Tuesday, March 7, 2017

HOJA MTAMBUKA: JIBU KWA MBUNGE MSIGWADk. Magufuli hajatia hofu watu isipokuwa
amevuruga uzushi na uongo wa wapinzani

Ø Ni udanganyifu pia kudai kuwa eti haiamini CCM

Na Charles Charles

KATIKA mahojiano yake na gazeti moja litolewalo kila siku nchini yaliyochapishwa hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Kanda wa Nyasa, Peter Msigwa alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Rais Dk. John Magufuli imewafanya watu kuwa na hofu wakati wote.

Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini alisema katika upande mwingine, Rais Magufuli akiwa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho hakiamini ingawa ndiye kiongozi wake mkuu!

“Mwalimu (Julius Kambarage) Nyerere (aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza) hakujenga majengo, lakini fikra zake zinadumu mioyoni mwa watu”, alisema kiongozi huyo wa Chadema ambapo, kanda anayoiongoza inaundwa na mikoa minne ya Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Alisema kutokana na kutoiamini kwake CCM, Rais Magufuli amefanya mabadiliko ya Katiba ili kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao vya juu na kuongeza: “Anafanya vitu vinavyotofautiana na Chama Cha Mapinduzi”.

Labda nianze kwa kukiri kuwa namfahamu vizuri Peter Msigwa kama Mbunge wa Iringa Mjini, na pia akiwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya hiyo kipindi kile maana niliishi katika jimbo hilo kwa miezi 10 mwaka 2011 nilipohamishiwa huko kikazi.

Naujua udhaifu wake kama mwakilishi wa wananchi bungeni, mahusiano yake na wapiga kura wa jimbo hilo na chuki zake kwa CCM, serikali yake na viongozi wake na hata yeye mwenyewe katika upande wa pili ananifahamu vizuri mpaka kunichukia.

Naujua uwezo wake mkubwa wa kutengeneza uzushi ama uongo wowote wa kisiasa anapodhani unaweza kukisaidia chama chake au hata mwenyewe, halafu yupo radhi na tayari kufanya hivyo wakati wowote, mahali popote au kwa namna yoyote ile dhidi ya CCM, serikali na hata viongozi wake anapokuwa akiamini kufanya hivyo kutaudhalilisha upande huo ambao kwake na Chadema yake ni kama adui namba moja na hatari zaidi.

Wakati aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipowasili Iringa mwezi Mei, 2011, Msigwa alipokwenda katika vikao vya bunge la bajeti ya mwaka 2011/2012 alipeleka uongo uliowaacha wananchi wa jimbo hilo wakipigwa bumbuwazi na kile alichozungumza kwa nguvu zake zote kinywani mwake!

Katika uongo huo, mbunge huyo alidai siku ambayo Kiwete aliwasili Iringa, barabara inayotokea Uwanja wa Ndege wa Nduli kwenda katikati ya mji huo ilifungwa kutwa nzima kutoka saa tano asubuhi hadi saa 11 jioni ili kusubiri kiongozi huyo kwanza apite.

Msigwa aliyekuwa akiongea bila aibu usoni wala haya kinywani, alisema hatua hiyo aliathiri biashara pamoja shughuli nyingi zinazofanywa na wananchi wa jimbo hilo na sehemu nyingine.

Lakini katika ukweli halisi, Kikwete ambaye aliwasili majira ya saa 12 za jioni na kulala kwa siku moja katika Ikulu Ndogo mjini hapo akiwa njiani kwenda Njombe, kuhudhuria mazishi ya marehemu mama yake mzazi na aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda alitumiwa kutengenezea uongo wa asilimia 100 na mtu huyo.

Nasema hivyo kwa sababu nilikuwepo katika mji huo kabla, wakati akiwasili na baada ya kuondoka kwake kwenda Njombe, na pia nilikuwepo aliporudi tena na alipopanda ndege kutoka Iringa kuelekea Dodoma kesho yake, saa 11.30 jioni.

Hakuna barabara iliyofungwa na polisi eti kutwa nzima ili kupisha msafara wa Kikwete upite. Kilichofanyika ni itifaki ya kawaida sehemu zote duniani ya kuipisha misafara yote ya viongozi wakuu wa kitaifa wanapopita, hivyo hata siku hiyo jambo hilo halikufanyika kabla na baada ya kupita kwake.

Kilichofanywa na polisi ni kusimamisha magari yote barabarani wakati msafara wake ulipoanza kutoka katika uwanja huo wa ndege kuelekea mjini, halafu njia zote ambazo zilifungwa kwa ajili hiyo hakuna iliyochukua angalau zaidi ya dakika tano tu.

Baada ya kurejea kwake jimboni na kukuta wananchi wamekereka, Msigwa alipokwenda katika vikao vingine vya bunge alitengeneza uzushi mpya na safari hii dhidi ya kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM kwa kumhusisha na biashara haramu ya nyara za serikali.

Alifanya hivyo huku akijua na kuamini kwamba anadanganya kwa asilimia 100, lakini kwa sababu ndio mfumo wake mwenyewe wa kisiasa na staili ya chama chake kutafuta wanachama, wafuasi na mashabiki bila kujali uharamu wake, Msigwa alisema hayo kwa nguvu zake zote mdomoni ingawaje alishindwa kuthibitisha popote hadi leo kwa sababu ulikuwa ni uzushi uliovuka mipaka.

Ndiyo maana hivi leo tena amekuja na uzushi, uongo na upotoshaji mwingine dhidi ya CCM, serikali na Rais Dk. John Magufuli kwa vile kufanya hivyo kwake ni kama jadi yake ya siku zote katika maisha yake ya kisiasa.

Hata anapoitwa mchungaji, neno ambalo lina maana ya kiongozi wa kanisa kuna wakati huwa ninajiuliza sana kiasi kwamba naona waumini wake wana mioyo iliyojaliwa ujasiri. Nawaona ni watu wanaostahili kupewa tuzo ya kuheshimu uvumilivu wao wa juu kabisa kwa sababu ya kukubali kusimamiwa kiroho na kiongozi wa aina ya Msigwa.

Leo anapokuja na uzushi eti kwamba Serikali ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Rais John Magufuli imewatia watu hofu ni kauli ambayo, kwa namna zote inaweza tu kutolewa na kiongozi wa kisiasa asiyeona aibu kusema uzushi wowote.

Ni Mtanzania gani aliyetiwa hofu na serikali hiyo ya sasa na kutokana na nini? Wapi alikokwenda na kuambiwa na wananchi kwamba wanaishi kwa wasiwasi?

Nafahamu kuwa kauli yake hiyo inatokana na uzoefu wa uongozi alioupata katika chama chake, kwamba ili uonekane kiongozi mzuri ni lazima uwe na sifa zenye ukakasi.

Mtu anayetaka kuwa kiongozi anayekubalika ndani ya Chadema lazima awe mzushi sana, muongo sana, mpotoshaji sana, mchonganishi sana, mchochezi sana na ambaye wakati wote na mahali popote awe radhi na tayari kusema chochote au lolote hata kama anaamini kwamba anaweza kusababisha umwagaji wa damu.

Hizo ndizo sifa anazopaswa awe nazo pia Msigwa akiwa ni kiongozi mwandamizi wa Chadema ambako ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa minne ya Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma; halafu ni mbunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama chake hicho.

Bila shaka analazimika kuwa na sifa hizo kwa sababu anapaswa kutekeleza matakwa ya kisiasa ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Freeman Mbowe ambaye tangu achukue wadhifa huo mwaka 2004 ameigeuza Chadema kutoka chama makini cha siasa hadi cha kiharakati zaidi katika shughuli zake zote.

Sina hakika sana na madai kwamba wafuasi wengi wa Chadema wakiwemo walioshiriki kufanya vurugu za Januari 21, 2011 kule Arusha hununuliwa ama kunyweshwa pombe ya aina ya viroba ili wapate kile kinachoitwa “stim”, na kwamba wakishakunywa ndipo sasa wanaingia barabarani ama kuandamana kwa kauli za ama zao ama za wale waliotumwa kwenda kuwafanyia fujo kwa jinsi wanavyoweza.

Hao ndio inawezekana hata Msigwa naye alilenga kuwadanganya kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imewafanya watu kuwa na hofu kwa sababu, washirika wa kundi hilo hawana utamaduni wowote wa kujiuliza, kuhoji wala kuomba ufafanuzi wa jambo lolote linalopandikizwa kwa nia mbaya akilini au vichwani mwao. 

Wao siku zote wanafanya au kutekeleza chochote wanachotumwa wafanye, hivyo hata wakiambiwa kwa mfano kwamba wakaharibu mali zao wenyewe kama nyumba zao, mashamba yao na hata vinginevyo ili isingiziwe serikali wataitikia “people’s power”, kisha wataingia barabarani na kufanya lolote lile kwa sababu wana hamasa ya viroba vya pombe ila bahati mbaya sana hatimaye vimepigwa marufuku.

 Kuhusu mfano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba “hakujenga majengo, lakini fikra zake zinadumu mioyoni mwa watu” kinyume na utawala wa sasa kwa hakika huo ni uelewa mdogo.

Katika uongozi wake wa miaka 23 akiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, mwasisi huyo wa taifa hakuwahi kuongoza nchi kinyume cha sheria na Ilani ya CCM au TANU iliyoishia mwaka 1977.

Alikuwa akiongoza serikali inayotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya TANU na kisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Alikuwa akiongoza serikali inayotokana na chama cha TANU, CCM na sera za vyama hivyo vyenyewe.

Hakuwahi hata siku moja kuongoza serikali iliyotokana na chama kingine chochote cha siasa isipokuwa hivyo viwili, kila kimoja kwa muda wake na hivyo hawezi akaangaliwa, kupimwa wala kufanyiwa tathmini ya uongozi kwa kutumia jina lake au sura yake binafsi isipokuwa Sera na Ilani za Uchaguzi za TANU na CCM.

Katika hali hiyo, Msigwa anapokuja na kauli inayohusu uongozi mahiri au makini wa Baba wa Taifa ajue kuwa anaongelea Sera, Ilani za Uchaguzi na serikali za TANU ama CCM na siyo vinginevyo.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa pia kwa Serikali ya Awamu ya Pili, Serikali ya Awamu ya Tatu na Serikali ya Awamu ya Nne. Zote zilikuwepo madarakani na kuongozwa na Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kwa kutekeleza Ilani za Uchaguzi na Sera za CCM kama ilivyo sasa kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Kuhusu madai kuwa eti Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM hakiamini chama hicho nao ni upuuzi unaopaswa kutupiliwa mbali na kupuuziwa huko.

CCM kama chama cha siasa, kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayotumika sasa kina Katiba yake ambapo, yeye mwenyewe ni mmoja kati ya maelfu ya wanachama wake waliopo nje na ndani ya nchi hii.

Aidha, Ibara ya 7 ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 inayotumika hivi sasa nayo inasema: “Raia yeyote wa Tanzania mwenye umri usiopungua miaka 18 anaweza kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi iwapo anakubali imani, malengo na madhumuni ya CCM” (mwisho wa kunukuu).

Kama kifungu hicho cha Katiba ya CCM kinaeleza hivyo na Rais Magufuli akiwa mwanachama wake hivi hata kwa akili ndogo ya kisiasa ya Msigwa, ufahamu mfupi na hata vinginevyo inawezekanaje awe hakiamini chama chake wakati “anakubali imani, malengo na madhumuni” yake?

Sikubaliani pia na madai ya kipuuzi ya kiongozi huyo wa Chadema anapodai kuwa Rais John Magufuli “anafanya vitu vinavyoofautiana na Chama Cha Mapinduzi”. Mbona hakuvitaja ili pia watu wengine nao wavielewe na kupima ukweli wake, uzushi, uongo ama upotoshaji unaotaka kupandikizwa ili kukidhi matakwa yake ya kisiasa?

Katika kuthibitisha uongo wa Msigwa, Ibara ya 4 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 inasema ifuatavyo:

“Katika miaka mitano ijayo (kwa maana ya kuanzia mwaka 2015 – 2020), CCM ikiwa madarakani itaielekeza serikali yake kutumia nguvu zake zote kuendelea kupambana na changamoto kubwa nne (ambazo):

“Kwanza ni kuondoa umasikini, pili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na hasa kwa vijana, tatu kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma na nne, kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao”.

Aidha, Ibara ya 12 ya Ilani hiyohiyo inasema lengo la mapambano dhidi ya rushwa ni “kuziba mianya ya rushwa katika taasisi za umma, kuchukua hatua kali na za haraka kwa wote watakaobainika kuendeleza rushwa serikalini na katika sekta binafsi, kuimarisha vyombo na taasisi zinazohusika na kuzuia na kupambana na rushwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mahakama Maalum kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi”.

Nayo Ibara ya 13 ya Ilani hiyo inasema “sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, serikali pia itatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuchelewesha kutoa maamuzi yenye maslahi kwa umma na kusimamia uwajibikaji katika kutekeleza masuala yenye maslahi kwa umma”.

Kutokana na hali hiyo na kulinganisha na yale yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano akiwemo Rais John Magufuli binafsi, hivi unawezaje kuja na udanganyifu kwamba haiamini CCM na kuwa eti anafanya vitu vinavyotofautiana na chama hicho?

Baada ya haya yote ninaomba sasa nibainishe ukweli kuwa Rais John Magufuli hajawatia hofu watu katika utekelezaji wa kazi zake, utendaji wa serikali yake na hata vinginevyo, bali alichofanya ni kuvuruga mianya ya wapinzani iliyotumika kufanyia uzushi na uongo kwa muda mrefu.

Safi sana!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam

Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.