Wednesday, September 21, 2016

MAKALA:RAIS MAGUFULI NA KASI YA UKUAJI WA UCHUMI.

Image result
RAIS JOHN POMBE MAGUFULI

Na:Nassir Bakari

Mijadala mingi mitandaoni na sehemu mbalimbali kwenye mikusanyiko ya watu kwa siku za hivi karibuni ni kuhusu uchumi wa Tanzania na wanasiasa wengi kwa makusudi kabisa tena bila aibu wanawahadaa wananchi kwa malengo yao binafsi ikiwemo kisisasa, wanasema uchumi wa nchi umeshuka na wananchi wengi bila kufahamu wamekuwa wakiitupia lawama serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, ukweli uliopo ni kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka mara dufu.

  Wanasiasa wengi wa upinzani wanasema uchumi wetu umedorora bila kuainisha sababu ama vyanzo vinavyooneshahali hiyo,kitu ambacho kimekuwa kikiwachanganya wananchi  ambao wanategemea taarifa sahihi kutoka kwa viongozi wao.

   Wengi kwa kukosa hoja wamebaki wakisema  hali ya kupotea kwa pesa mitaani kuwa ndiyo kiashiria kikuu cha kudorora kwa uchumi, la hasha! pesa haionekani mitaani kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya tano kuwapokonya wachache na kuzirudisha serikali kuu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na muda si mrefu zitarejea kwenye mzunguko, sio tena kwa watu wachache ni kwa wote,

  Mbunge wa Kigoma mjini, Zito Kabwe alisema uchumi umedorora sababu yake kubwa ni kutoonekana pesa mtaani, sijajua kama aliuliza kwa wachumi au aliamua aseme kwa sababu zake binafsi ama kwa malengo ya kisiasa au sijui naye ni mmoja wa kundi dogo la watu waliokuwa wananyonya wengi? Hilo mimi sijui.

   Pia Kiongozi wa Kambi Maalumu ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.  alikwenda mbali zaidi kwa kusema deni la taifa limepanda huku akieleza hali ya maisha ilivyozidi kuwa ngumu,  juzi tu nilisoma kwenye gazeti anadaiwa bilioni 1.172 na shirika la Nyumba la Taifa(NHC), sasa sijaelewa alikuwa analalamika mianya yake ya kupiga dili imefungwa? Au sababu za kisiasa.?

UKUAJI WA UCHUMI.

   Wanasiasa  na wachambuzi wengi wamekuwa wakielezea uchumi wa Tanzania, chini ya serikali ya awamu ya tano, wengi wamekuwa wakieleza kiushabiki na wengine kwa ajili ya masilahi yao binafsi ni maoni yangu kuwa tujenge tabia ya kuheshimu na kukubaliana na vitu vyenye hoja za kitalaamu, ni vyema kama huna hoja yenye msingi wa kitalaamu ukae kimya, haipendezi na haikubaliki kukataa au kubeza kitu eti kwa kuwa kitakudhoofisha kisiasa,kimaslahi ama kinamna yoyote.

   Kwa nini wataalamu waliobobea wa uchumi wanasema uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi? sababu zipo nyingi,ila kwenye makala hii nitataja chache:-

    Kwanza, kushuka kwa mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 5.5 Juni mwaka huu na asilimia 4.9 Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 iliyokuwapo Desemba, 2015, sababu zilizochangia kupungua kwa kasi hiyo ya bei ya bidhaa na gharama kuwa ni kushuka kwa bidhaa takribani zote za vyakula na zisizo za vyakula, hali hiyo imeifanya thamani ya shillingi katika manunuzi kuimarika kiasi ambapo kila shillingi mia moja inaweza kufanya manunuzi yenye thamani ya shilingi 96 na kwamba kiwango cha sasa cha mfumuko wa bei hakina tofauti sana na ilivyo nchi nyingine za Afrika MasharikI.

   Pili, ukuaji wa uchumi wa 7% kwa wastani,  unaochochewa na sekta za mawasiliano, fedha, usafirishaji, kilimo, ujenzi, uzalishaji viwandani na uwekezaji kwenye miundombinu.

   Aidha Tanzania imeorodheshwa ya pili kwa kuwa na uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika baada ya Ivory Coast iliyo na ukuaji wa asilimia 8.5.

   Tatu, ukuaji wa pato la Taifa ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka jana.

    Nne, kuongezeka  bajeti ya shughuli za maendeleo Sh 11.82 trilioni, sawa na asilia 40 ya bajeti nzima , zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, katika bajeti iliyopita, matumizi ya kawaida yalitengewa Sh 16.7 trilioni, sawa na asilimia 74.3 wakati shughuli za maendeleo zilipangiwa  Sh 5.76 trilioni, sawa na asilimia 25.

   Tano kukuwa kwa pato la wastani la Mtanzania kutoka Sh. 770,464 mwaka 2010, hadi Sh. 1,918,928 mwanzoni mwa mwaka  2016.

    Sita, kuimalika kwa shughuli za uchumi ambapo mauzo ya nje ya Tanzania yameongezeka kwa wastani wa asilimia 3.3 huku kiwango cha uagizaji bidhaa kikiwa kimeshuka kwa asilimia 0.58.

   Saba,  ongezeko la akiba ya fedha za kigeni limefikia dola za Marekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi minne.

  Nane Uagizaji wa malighafi za viwandani kutoka nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia19.4 na akiba ya fedha za kigeni bado ni nzuri na tarehe  13/9/2016 ilikuwa dola bilioni 4.

UKWELI USIOPINGIKA.

    Maneno mengi yanasemwa mitaani kuhusu kupungua kwa mizigo bandarini ,ni kweli mizigo imepungua kwa kuwa wale ambao walikuwa wanafanya biashara haramu ya kupitisha mizigo bila kulipia hawafanyi tena kwa mfano kuwa na mizigo 40 inalipiwa mizigo minne na kuwa na mizigo 10 na kulipiwa yote kipi bora,? ndiyo mizigo imepungua na mapato kuongezeka maradufu na kuifanya Tanzania kuwa kati ya nchi kumi za Afrika ambazo uchumi wake unakua vizuri.

   Pia  pesa zilikuwa zinamilikiwa na watu wachache ambao walikuwa miungu watu kwa sasa pesa zimehama kutoka kwa wachache wenye mikono haramu kwenda kwenye matumizi halali na sahihi kwa umma.

   Pia kumekuwa na maneno mengi kuwa utalii umepungua, hapana ukweli  ni kwamba Kwa thamani na wingi, utalii umeongezeka, haujapungua, Zanzibar idadi ya ndege zinazoingia na watalii zimeongezeka.

NINI KIMESABABISHA KUPOTEA KWA PESA MTAANI.

    Kupotea kwa pesa kunatokana na Serikali ya Awamu ya Tano kudhibiti makusanyo ya kodi, kuziba mianya mbalimbali ya upotevu wa fedha na kubana kazi zisizokuwa rasmi ‘misheni town’ na fedha hizo kuelekezwa kusaidia umma badala ya kwenda kwa wachache wanaojipatia isivyo halali.

UCHUMI KUENDELEA KUIMALIKA.

    Kauli zinatolewa na wataalamu wa uchumi nchini akiwemo Gavana wa Benki kuu ya Tanzania(BoT) Bw. Benno Ndulu zinaashiria kuwa uchumi wetu unakuwa kwa kasi kubwa na utaendelea kuimalika kwa miaka ijayo kwa kuwa ipo miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kazi siku za usoni ambayo itachangia katika kuimarika kwa uchumi.

Miradi hiyo ipo mingi kwenye makala hii nitaitaja baadhi;-

   Moja, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa ambacho kitakuwa sawa na viwango vya reli za nchi zilizoendelea na kupelekea usafiri wa gari moshi kuwa wa uhakika na salama zaidi

   Pili, ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo litahusu vilevile upanuzi wa bandari ya Tanga,ikumbukwe kwamba bomba hili lilileta taflani kubwa na hatimaye tukafanikiwa kakika hilo.

    Tatu, ujenzi wa eneo la kibiashara, Kurasini itakayokuwa mhimili wa biashara kati ya China na ukanda wa Afrika na kusababisha kuongezeka kwa fedha za kigeni.

   Nne, kuzalisha megawati 240 za umeme wa Kinyerezi II,a zitakazopelekea kupatikana kwa umeme wa uhakika kwa ajili ya kufanyia shughuli za maendeleo na ikiwezekana kuuza nchi za jirani.

   Tano, kupanua viwanja vya ndege nchini lengo likiwa ni kuongezea idadi ya ndege zinazotakiwa kutua na idadi ya wageni kutoka nchi mbalimbali..

   Sita, ujenzi wa maghala ya Taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350, hapa nchi hata iwe na ukame kiasi gani wananchi watapata chakula cha kutosha.

   Saba.  ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza marumaru Mkuranga mkoani Pwani, kitapunguza idadi ya watu wasio na ajira na kupunguza uimasikini..

   Nane, ni ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi kitachotengeneza ajira kwa wananchi na kuongezeka kipato.

  Tisa, kiwanda cha bidhaa za chuma mkoani Pwani ambacho kipo mbioni kukamilika, kitaongeza uzalishaji wa chuma na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje.

   Kutokana na kuwepo miradi  hiyo ni dhahiri kuwa hali ya uchumi nchini ni nzuri na inatoa matumaini makubwa kwamba shughuli halali za kiuchumi zinaendelea kama ilivyotarajiwa hapo awali.

PONGEZI KWA RAIS.

   Kwa juhudi anazozifanya Rais, John Pombe Magufuli  anastahili pongezi kutoka kwa  watanzania  kwa maana anapambana usiku na mchana  na  wanaofanya ubadhilifu wa mali za umma tena bila kuchoka na bila huruma kwa mfano kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kwenye taasisi za serikali na kuwaweka kando wote wanaoenda kinyume na maadili ya kazi

TUMUOMBEE.

   Huu  ni msemo maarufu sana anaopenda kuutumia Rais, John Pombe Magufuli, anapohutubia wananchi mpaka imefikia hatua baadhi ya viongozi kuutumia, kwa hakika dua zetu ni muhimu  na zinahitajika ili aweze kupambana na mafisadi na wote wasiopenda maendeleo maana kuna mambo mengi mabaya  yanaweza kufanywa na wanaopinga juhudi zake ili kumkwamisha nia yake ya dhati ya kuwatumikia watanzania.

Mungu ibariki Tanzania.

Mungu mbariki Rais, John Pombe Magufuli.

MUANDAAJI. NASSIR BAKARI
OFISI NDOGO ZA CCM
LUMUMBA
PHONE:0713 311 300
EMAIL: nassiribakari@gmail.com
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.