LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 13, 2012

CHADEMA WAJISALIMISHA POLISI, KUHUSU TUHUMA ZA NJAMA ZA KUUAWA VIONGOZI WAO

NA BASHIR NKOROMO, DAR ES SALAAM,
Baada ya kujaribu kuweka kigingi kwamba Chadema hawatakwenda polisi kueleza kuhusu madai yao ya viongozi wa  chama hicho kuundiwa njama za kuuawa na  serikali, hatimaye leo, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilblod Slaa amejisalimisha makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.
    Dk. Slaa akifuatana na baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo mbunge wa zamani wa Arusha mjini Godbless Lema, alifika mida ya saa  nne asubuhi kwa shangingi lake lenye namba za usajili T 875 AKS aina ya Toyota Landcruise.
     Baada ya kufika Dk. Slaa, Lema na  wakili  Dk. Rugemereza Nshala, walishuka na kwenda kwa wenyeji wao Polisi tayari kwa kuhojiwa.
     "Tumefika kuitika wito wa polisi" alisema  Lema baada ya baadhi ya waandishi wa habari kuuliza nini kimewalazimu kuja polisi ilihali walikuwa wameshasema kwamba hawana imani na polisi?
“Tumepata wito na tumeitikia tambueni mjumbe hauawi sasa ni wito wa namna gani ngoja tukawasikilize lakini na ninyi waandishi wa habari hampitwi na kitu kila sehemu mpo” Dk Slaa  akaongeza huku akicheka.
     Baada ya kufika mapokezi Dk Slaa na Lema walielekezwa kwenda chumba namba 703 ambapo walikaa kwa muda wa dakika tano na kisha wakatoka kuelekea chumba namba 808 huku ofisa wa Polisi aliyevaa kiraia akiwataka waandishi wa habari wasiwafuate.
     Katika Chumba namba 808 walichoingia ofisa huyo wa Polisi aliwakaribisha huku akisikia kuwaambia Dk Slaa,Lema na wakili wao Dk. Nshala kuwa wakaribie ingawa eneo hilo lipo, katika ukarabati na kisha kufunga mlango.
      Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa jeshi la polisi Advera Senso, alisema Dk Slaa na wenzake waliitwa kwa ajili ya maelezo ya awali ya kusaidia uchunguzi dhidi ya malalamiko yao ya kuuawa.
     Alisema jeshi la polisi limefungua jalada la uchunguzi na kwamba mlalamikaji ni ni lazima atoe maelezo yatakayoweza kufanyika kwa uchunguzi huo kabala ya jalada kupelekwa kwa Mwendesha mashtaka.
      “Tumewaita kwa hati maalum, dhidi ya malalamiko yao naamini tutashirikiana nao kubaini ukweli na kisha tutafanyia kazi kwa kuwa wajibu wetu ni kumlinda kila mmoja hata kama atakuwa ametolea malalamiko yake chumbani”alisema Senso.
     Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka Dk Slaa alisema suala aliloitiwa ni juu ya malalamiko yao ya kutishiwa kudhuriwa na kwamba alichowaeleza polisi ni kwamba wanapaswa kuyatolea kwanza maelezo ya taarifa za nyuma za kutishiwa kwao ikiwamo suala zima la kuwekewa vinasa sauti wakati akiwa mbunge mjini Dodoma.
      Kila kitu kipo wazi nimewaambia kwa sasa sina maelezo mengine zaidi ya yale niliyotoa katika mkutano na waandishi wa habari, na kubwa nikawataka wanipe mrejesho wa taarifa mbali mbali za kutishiwa kwetu tulizowafikishia kabla”alisema Dk Slaa.
Wakili aliyefuatana na viongozi hao Dk. Rugemereza Nshala, alisema wateja wake wameahidi kupeleka maelezo waliyotoa mbele ya waandishi wa habari na kwamba suala la kuhojiwa ni la kisheria hivyo wananchi wasubiri kujua kitu gani kitaendelea.
Jumapili ya wiki iliyopita Dk Slaa akiwa na viongozi wengine wakuu wa Chadema,walidai kubaini mkakati wa makusudi wa kuwadhuru viongozi wakuu wa chama hicho, mpango waliosema unaratibiwa na baadhi ya vigogo katika idara ya usalama wa Taifa.
PICHANI: Dk. Slaa akishuka kwenye shangingi lake baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Leo kuhijiwa (Picha kwa Hisani kubwa ya Habari Mseto Blogu)

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages