Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshangazwa na kustushwa na matamshi yaliojaa upotoshaji, yakimangimeza na fitna za kisiasa yaliotolewa na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad kwa wananchi wa Zanzibar kuhusu maendeleo ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu uundwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoeendelea nchini.
Kwa masikitiko makubwa, CCM kimestushwa na matamshi ya kiongozi huyo ambayo kwayo licha ya kwenda kinyume na dhana ya Utawala Bora, kwa makusudi yamelenga kukiuka misingi ya utawala wa Sheria, kuingilia kazi za Tume ilioundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria na kutaka kuwaparaganya wananchi.
Katika mkutano wa CUF ulioanyika katika Uwanja wa Alabama Wilaya ya Mjini Kisiwani Unguja, Kingozi huyo matamshi yake yameishinikiza Tume ya Rais inayoongozwa na Jaji Jeseph Sinde Warioba, itii na kufuata matakwa yake kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria, huu ni unafiki na upayukaji unaohitaji kupuuzwa.
CCM kinamtaka Katibu Mkuu huyo wa CUF kuacha kuingilia kazi za Tume na badala yake kiongozi huyo aheshimu utaratibu uliopo bila ya kuleta vitisho pia aache kubashiri mambo kama mganga wa kienyeji.
Seif ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inamtaja ni Mshauri Mkuu wa Rais katika utekelezaji wa kazi zake na kwamba atafanya kazi zote atakazopangiwa na Rais.
Aidha Kiongozi huyo anapotaka CUF ielezwe na Tume ya Jaji Warioba kuhusu utaratibu wa uundwaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya , kuutilia shaka uadilifu wa Rais wa Zanzibar katika uteuzi wa wajumbe 164 wa Baraza la Katiba, inaonyesha fika ni jinsi gani asivyomuamini hata Rais aliyemteua kushika wadhifa alionao, akitamani kuamsha malumbano na kutafuta shari mbichi.
Tume haiwezi kukieleza chama chochote cha siasa au mtu binafsi kazi zake, ina haki ya kufuata utaratibu wa utendaji kazi zake unaotegemea matakwa ya sheria, si kinyume na hivyo.
CCM imemsikia Katibu Mkuu wa CUF akitaka kufanyike uteuzi wa Wajumbe wa Baraza la Katiba kulingana na fomula ya matokeo ya kura za urais wa Zanzibar jambo ambalo si la kisheria na halipaswi kulazimishwa na mtu au Taaasisi yeyeote kinyume na sheria inavyoelekeza.
Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika muundo wake wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikufuata fomula ya matokeo ya kura za urais, kilichoangaliwa ni matokeo ya viti vya chama kilichoshinda katika majimbo ambapo CCM ilishinda viti 28 na CUF viti 22 katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba.
Hata hivyo ni vyema Katibu Mkuu huyo wa CUF akafahamu kuwa wananchi wa Tanzania na Zanzibar hupiga kura baada ya kujiandikisha kwenye Daftarai la Kudumu la Wapiga kura bila ya kutenganishwa kwa uzanzibari na Utanzania wao kwa wale wanaoishi Tanzania Bara na Zanzibar.
Mapendekezo anayoyapigania si ya Kikatiba wala hayana mashiko yoyote ya kisheria zaidi ya kutaka kuanzisha vurugu mpya za kisiasa na malumbano yasio na tija katika majukwa ya ya kisiasa.
Pengine anachokitafuta Seif katika zoezi hili la mchakato wa ukusanyaji na utoaji wa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya linaloendelea , ni utekelezaji wa wa mikakati yake ya miaka mingi ya kuwabagua na kuwatenga Wazanzibari miongoni mwa Watanzania ili kuyafakikia matatarajio yake anayoyaanona yameanza kutoweka.
Ikiwa yeye anatajwa na Katiba ya Zanzibar kama Mshauri Mkuu wa Rais, anayo nafasi ya kukutana na Rais,
kumshauri bila ya kuwakanganya na kuwajengea hofu wananchi katika kushiriki kwao na hatma ya zioezi hilo la mchakato wa Katiba linaloendelea.
Chama Cha Mapinduzi kinamuomba Katibu Mkuu huyo wa CUF aache kuwachannganya wananchi na badala yake aheshimu nafasi yake ya Umakamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akifauta utaratibu wa Katiba ya Zanzibar na mtiririko wa kazi atakazopangiwa na Rais.
Ni busara ikiwa Katibu Mkuu wa CUF ataipa uhuru Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba iendelee na kazi zake bila ya kuivuruga au kuiingilia kwa kutaka matakwa yake ya kisisasa yafuatwe hatimae ikiuke taratibu za Kisheria zilizopo.
Kwa nia njema kabisa, CCM inayalaani vikali matamshi hayo yanayokwenda kinyume na ukweli wa mambo ulivyo kuhusu maendeleo ya machakato wa ukusanyaji na utoaji wa maoni unaoendelea.
Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria, ni vyema wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni yao kwa uwazi na kuamini litafika katika hatma itakayoleta faraja kwa mustakabali wa maendeleo ya demokrasia bila ya kutiwa mikono na walafi wa madaraka.
Kadhalika Chama Cha Mapinduzi kinaiomba Tume ya Jaji Warioba iwe macho na njama zinazofanywa na baadhi ya vyama vya Siasa za kuandaa makundi ya vijana ambao si wakaazi wa vituo vya kutoa maoni katika Mkoa wa Mjini/Magharib wilaya ya Mjini jambo ambalo linawanyima fursa na haki wananchi walio wengi kutotoa maoni yao.
Vurugu hizo zimesababisha wananchi wa Shehia ya Mzalendo/Magomeni na Mpendae kushindwa kutoa maoni yao.
Ali Mwinyi Msuko
Katibu Msaidizi Mkuu,
Idara ya Itikadi na Uenezi,
Afisi Kuu ya CCM Zanzibar
11.12. 2012.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇