Mama JK akipokea aliyekuwa CUF Lindi |
MJUMBE WA Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amehitimisha siku saba za ziara yake Wilaya ya Lindi mjini akiwa ameikomba CUF wanachama 89, kati ya wanachama 1,120 waliojiunga na CCM wakati wa ziara hiyo.
Ziara hiyo iliyomalizika jana ilikuwa na lengo la kukagua na kuimarisha kuimarisha uhai wa Chama, kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama, pia ilikuwa na lengo la kuwashukuru wana-CCM wa wilaya hiyo kwa kumchagua kuwa mjumbe wao wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Katika ziara hiyo Mama Salma Kikwete amefanya mikutano 36 ikiwemo ya nje na ya ndani katika kata 18 zilipo katika wilaya hiyo ambazo ni Mbanja, Chikonji, Ng’apa, Mtanda, Tandangongoro, Rahaleo, Msinjahili, Mingoyo, Mitandi, Mwenge, Jamhuri, Makonde, Ndolo, Matopeni, Wailes, Mikumbi, Lasbula, Mikumbi na Nachingwea.
Karibu kata zote ziliingiza wanachama wengi lakini iliyoongoza zaidi ni Mbanja ambayo wanachama kutoka CUF walikuwa 26 na wanachama wananchi wa kawaida wapya ni 148.
Wanachama kutoka CUF ambao walipata fursa ya kuzungumza mbele ya Mama Salma Kikwete wengi wao walisema wameamua kukihama CUF kwa hiari yao na kwa kuamini kuwa CCM ni Chama makini na pekee chenye uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli Tanzania kwa sasa licha ya kuwepo mfumo wa vyama vingi.
"Katika vyama vya upinzani hususan CUF tulikokuwa hakuna lolote la maana zaidi ya viongozi kutetea maslahi yao binafsi", walisema kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama hao.
Akiwapokea wanachama hao, Mama Salma aliwapongeza kwa uamuzi wao na ,kuwataka watanzania popote walipo wainge mkono kuiunga CCM ili itekeleze ilani ya uchaguzi ili iwaletee maendeleo.
Katika ziara hiyo Mama Salma Kikwete aliambatana na viongozi mbalimbali mkoa na wilaya wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mjini ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa mkoa wa Lindi Dk. Nassoro Ali, Katibu wa CCM mkoa huo, Adelina Gefi, Katibu wa UWT mkoa, Zita Maliyaga, Mbunge wa Viti maalumu, Fatuma Mikidadi, Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Muhsin Ismail na Mwenyekiti wa UWT mkoa, Fadhia Chiwangu.
Mama Salma amemaliza ziara hiyo kwa kufanya vikao cha ndani na viongozi wa CCM mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇