Wednesday, May 17, 2017

HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO YAJENGA VYUMBA 60 VYA MADARASA VITAKAVYOGHARIMU MIL.840

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo wa kushoto akimwongelesha jambo diwani wa Kata ya Mapinga ,Ibrahim Mbonde wa katikati aliyevaa kibagharashia ,wa kwanza kulia ni mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alhaj Majid Mwanga.
 Baadhi ya wananchi Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo wakimsikiliza mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo baada ya kutembelea ujenzi wa madarasa sita ,shule ya msingi Kimele .(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani,inaendelea na harakati za kukabiliana na tatizo la upungufu wa madarasa ambapo kwasasa inajenga vyumba 60 vitakavyogharimu sh.mil.840.
Kufuatia hatua hiyo mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Majid Mwanga,amechangia mabati 2,000 na mifuko ya saruji 1,000 ili kusaidia tatizo hilo.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Bagamoyo,Ally Ally Issa,wakati mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,alipotembelea shule ya msingi Kimele,kata ya Mapinga kujionea hali ya ujenzi inavyoendelea.
Ally Issa alifafanua wamejipanga kuondoa uhaba wa madarasa ambao bado upo katika shule za msingi na sekondari.
Alieleza kuwa vyumba vya madarasa vinavyojengwa katika maeneo mbalimbali ya kata zilizopo kwenye halmashauri hiyo ,vipo hatua mbalimbali ya ujenzi.
Nae diwani wa kata ya Mapinga,Ibrahim Mbonde,alisema kata hiyo inatekeleza miradi mitatu ya maendeleo.
Alieleza,miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule ya msingi Udindivu, vyumba vinne vya madarasa S/M msingi Kimele na zahanati ya Tungutungu.
Mbonde alisema,wananchi tayari wamechangia asilimia 50 kwa kujitolea fedha na nguvu ambapo kampuni ya Simba Motors imetoa eneo la heka 20 kati ya hizo heka tano zinatumika kwa ujenzi wa shule na heka 15 huduma nyingine za jamii.
“Tumekubaliana kila kaya kuchangia sh.20,000 na hadi sasa tumeshapata zaidi ya sh.mil 46 na bado tunaendelea kuchangishana ili kufikia malengo”alisema Mbonde.
Mbonde alielezea kwamba,katika ujenzi wa S/M Kimele bado zinahitajika sh.mil 10.6 ili waezeke,S/M Udindivu mil.10.22,zahanati ya Tungutungu inahitajika mil.9.12.Diwani huyo wa Mapinga,alisema,kata ya Mapinga itakuwa na jumla ya shule nne za msingi mara baada ujenzi wa hizo mbili kukamilika.
Aliwashukuru wadau wa maendeleo katika kata hiyo akiwemo mzee Hamoud Jumaa kwa kutoa hekari tano na kiwanda cha kusindika matunda cha Elven Agri co.ltd kinachowajengea madarasa mawili katika shule ya msingi Kimele.
Kwa upande wake ,mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Ndikilo,alichangia sh.mil. moja ili kuunga mkono juhudi za wananchi.
Alibainisha kuwa,shule hiyo inatarajia kusajiliwa mapema baada ya ujenzi kukamilika hivyo itawapunguzia kero ya mlundikano madarasani wanafunzi wa shule ya msingi Mtambani.
Mhandisi Ndikilo alielezea,shule hiyo kwasasa inahemewa na wanafunzi 2,400 hivyo endapo shule ya msingi Kimele ikianza baadhi ya wanafunzi wa Mtambani watahamia shuleni hapo.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Mwanga ,alichangia mifuko ya saruji 125 na mabati 60 katika shule ya msingi Kimele ili kuongeza nguvu.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.