LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 22, 2017

WAWILI JELA MIAKA 22 KILA MMOJA KWA DAWA ZA KULEVYA


Na Mwandishi Maalum
Abbas Kondo Gede na  Albeto Mandes wamehukumiwa kwenda jela miaka 22 kila moja kwa  kosa la   kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Cocaine na Heroin.

Washitakiwa hao ambao walitenda makosa yao kwa nyakati tofauti wamehukumiwa pia kulipa faini ya jumla ya  shilingi  320.7 milioni.

                Hukumu  ya Abbas Kondo  Gede   ya kwenda jela  miaka 22 na  kulipa faini ya  jumla ya shilingi  175,764,000/=  imetolewa  leo  (  Jumatano)   na   Mhe. Jaji   Korosso baada  ya kujiridhisha  pasipo shaka kwamba, mshtakiwa alikuwa na   hatia ya kujihusisha na  biashara ya dawa za kulevya.

Abbas Kondo Gede  mtanzania, na  mkazi wa  mtaa wa Lindi, Wilaya ya  Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na ambaye  alikuwa ni mcheza mpira wa miguu.  Alikamatwa tarehe 14/5/2011 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akitokea  Sao Paulo, Brazil,  kwa usafiri wa  Shirika la  Ndege la Quater akiwa na   kete 77 sawa na  gramu 1,171.75  za   cocaine   zilizokuwa na thamani  ya   shilingi  58,588.000/= milioni.

Kesi ya  Abbas Gede iliendeshwa na   Mawakili wa Serikali  Batilda Mushi na Frank Tawala ambapo katika  maelezo yao waliiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na  biashara hiyo haramu.
 Kwa upande wa  Albeto Mendes ambaye ni  raia wa Guinea  Besau yeye alikamatwa  tarehe 15/4/2012 katika  Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere akiwa na    gram 1,277.41 za Heroine  zilizokuwa na thamani ya   shilingi  milioni  57,483.000/= akiwa katika harakati  za kusafiri   kwenda  nchini Mali.
 Hukumu ya Albeto  Mendes  ya kwenda jela miaka 22 na kulipa faini  ya shilingi  144,955,700/= imetolewa leo  ( jumatano) na Mhe.  Jaji Mfawidhi Matogolo baada ya  kujiridhisha pasipo shaka kwamba mshtakiwa alikuwa na hatia.
 Mawakili wa Serikali  walioendesha kesi hiyo na kuiomba  Mahakama kutoa  adhabu kali  walikuwa ni    Joseph Maugo ambaye ni  Wakili wa Serikali  Mwandamizi na  Wakili  Clara Chalwe.
Imetolewa na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam
20/9/2017


No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages