LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 20, 2021

LIJUE KANISA HALISI LA MUNGU BABA: LINAHIMIZA KUABUDIWA MUNGU BABA PEKEE, AMANI, UPENDO USIOBAGUA, NA UZALISHAJI KWA HAKI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog.
Duniani dini zilianza karne zilizopita, lakini dini hizo hazikuwa nyingi kama ilivyo siku hizi. 


Kwa Tanzania dini zilizotangulia kutambuliwa ni Ukisto, Uislamu, na dini za asilia za Afrika (za jadi), nje ya hizo ni chache kama Uhindu, Usikh na dini nyingine ambazo wafuasi wake wengi ni Wahamiaji katika nchi au wamezaliwa katika vikundi vyenye asili ya uhamiaji kutoka nje.


Katikati ya Karne ya 19 Wamisionari wa kwanza Wakristo walianza kufika Pwani ya Tanzania na kujenga vituo vyao katika Bara la Afrika, Wakristo na Waislamu wakikuta kote wafuasi wa dini za jadi wakihamia polepole upande wa dini hizo za kigeni.  

Pamoja na dini za jadi kuhamia dini za kigeni, lakini desturi na ibada mbalimbali za jadi ziliendelea kufuatwa na baadhi ya Wakristo na Waislamu wapya hadi leo.

 

Madhehebu ya Kikristo yanajumuisha Kanisa Ktoliki, Waprotestanti wa aina mbalimbali (Walutheri, Wapentekoste, Waanglikana, Wamoravian, Wasabato, Wameno, Kanisa Jipya la Kitume n.k), Waorthodoksi wa Mashariki wachache, mbali ya Wamormoni na Mashahidi wa Yehova ambao mara nyingi hawahesabiwi na madhehebu hayo kuwa Wakristo kwa sababu ya kutosadiki Umungu wa Yesu.


Ukristo nchini Tanzania ulianzishwa na Wamisionari wa Shirika la Mt. Agostino kutoka Ureno walioongozana na Vasco da Gama mwaka 1499 hadi Zanzibar. Huko walijenga 'Konventi' ya shirika lao ili kuhudumia kiroho Wakristo toka Ulaya tu. Misheni ilipingwa na Waarabu Waislamu na kukoma mwaka 1698, Kisiwa hicho cha Zanzibar kilipotekwa na Waarabu wa Oman.


Kwa mujibu wa historia, Uinjilishaji ulifanikiwa zaidi katika sehemu ya pili ya Karne ya 19 hasa ulipofanyika katika maeneo ya Bara. Kati ya Waprotestanti, waliotangulia walikuwa wamisionari Krapf na Rebmann waliotumwa na Chama Cha C.M.S.; kutoka kwa kituo chao karibu na Mombasa walifika mpaka eneo la Tanzania ya leo. Kituo cha kwanza cha C.M.S. katika Tanganyika kilikuwa Mpwapwa mwaka 1876.


Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na Masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu. Halafu hao mwaka 1868 wakafungua katika eneo la Bagamoyo Kituo cha kukalisha watumwa waliowanunua na kuwapa uhuru.  Mwaka 1878 Walifuatwa na Mapadri Weupe (White fathers), walioanza mwaka 1879 kwenye Ziwa Tanganyika.


Historia inasemwa, Katika mazingira ya Kanisa la Anglikana Chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati (Universities` Mission to Central Africa - U.M.C.A) kiliundwa kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika. Waliingia Zanzibar mwaka 1864, wakajenga Kanisa Kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.


Baada ya kuanza ukoloni wa Kijerumani serikali iliomba Makanisa ya Ujerumani kuchukua wajibu badala ya kuwaachia watu wa mataifa wengine. Lakini itikio lilikuwa tofauti. Kwa mfano, tarehe 18 Aprili 1887 Padri Andreas Amrhein, mwanzilishi wa Wabenedikto wamisionari wa Mt. Otilia, alimuandikia hivi Papa Leo XIII kuhusu mazungumzo yake na Karl Peters: "Wao wanataka wamisionari kwa ajili ya faida yao wenyewe. Lakini nimeweka masharti: wamisionari wafanye kazi yao kwa uhuru wote, bila kupingwa kwa namna yoyote na wakoloni. Licha ya hayo naona kwamba wamisionari wataweza kuwalinda wenyeji wasinyonywe ovyo na wakoloni na wafanyabiashara".


Walutheri wa kwanza walifika Dar es Salaam mwaka 1887 na Mwaka 1888 walifika watawa Wajerumani wa kwanza wa shirika la Mt. Benedikto waliounda baadaye 'monasteri' za Peramiho na Ndanda na kushughulikia uinjilisti kote Kusini.


Mwaka 1891 walifika wamisionari Walutheri (misheni ya Berlin) na Wamoravia kupitia Ziwa Nyasa wakiwa wamepatana kugawa kati yao maeneo ya kazi kama walivyogawana wachungaji wa Ibrahimu na Lutu; walijenga vituo katika Unyakyusa kule Rungwe na Manow.


Ni kwamba Walutheri waliomba Wamoravia kuanza kazi pamoja katika Tanganyika Kusini-Magharibi. Baadaye walichapisha hata kitabu cha pamoja cha nyimbo za Kikristo. Walutheri wengine yena (misheni ya Leipzig) walianza kule Uchagga kituo cha Moshi.


Wajerumani wengine waliofika mapema walikuwa Waadventista Wasabato na Kutoka Kenya ilianzishwa kazi ya Africa Inland Mission - A.I.M) katika mkoa wa Mwanza - chama hicho kiliundwa Marekani kama misheni ya kimadhehebu yenye athari kubwa ya Kibatisti.


Karne ya 20 iliona wamisionari wengi kutoka madhehebu mbalimbali ya Ulaya na Marekani.

Baada ya vita vya pili vya dunia Wamarekani walianzisha Kanisa la Kibatisti Kusini-Magharibi mwa Tanzania. Walifika pia wamisionari mbalimbali wa Kipentekoste. Tofauti na nchi za Afrika Kusini na Magharibi, wamisionari wa Makanisa ya Wamarekani Weusi hawakuwa na athari kubwa.


Tofauti na Kenya, ambako Kanisa la Kiorthodoksi la Kiafrika (linaloshirikiana na Patriarki wa Kigiriki wa Aleksandria-Misri) ni kubwa, nchini Tanzania halikuenea mapema, isipokuwa wahamiaji Wagiriki walijenga makanisa machache ya Kiorthodoksi Dar es Salaam, Iringa, Arusha n.k.


Katika karne ya 20 ikawa ya kurudisha umoja. Wakristo wa madhehebu mbalimbali yakashirikiana kirahisi katika shughuli mbalimbali.


Mwaka 1936 viongozi wa madhehebu kama Walutheri, Waanglikana, Wabaptisti na Wamoravia waliunda "Baraza la Misheni Tanzania". Baraza hilo lilikuwa mtangulizi wa CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania / Christian Council of Tanzania).


Katika miaka ya 1960 viongozi wa Makanisa ya Kiprotestanti waliongea juu ya kuunda Kanisa la Muungano katika Afrika Mashariki. Kwa bahati mbaya wafadhili wengine kutoka ng'ambo waliona hawawezi kusaidia Kanisa la Muungano kama si tena la madhehebu yao. Ilionekana hiyo ni hatari kwa kazi kama hospitali na shule zilizotegemea msaada kutoka ng'ambo, hivyo muungano ulisimamishwa.


Lakini madhehebu yaliyoongea hivyo wakati ule yanaendelea kushirikiana katika vyombo vya pamoja kama vile CCT. Wanachama wa CCT ni wafuatao: Walutheri, Waanglikana, Wamoravia, African Inland Church, Wabatisti, Wapresbiteri, Jeshi la Wokovu, Kanisa la Uinjilisti (Mbalizi), pia vyama kama TCRS/Huduma ya Kikristo ya wakimbizi Tanzania.


Ushirikiano umejengwa pia kati ya Waprotestanti na Kanisa Katoliki. Zamani za wamisionari uhusiano huo ulikuwa mgumu mara nyingi. Lakini mabadiliko mengi yamejenga msingi wa uelewano na hali ya kuheshimiana.


Hatua muhimu sana ilikuwa mkutano mkuu wa Kanisa Katoliki duniani ulioitwa 'Mtaguso' wa Pili wa Vatikano miaka 1962-1965. Hapo maaskofu wote chini ya uongozi wa Papa (kwanza Papa Yohane XXIII, halafu Papa Paulo VI) walitamka kwamba Wakristo wote ni ndugu na kwamba kujenga umoja wa Kanisa ni wajibu wa kila mmojawao.


Leo hii makanisa ya CCT na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hushirikiana katika shughuli mbalimbali kama Baraza la Kikristo la Afya Tanzania (Tanzania Christian Medical Board) au katika kuandaa mafundisho ya pamoja katika elimu ya Kikristo mashuleni.


Chama cha Biblia ni chombo kingine cha ushirikiano wa kimadhehebu. Chama hicho kina kazi ya kutoa Biblia kwa bei nafuu kwa watu wengi. Kinasimamia tafsiri ya Biblia katika Kiswahili cha kisasa na lugha nyingine za kikabila. Kinaandaa matoleo mapya ya Biblia na misaada ya kuielewa kama 'Itifaki ya Biblia'.


Pamoja na kwamba sasa Tanzania zipo dini au madhehebu mengi ya dini mbalimbali, lakini msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kwamba inathamini na kuheshimu sana dini na madhehebu yote ya dini zote,  hata hiv msimamo mkuu wa Tanzania ni kwamba Serikali haina dini rasmi kwa hiyo Katiba ya Tanzania inatoa uhuru wa mwananchi kuabudu dini aitakayo au kuwa mpagani, na serikali inaheshimu haki hii kwa vitendo.

***

Mpendwa Msomaji, Hayo niliyotanguliza kuandika mwanzoni mwa makala hii hadi kwenye 'paragrafu' hii, nimeyaandika kwa minajili ya Utangulizi tu kwa kuwa siyo lengo langu kuu kueleza kwa undani dini zilivyo maana mimi siyo mtaalamu mbobefu katika Uwanda huo kitaaluma, isipokuwa tu ninayaelewa kwa kuwa yapo. Lakini kusudio langu  ni kujaribu kuelezea kuhusu Kanisa mojawapo lililopo hapa nchini, ambalo kwa mtazamo wangu naliona kuwa ni Kanisa la 'kipekee' kulinganisha na Makanisa au madhehebu mengine ya dini niliyobahatika kuyafaham. Kanisa hili linaitwa Kanisa Halisi.


Kanisa hili Makao yake Makuu yapo Tegeta Namanga, nje kidogo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi na Vituo vyote vya Kanisa hilo vilivyopo ndani na nje ya Tanzania anaitwa kwa jina Baba Halisi. Kwa mujibu wa Kanisa hilo neno Uzao linamaanisha ni wafuasi au waumini na Baba Halisi siyo cheo bali ndilo jina halisi la Kiongozi wa Kanisa hilo, na bila shaka kuhusu neno 'Halisi' kila mswahili anajua maana yake, yaani 'Orijino', 


Kwanza nitangulie kukiri kuwa mimi si mfuasi wa Kanisa hili, lakini kwa mda mfupi wa takribani miaka miwili niliyokuwa nasogeleana na Kanisa hili, hakika nimekuwa nikivutiwa na mwenendo wa jinsi viongozi na waumini wa Kanisa hilo, tangu  muonekano na utendaji ibada na falsafa za misingi ya ibada za Kanisa hilo.


Mambo hayo ni mengi, lakini zaidi ni jinsi Viongozi na waumini wa Kanisa hili wanavyofanya ibada zao huku wakionyesha dhahiri kwamba ni Wazalendo kwa nchi yao ya Tanzania na pia wanaonyesha dhahiri kuwa na upendo wa dhati kwa  viongozi wa nchi hususani Mkuu wa Nchi yaani Rais na Wasaidizi wake.


Katika siku nilizowahi kuingia kwenye Ibada za Kanisa hilo kwa shughuli zangu za kikazi, sikuwahi kutoka bila kusikia wakimpongeza Rais kwa Uchapakazi wake na kwa Uongozi wake ulio makini. Mfano ni Wakati Kanisa hilo lilipokuwa likifanya uzinduzi wa Kitabu walichokiita "Ufahamu Ulioanzia Tanzania kwenda Katika Mataifa Mengine'.


Katika Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Makuhani wa Kanisa hilo kutoka hadi nchi za nje, nilishuhudia kila Kuhani aliyepanda Jukwaani akimtaja Rais Dk. Magufuli (ambaye sasa ni Hayati) kwa sifa njema zilizotukuka, akielezewa kuwa ni Kiongozi aliye na roho wa Mungu ndani yake na kwamba ndiyo maana humtanguliza Mungu kwenye kila jambo analofanya.


Lakini mbali na hivyo, viongozi na waumini wengi wa Kanisa hili, kila kwenye ibada zao kuonyesha Uzalendo na Utaifa kwa Nchi yao, kwa kuvaa skafu au beji zenye rangi za Bendera ya Taifa la Tanzania au hata kuwa na kitambaa mkononi chenye rangi za Bendera hiyo, jambo ambalo binafsi sijawahi kuliona kwenye ibada ya Kanisa au dini yoyote ukiacha Kanisa Halisi la Mungu Baba. 


Nilipomuuliza Baba Halisi kisa cha waumini kufanya Ibada wakiwa na Skafu na beji zenye rangi za a Bendera ya Taifa alisema, "Tunafanya hivi kwa sababu tumefundishwa kwamba moyo wa Kanisa na Taifa ni Mmoja".


Jambo lingine ambalo nimevutiwa na Kanisa hilo japo siyo kwa imani bali kwa uhalisia na tafsiri ya akili na macho, ni namna ya uvaaji wa Viongozi na waumini wa Kanisa hili ambapo wote, wake kwa waume, wakubwa kwa watoto huvaa mavazi masafi meupe. Najua  lazima wanayo sababu ya kiimani inayowafanya kuvaa namna hiyo, lakini kwangu naliona ni jambo ambalo kwanza linawafanya wote kuwa wasafi na nadhifu wakati wote, linawafanya wajione wote wapo sawa au kitu kimoja, lakini pia kwa anaye waona katika mavazi hayo yanamfanya aone hakuna aliye na hali bora au duni kimaisha kuliko mwenzake..


Lakini jambo lingine ukiacha hilo la mavazi, Kanisa Halisi ni Kanisa ambalo linahimiza kila mtu kuzalisha mali kwa kutumia vyanzo alivyo navyo, badala ya kusubiri hali bora ya maisha kupitia miujiza.


Himizo hilo limenivutia kwa kuwa ni miongoni kwa kaulimbiu za mwanzo za aliyekuwa Rais Rais Dk. John Magufuli za 'Hapa Kazi Tu' ambazo bila ubishi zimesaidia Watanzania kujituma zaidi kufanya kazi, hali ambayo inaifanya Nchi sasa kuonekana kupiga hatua kimaendeleo katika nyanja mbalimbali za Kiuchumi, Sasa kaulimbiu hiyo chini ya Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan ni 'Kazi Iendelee'.


"Kanisa Halisi tunahimiza hivi kwa sababu hili linathibitishwa na Sauti inayofundishwa kila siku inayoonyesha wazi kuwa Mungu Baba alikusudia asiwepo maskini hata mmoja. Ndiyo maana Kauli Mbiu ya Kanisa inasomeka hivi:- 

1. Utawala wa Amani (Isaya 2:4); 

2. Upendo Usiobagua (1Wakorintho 13:13 (c); 

3. Kuzalisha kwa kuanza na ulichonacho (Mwanzo 2:15)", alisema Baba Halisi nilipotaka kujua kwa nini Kanisa hilo linahimiza sana watu kufanyakazi na kuhimiza Upendo na Amani.


Kuhusu malengo na mwelekeo wa Kanisa Halisi alisema Baba Halisi wa Uzao: "Baada ya aliyepokea Sauti ya Saba, kumpisha Mungu Baba, Dira ya Kanisa anayo Mungu Baba Mwenyewe.  Maana kwa mujibu wa Isaya 57:15 sasa Mungu Baba anaishi ndani ya Moyo wa kila mmoja anayemkubali. 


Kanisa hilo linayo mengi ya kuandika, lakini kwa kumalizia, Tafadha soma kwa utimilifu aliyoandika Baba Halisi mwenyewe kulitambulisha Kanisa hilo

Soma Hapo👇


UFUNGUO:

Katika Kitabu, kuna Mfululizo wa Sauti Kuu Saba za MUNGU BABA kama ifuatavyo:

(1)  Kerubi (Ezekiel 28:15);

(2) Adamu wa Kwanza (Mwanzo 2:15);

(3) Musa (Kutoka 3:1);

(4) Eliya Mtishibi (1Wafalme 17:1);

(5) Yesu (Matendo ya Mitume 10:38);

(6) Eliya Adamu wa Pili (Yohana 9:7); na

(7) Miaka 1000 (Isaya 33:6).

Kwa mujibu wa Luka 13:6-7, Waliotumwa wote saba walifanya kazi kwa miaka mitatu peke yake. Hata Musa ambaye imeandikwa kuwa alifanya kazi kwa muda wa miaka 40, mbele za MUNGU BABA ni miaka mitatu peke yake kwa maana ya tangu alipopokea torati na wakati alipopiga mwamba mara mbili. Miaka 1000, alimpisha MUNGU BABA ili yeye ndiye aongoze Kanisa, baada ya kuona wote waliomtangulia waliishia njiani.


Kanisa Halisi la MUNGU BABA lilikuja baada ya Sauti saba  kumaliza majira yake. Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya hizo Sauti Saba, iliyosikika wakati wa Hija ya pili Mjini Kigoma Lango la 26Thebeti,1 (25 Mei 2019), ndiyo iliyokuja kulisimamisha Kanisa Halisi la MUNGU BABA zaidi. Aidha, Sauti Mpya ndiyo iliyosimamisha Tanzania kuwa Taifa Baba na Bara la Afrika kuwa Bara la Nuru, tofauti na lilivyokuwa linajulikana zamani kuwa ni Bara la giza. Pia, Sauti Mpya ililivusha Kanisa KORONGO la giza kwa mujibu wa 2Wakorintho 4:6. Korongo hilo ambalo liko baada ya kitabu cha Ufunuo wa Yohana (ambacho ndicho kitabu cha Mwisho katika Mfululizo wa orodha ya vitabu 66 vya Biblia),  waliotumwa wote, kama walivyoorodheshwa pale juu hawakuweza kulivuka. Hata aliyewateka ambaye anajulikana kama ishara ya kwanza Mbinguni kwa mujibu wa Ufunuo 12:1, hawezi kulivuka. Huyu ishara ya kwanza ndiye aliyeanzisha ugonjwa wa corona. Kwa kuwa Taifa la Tanzania liko Ng’ambo ya KORONGO la giza, ameshindwa kuruka kuleta corona Tanzania. Maana yeye mwenyewe  haruhusiwi kulivuka hilo KORONGO ambalo watanzania tumevushwa kwa upendeleo wa MUNGU BABA.

Sasa kuna Sauti ya Moyo ambayo ndiyo imesababisha kutimia alichosema Yesu katika Mathayo 21:43, zaidi ya Miaka Elfu Mbili (2000) iliyopita kuwa  Ufalme wa MUNGU BABA utahama kutoka Mashairki ya Kati kwenda Taifa lingine ambalo sasa imejulikana kuwa ni Tanzania.

 

(1)       Chimbuko la Kanisa Halisi la MUNGU BABA

Kanisa Halisi la MUNGU BABA lilitambulishwa kwa mara ya kwanza kwenye Mkutano uliofanyikia Mji mdogo wa Namanga-Tanzania 25 Abibu, 1 (15 Septemba, 2018) mbele ya Vituo vyote vya Kanisa Halisi la MUNGU BABA Tanzania, Kenya na Zambia. Ilikuwa ni Mwaka Mmoja baada ya Nafsi ya Baba, kwa mujibu wa Nafsi Tatu za MUNGU katika 1Yohana 5:8, kuja Juu ya Nchi Mwaka 2017 kupitia Tanzania.

 

Hivyo, Kanisa Halisi la MUNGU BABA limeanzia Tanzania kwa Sauti ya MUNGU BABA Mwenyewe. Wengi wanachanganya Kanisa Halisi la MUNGU BABA na Siloam, bila kujua kuwa kila aliyetumwa  kwa mujibu wa Yohana 9:7 ni Siloam, ikiwa na maana ya dini na dhehebu lolote linalotokana na Kerubi, Adamu, Musa, Eliya Mtishibi, Yesu, Eliya Adamu wa Pili. Ni Kanisa Halisi la MUNGU BABA peke yake ambalo siyo Siloam kwa kuwa limeanza baada ya majira ya wote waliotumwa kwisha. Uthibitisho wa jambo hili ni jinsi Kanisa Halisi la MUNGU BABA tunafanya kazi pamoja na Taifa wakati Musa hakufanya kazi na Mfalme Farao, Eliya Mtishbi hakufanya kazi na Mfalme Ahabu na Yesu hakufanya kazi na Mfalme Herode.

Kanisa Halisi la MUNGU BABA linaongozwa na Sauti ya MUNGU BABA ambayo husikika kila lango (siku) kwa Aliyekusudiwa na MUNGU BABA Mwenyewe. Suala la kuisikia Sauti ya MUNGU BABA siyo geni, maana limeandikwa katika Kitabu sehemu nyingi.  Hata hivyo, dunia na ulimwengu kwa sasa wanapata shida kwa kuwa  hawakudhani kama kuna Mwafrika au Mtanzania anayeweza kuisikia Sauti ya MUNGU BABA kila siku na kufundisha wengine alichosikia kwa ufasaha kisha kukiandika kwenye vitabu.


Ufahamu unaotokana na Sauti hiyo, ulizinduliwa rasmi 26 Eluli, Vol.1 (6 Desemba, 2020)  Uwanja wa Uhuru mbele ya Umma wa  Watanzania na Mataifa yote yaliyoizunguka Tanzania.

 

(2)       Dira ya Kanisa Halisi la MUNGU BABA

Baada ya aliyepokea Sauti ya Saba, kumpisha MUNGU BABA, dira ya Kanisa anayo MUNGU BABA Mwenyewe.  Maana kwa mujibu wa Isaya 57:15 sasa MUNGU BABA anaishi ndani ya Moyo wa kila mmoja anayemkubali. Hili linathibitishwa na Sauti inayofundishwa kila siku inayoonyesha wazi kuwa MUNGU BABA alikusudia asiwepo maskini hata mmoja. Ndiyo maana Kauli Mbiu ya Kanisa inasomeka ifuatavyo katika kipengele kinachofuata.

(3)       Kauli Mbiu ya Kanisa Halisi la MUNGU BABA

1. Utawala wa Amani (Isaya 2:4);

2. Upendo Usiobagua (1Wakorintho 13:13 (c);

3. Kuzalisha kwa kuanza na ulichonacho (Mwanzo 2:15)

 

(4)       Vituo vya Kanisa Halisi la MUNGU BABA

Kanisa lina Vituo kila Mkoa Nchini Tanzania. Aidha, Kanisa lina Vituo katika Mataifa yote yaliyoizunguka Tanzania na Pia lina vituo Marekani na Ujerumani. Wafuasi wengi zaidi ni wale wanaofuatilia masomo kwenye Youtube na Whatsapp kila siku. Msisitizo siyo watu kuwa kwenye majengo, bali ni kukubali msamaha bure wa MUNGU BABA (Isaya 43:25) ili wawe uzao wake. Mfano Tanzania wamefikia 1,000,000; Kenya 30,000; Marekani 10,000 na kadhalika ila hawako ndani ya majengo. Wafuasi wa aina hii wako katika mataifa karibu 130. Wanatafsiri kiswahili kwa lugha zao kwa kuwa wanapenda kujua unawezaje kuisikia Sauti ya MUNGU BABA na kuifundisha kwa wengine.

 

(5)       Mwelekeo wa Kanisa Halisi la MUNGU BABA

Kila Mwezi Mataifa yaliyopokea Ufahamu huu wanakuja mara moja Makao Makuu ya Kanisa Halisi la MUNGU BABA, Tegeta Dar Es Salaam Tanzania, kuhudhuria Ibada kwa mujibu wa Isaya 66:23.  Aidha, Kila Mwaka wafuasi ndani na nje ya Tanzania wanakwenda Hija Mkoani Kigoma, kwenye chanzo cha Sauti ya MUNGU BABA. Mafundisho yanafika katika mabara yote saba kwa mujibu wa takwimu za YouTube.

Kila Taifa kwa kadri wanavyoendelea kujua kiswahili watakuwa na vituo, ingawa msisitizo ni kuwa, Uzao wa MUNGU BABA hata kama hauko Kanisa Halisi la MUNGU BABA, kama ambavyo watanzania wote wamejikuta ni chanzo cha Baraka ingawa si wote wako ndani ya Kanisa Halisi la MUNGU BABA. HERI ULIYEBARIKIWA NA MUNGU BABA KULIKO WOTE.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi na Vituo vyote vya Kanisa hilo Ndani na Nje ya Tanzania Baba Halisi.

7 comments:

  1. Imekuwa kubwa MUNGU BABA NI MWEMA

    ReplyDelete
  2. Nashukuru kwa makala hii nzuri hata mimi ni mmojawapo wa makuhani wa kanisa hilo

    ReplyDelete
  3. Nimebarikiwa sana na Mungu Baba. Matendo 4:12; Efeso2:13,20-22; Wafilipi2:9-11; ufunuo 22:13,17-20
    Nimeandika haya juu munieleweshe vizuri maana sijaona Yesu Kristo akiinuliwa na Kanisa la Mungu Baba.

    Je, Yesu ni Bwana na Mwokozi katika kanisa la Mungu Baba? Au Yesu kristo ni nani kwenu?
    Heri heri heri imekuwa.

    ReplyDelete
  4. SWALI, sisi watu wenye tuko mbali na Tanzania na Hatuko wa Tanzania chama cha siasa kitakuwa na manufaa gani kwetu sisi ambao Kristo akitujalia Tutajiunga na kanisa la Mungu Baba?

    2. Chama cha mapinduzi kina usiano gani na kanisa la Mungu Baba Halisi maana wengi waliomo kwenye CCM wa moja ni waeslam,wengine wasio Mcha Mungu Muumba wa Mbingi na nchi pia wale walio kwenye vyama vingine tofauti na CCM muna wasaidia je? Asanteni.
    HERI HERI IMEKUWA.

    ReplyDelete
  5. Nimeyasoma maelezo yenu lakini nimeiona ni ujumbe wa mpinga kristo kuweni makini sku za mwisho mafundisho Kama haya yalitabiliwa.

    ReplyDelete
  6. Tuliza kichwa utaelewa nn mwandishi kaandika...ukikurupuka matokeo yake utapinga..

    ReplyDelete
  7. Tuliza kichwa utaelewa nn mwandishi kaandika...ukikurupuka matokeo yake utapinga..

    ReplyDelete

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages