Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilson Mukama, ameagiza
majengo yaliyovunjwa wakati wa maboresho ya Chuo Cha Kilimo na Ufundi
cha Kaole, Bagamoyo mkoa wa Pwani, yajengwe tena na kuwa katika
muonekano wake wa awali ili kuhifadhi historia ya harakati za ukombozi
Barani Afrika.
Ameagiza pia kupitiwa upya mkataba kati ya Jumuiya ya
Wazazi Tanzania na mwekezaji ili kuhakikisha kuwa hakuna
mkanganyiko unaojitokeza katika usimamizi na pia kuainisha wazi namna
majengo hayo ya kihistoria katika eneo hilo yatakavyotunzwa.
Mukama ametoa maagizo hayo wakati alipozungumza na
mwekezaji wa mradi wa chuo hicho, Julian Bujugo na uongozi wa Jumuiya ya
Wazazi inayomiliki eneo hilo, baada ya kufanya ukaguzi na kushuhudia
majengo matatu yaliyokuwa yakitumiwa na Wapigania Uhuru wa Chama Cha
FRELIMO cha Msumbiji yakiwa yamebomolewa.
Majengo yaliyobomolewa ni pamoja na ukumbi uliokuwa
ukitumiwa kufanyia mikutano na wapigania ukombozi, banda la mlinzi na ghala
la kuhifadhia vifaa mbalimbali wakati huo.
FRELIMO
ilikabidhi majengo yote katika eneo hilo kwa CCM baada ya Msumbiji
kupata uhuru wake mwaka 1975 ambapo baadaye CCM nayo iliyakabidhi kwa
Jumuiya yake ya Wazazi, kwa ajili ya kuanzisha mradi wa shule ya
sekondari.
Upande wa majengo yaliyovunjwa, Mukama alisema, ni
lazima yajengwe tena pale pale yalipokuwa na yawe na muonekano ule wa
zamani hata kama yataboreshwa lakini yasipoteze uhalisia wake.
"Majengo haya ni kumbu kumbu muhimu ya harakati za ukombozi barani
Afrika, haifai kuyabomoa kwa kisingizio chochote, ninaagiza
walioyabomoa wayajenge kama yalivyokuwa kwa sababu yataendelea kuwa
heshima kwetu", alisema Mukama.
Alimtaka msimamizi wa Chuo hicho kuhakikisha katika
kuboresha majengo yote katika eneo hilo, ayafanye kuwa na muonekano
mzuri tu, lakini asiyabadilishe muundo wala muonekano wake.
Kuhusu mkataba, Mukama alisema, ili majengo na masuala mengine yote
yaweze kuwa na udhibiti wa uhakika ni lazima upitiwe upya ili usizuke
mgogoro baadae wa nani ni nani katika umiliki, kwa sababu licha ya
mwendelezaji kubadili kutoka shule ya sekondari na kuwa chuo bado
mmiliki halali ni Jumuia ya Wazazi.
Katika mazungumzo, baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya
Wazazi waliofuatana na Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Suleiman Dadi,
walionyesha wasi wasi wao ikiwa mwendeshaji huyo anafanya mambo yake kwa
sasa kwa mujibu wa mkataba.
"Hadi sasa tunaona hapa sasa ni Chuo badala ya
sekondari lakini hatujajua msimamizi halisi ni nani, maana tukija hapa
Mwendeshaji (Bujugo) anasema hatutambui, wakati sisi ndiyo viongozi wa
Jumuia hii hapa wilaya ya Bagamoyo", alisema Mwenyekiti wa Wazazi wilaya
hiyo, Kasim Gogo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mukama ameutaka
uongozi wa Chuo hicho kuacha kufanya biashara ya kuuza pombe na nyama ya
nguruwe kwenye eneo la chuo hicho kwa sababu kufanya hivyo si sahihi
kwenye chuo kwa kuwa wanaosoma eneo hilo wengi bado ni vijana wadogo.
"Hili la kuuza pombe hapa, na kitimoto,
halikubaliki, vijana wanaosoma hapa wengi bado ni wadogo, sasa kuweka pombe
katika eneo la chuo namna hii mtawaharibu, baa ifungwe mara moja",
alisema Mukama.
Mapema Mukama alitembelea maeneo ya chuo hicho na
kushuhudia ukarabati mkubwa ukifanyika, ikiwemo kujenga upya madarasa na
vyoo na baadhi ya majengo yakiwa tayari yamebomolewa kwa ajili ya
kujengwa mapya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇