TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha kinyama
alichofanyiwa Sheikh Fadhili Soraga cha kumwagiwa tindikali sehemu ya uso na kifuani. Sheikh
Soraga ni mtu maarufu hapa Zanzibar kwani huwa anashiriki katika shughuli mbali
mbali za kidini hapa nchini, yeye ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar. Sheikh
Soraga amefanyiwa unyama huo na watu wasiojulikana wakati akitoka kwenye mazoezi ya
viungo asubuhi ya leo.
Sheikh Soraga ni
miongoni mwa masheikh wachache hapa zanzibar wenye kuheshimika na kueleweka. Hivi
karibuni Sheikh Soraga alitoa khutba nzuri na fasaha kwenye sala ya Eid-Haji
juu ya kuimarisha amani na utulivu katika visiwa vyetu vya Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla. Khutba hiyo aliitoa mbele ya viongozi wakubwa wakitaifa
waliohudhuria katika sala hiyo, miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo
wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharifu Hamadi, Rais Mstaafu wa awamu
ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na viongozi wengine kadhaa.
Siku hiyo hiyo katika Baraza la Iddi lililofanyika katika
Ukumbi wa Salama Bwawani Sheikh Soraga wakati akitoa khutba ya utangulizi
aliwaasa tena wazanzibari na watanzania kwa ujumla juu ya umuhimu wa amani,
lakini katika hafla hiyo Sheikh Soraga alikwenda mbali zaidi kwani alitoa
takwimu za hasara iliyoipata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano, mashirika ya watu binafsi na ya Umma, taasisi za Kidini pamoja na
vyama vya Siasa hasa Chama Cha Mapinduzi kufuatia vurugu mbali mbali zilizokuwa
zikifanywa na Uamsho.
Vitendo vya kumwagiwa watu tindikali hapa Zanzibar vimeanza
siku nyingi. Kama tutakumbuka mnamo mwaka 1995 Kada wa Chama Cha Mapinduzi
ndugu Ali Mwinyi Msuko alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana huko Wete
Pemba, mwaka 2007 wakati zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura
huko Pemba Sheha mmoja alimwagiwa tindi kali, na mwaka uliopita Ndugu. Rashid Ali
Juma, Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa
Zanzibar nae alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana na leo hii Sheikh
Fadhil Soraga Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar nae amemwagiwa tindikali pia na
watu wasiojulikana.
Chama Cha Mapinduzi kinasema kimechoka kusikia vitendo hivi
vya kinyama vya kumwagiwa watu tindikali na watu wasiojulikana. Tunaviomba
vyombo vya Dola kuwatafuta watu hawa waovu wasio na huruma na wenzao ili
wakamatwe waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Mwisho Chama Cha Mapinduzi kinawaomba wananchi wote wapenda
amani na utulivu kumuombea dua Mwalimu wetu Sheikh Fadhil Soraga Mwenyezi
Mungu ampe moyo wa subira yeye na familia yake na amjaalie wepesi ili apone
haraka. Sheikh Soraga hivi sasa amesafirishwa kupelekwa Muhimbili kwa Matibabu
zaidi.
“KIDUMU CHAMA CHA
MAPINDUZI’
MAPINDUZI DAIMA
Issa Haji Usssi Gavu
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC
Idara ya Itikadi na Uenezi
ZANZIBAR
06/11/2012
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇