LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 5, 2016

RAIS DK. MAGUFULI AAHIDI KUJENGA BARABARA YA UBUNGO KIBANGU HADI RIVER SIDE, DAR ES ASALAAM

Na Bashir Nkoromo
Rais DK. John Magufuli ameahidi kwamba Serikali yake itaitengeneza barabara kutoka Ubungo Kibangu hadi Riverside itakayoungana na Barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo na Ikulu, imesema Rais ametoa ahadi hiyo ameitoa kwa waumini wa Kanisa la Maombezi linaloongozwa na Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) lililopo Ubungo Kibangu Jijini Dar es Salaam alipotembelea Kanisa hilo leo Juni 5, 2016.

Imesema, Rais Magufuli ambaye amezungumza katika ibada ya asubuhi ya Kanisa hilo amesema amepita katika barabara hiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na waumini hao na wananchi wengine wa eneo la Ubungo Kibangu kwa lengo la kujionea hali halisi.

Aidha, Rais Magufuli amempongeza Kiongozi wa Kanisa hilo Mchungaji Antony Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako kwa huduma ya maombezi anayoitoa kwa waumini wake na watazamaji wanaofuatilia vipindi vyake vya Mahubiri kupitia Luninga.

“Mimi ni mfuatiliaji mzuri sana wa mahubiri yako, kwa hiyo mahubiri unapoyatoa yanasambaa, kwa kweli mimi na familia yangu huwa yanatubariki sana, kwa hiyo nataka kukuthibitishia ninakupenda sana.

“Ndio maana kuna siku moja, ulizungumza kuhusu shida ya barabara yako ikabidi nitafute mbinu za namna gani tunaweza kuishughulikia kwa utaratibu ulio wazi, nikamtuma meneja wa barabara wa Mkoa wa Dar es salaam, akaja, akaipitia na akafahamu changamoto zilizopo, akafanya upembuzi yakinifu na usanifu, nataka kukuthibitishia kuwa fedha za kutengenezea barabara hii zipo” Amesema Dkt. Magufuli huku akishangiliwa na waumini.

Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa la Maombezi Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) amemshukuru Rais Magufuli kwa kulitembelea kanisa hilo, na amemuombea heri katika uongozi wake ili aweze kufanikisha azma ya kuliletea taifa maendeleo ikiwemo mpango wa kuanzisha viwanda.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages