauli na
matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama na magomvi
baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea Buseresere
Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu
zangu;
Watanzania hatujawahi kuwa hivi,
kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu tunaotambua na kuheshimu tofauti
za dini zetu mbalimbali tunazoabudu.
Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti
zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu, kwa umoja na kushirikiana
kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati kila mmoja anapoingia
kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na taratibu ya dini yake.
Watanzania wa dini zote na makabila tofauti wanaishi
nyumba moja, wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na
ushirikiano. Kuna koo na familia zenye
watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo. Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na
wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake. Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto
na wanashirikiana kulea watoto wao. Hayo
ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu
tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi
sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu
zetu.
Ndugu
Wananchi;
Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua
wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii
nzuri. Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani
hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu. Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia
hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya
dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha
Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna
hiyo. Wawachukulie hatua stahiki wale
wote wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo
wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”. Wachochezi
wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa
ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia. Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi
wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao. Pia nimewataka Polisi wakamilishe mapema
upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye
vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ndugu
Wananchi;
Naendelea
kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum wa
kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na mifarakano
miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini.
Hali kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza
na wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano
mwema baina yao.
Ndugu
Wananchi;
Kuna msemo maarufu usemao “mjenga
nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa
wabomoa nchi. Hivi tukiibomoa nchi yetu
tutakwenda wapi? Tutaishi wapi?
Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.
Kwa
mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole makanisa,
familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa
kuondokewa na wapendwa wao. Serikali na
wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu. Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa
waumini wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki
Tanzania kwa kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu
azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu.
Amin.
Matokeo
ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu
wananchi;
Tarehe
18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012. Wanafunzi
397,132 walifanya mtihani huo na
kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani
sawa na asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903
ambao ni sawa na asilimia 65.5
hawakufaulu mtihani huo. Kwa ulinganifu,
matokeo hayo ni mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi
karibuni.
Mwaka
2011, jumla ya wanafunzi 336,782
walifanya mtihani huo na waliofaulu walikuwa asilimia 53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia 46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya
wanafunzi hao walifaulu na asilimia 49.6 ya wanafunzi hawakufaulu.
Ndugu
Wananchi;
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne
mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki
kabisa. Kwanza, kwamba kiwango cha
kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia
34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni
kubwa sana. Pili, kwamba hata shule
zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule
za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo
hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii
hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao.
Nazo zimejikuta zikiwa na idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la
pili na la tatu ikipungua wakati waliopata daraja la nne na waliofeli
wakiongezeka.
Isitoshe
na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua pia.
Mwaka 2010 wanafunzi 10 bora
wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama au pointi 7. Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza kwa alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora, watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 na
wawili alama 11.
Ndugu
Wananchi;
Haya
ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa majawabu ya
uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mhe.
Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima la mitihani ya
mwaka 2012 na matokeo yake. Hali hii
haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi
yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika. Hii itawezesha Serikali na wadau wengine
kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo
yawe mazuri siku za usoni. Tusipofanya
hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa
Serikali.
Ndugu
Wananchi;
Hivi sasa kunatolewa mawazo lukuki
kuhusu sababu za kwa nini matokeo yamekuwa mabaya. Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika
utungaji wa mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. Wapo wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo
au baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha.
Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika kufuatilia masomo
na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni. Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera,
mitaala na uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu.
Wapo wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu
kwa asilimia 100 kama walivyotaka imechangia.
Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana mawazo yake. Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa
tunadhani kwa sababu tunayo dhamana maalum.
Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe
kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele cha juu sana kwa
elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na wenzangu wote
Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana
na matokeo haya. Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na
asilimia 24 ya bajeti yote ya
Serikali ndiyo kubwa kuliko zote. Kwa
ajili hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi
mkubwa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu.
Bado hatujazimaliza changamoto zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele
yetu, lakini mafanikio yanaendelea kupatikana.
Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo itakapofikia
mahali kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mungu Ibariki
Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇