TAARIFA RASMI … CCM 15/12/2012
KAMATI Maalum ya NEC ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, leo imefanya kikao kilichokuwa chini ya Uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Taarifa iliyotolewa na Afisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Vuai Ali Vuai, imesema kikao hicho cha kawaida cha siku moja, pamoja na mambo mengine, kilipokea na kujadili kwa kina taarifa mbalimbali kutoka Idara na Vitengo vya Chama hicho.
Kikao pia kimefanya Mabadiliko katika Safu yake ya Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar. Wajumbe walioteuliwa kuunda Sekretarieti hiyo mpya ni hawa wafuatao :-
1. Ndugu Haji Mkema Haji - Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Organaizesheni.
2. Ndugu Waride Bakari Jabu - Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi
3. Ndugu Hamad Masauni Yussuf - Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) na
4. Ndugu Seif Shaaban Muhamed - Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Uchumi na Fedha.
Aidha, Kamati Maalum ya NEC kwa kauli moja imempongeza kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar (Awamu ya Saba) Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kufuatia kuchaguliwa kwake na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, uliofanyika Mjini Dodoma Novemba 11 - 13, 2012, kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar baada ya kupata kura zote za ndio.
Sambamba na hilo, kikao pia kimewapongeza Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu huo, kwa kumchagua kwa mara nyengine tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2012 - 2017).
Kikao kimempongeza kwa dhati kabisa Makamu Mwenyekiti (Mst.) wa CCM Zanzibar kwa kazi nzuri ya kuwaongoza Wana CCM kwa kipindi chote cha miaka kumi (10) iliyopita tena kwa mafanikio makubwa. Aidha, kikao kimemtakia kila la kheri yeye na familia yake na kumuomba Mwenyezi Mungu amjaalie salama na amani muda wote wa maisha yake.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi kimempongeza kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Ali Muhamed Shein kusimamia na kuimarisha masuala ya Amani na Utulivu, Utekelezaji wa Ilani pamoja na kuisimamia ipasavyo Serikali yake na kuzishughulikia kero mbali mbali zinazowagusa wananchi yakiwemo matatizo ya ardhi.
Mwisho.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
……………….
(Vuai Ali Vuai),
Naibu Katibu Mkuu - CCM,
ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇