Wanaosubiri
kuiona CCM inashindwa
kama PDP Nigeria
kwa hakika wanaota
Na Charles
Charles
KUSHINDWA
kwa Rais wa Nigeria katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi Machi 28, mwaka
huu, Goodluck Jonathan, kumeanza kuwaotesha pia ndoto za mchana baadhi ya watu
kwamba eti Chama Cha Mapinduzi (CCM), nacho kitashindwa katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu!
Katika
uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha upinzani cha Alliance
Progressive Congress (APC), Jenerali Muhammadu Buhari alimng’oa Jonathan
aliyekuwa akitetea nafasi hiyo kupitia Chama cha People’s Democratic (PDP) na
kuwapa ndoto za alinacha baadhi ya watu hapa nchini!
Jenerali
Buhari mwenye umri wa miaka 72 sasa anatarajiwa kuapishwa Mei 29, mwaka huu,
kuanza kuiongoza nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu kuliko zote barani
Afrika.
Ili
kuhalalisha ndoto hizo unatolewa mpaka mfano wa mwaka 1991 huko Zambia, wakati aliyekuwa
mgombea urais kutoka chama cha upinzani cha Movement for Maltiparty Democracy
(MMD) ambaye sasa ni hayati, Frederick Titus Chiluba alipomshinda Baba wa Taifa
hilo na mgombea kutoka chama kilichokuwa madarakani cha United National
Independency Party (UNIP), Kenneth Kaunda.
Tunaambiwa
mfano wa aliyekuwa Rais wa Benin, Jenerali Mathieu Kerekou aliposhindwa na mgombea
kutoka chama cha upinzani nchini humo, Nicephore Soglo.
Tunakumbushwa
pia mwaka 2002 wakati aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa vyama vya
upinzani vya kundi la National Rainbow Collition (NARC), Emilio Mwai Kibaki
alipomshinda mgombea kutoka chama cha Kenya African National Union (KANU),
Uhuru Muigai Kenyatta kilichokuwa kimetawala kwa miaka 39 na kuking’oa
madarakani.
Tunaelezwa
kuhusu ushindi wa aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Patriotic Front (PF),
Michael Satta alipomwangusha aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mpito ya Zambia,
Rupia Banda kutoka chama tawala cha MMD, wakati huo.
Unatolewa
mfano wa jinsi aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mpito ya Malawi na kiongozi wa
Chama cha United Progressive (UPP), Dk. Joyce Banda alivyoshindwa na aliyekuwa
kiongozi wa upinzani kutoka Chama cha Democratic Progressive (DPP), Profesa Peter
Mutharika.
Pamoja
na ukweli huo wote, lakini hatuelezwi namna kiongozi huyo wa sasa alipoifikisha
nchi hiyo katika hali mbaya kabisa kiuchumi ndani ya miezi tisa tu. Imefikia
mpaka hatua ya kutokuwa na fedha katika Benki Kuu yake zinazotosha angalau kwa
matumizi ya wiki tatu tu!
Tunarudishwa
nyuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kuambiwa kuwa wapinzani walipata
zaidi ya wabunge 80 kati ya 340 waliopo katika Bunge la 10 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, jambo ambalo hata mimi nakubali.
Tunaelezwa
kuhusu ushindi wa CCM wa asilimia 79 katika uchaguzi wa serikali za mitaa,
vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka jana na vyama vyote vya upinzani nchini
kugawana asilimia 21 iliyobaki.
Hiyo
ndiyo mifano inayohalalisha kushindwa kwa CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika baadaye mwaka huu. Hiyo ndiyo mifano inayotumiwa na baadhi ya watu
wakiwemo waandishi wa habari wenye mapenzi yaliyopitiliza katika genge linalojiita
Umoja wa Katiba ya Wananchi, maarufu zaidi kwa kifupi cha Ukawa!
Ili
kuwachochea hasira zaidi wapiga kura watarajiwa katika kinyang’anyiro hicho cha
urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, waandishi hao wa habari wanakwenda mbali
zaidi kwa kusema kuwa “kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Mwaka 2014,
Tanzania sasa ni nchi ya 159 kati ya 187 duniani kwa umasikini!”
Nakubaliana
pia na takwimu hizo kwa vile ni za kweli, lakini sikubaliani kabisa na jinsi
zinavyotumiwa kuwa hoja za kutaka kuhalilishia propaganda na uongo dhidi ya
CCM.
Sababu
kubwa zilizomng’oa Rais Goodluck Jonathan kule Nigeria ni mbili tu: Ya kwanza
ni uwepo wa kundi la kigaidi linaloitwa Boko Haram, na pili ni tatizo sugu la
rushwa inayoshinda nchi zote barani Afrika!
Hayo
ndiyo mambo makubwa yaliyopelekea ashindwe kutetea nafasi hiyo yeye na chama
chake hicho cha PDP, vinginevyo angeshinda na kumalizia muhula wake wa pili
hapo Mei 29, 2019.
Lakini
pia, ushindi mwembamba alioupata Jenerali Buhari kutoka kwa wapiga kura
wanaokaribia idadi ya Watanzania wote waliopo hivi sasa, unatokana na kuwahi
kwake kuitawala nchi hiyo akiwa Kiongozi wa Kijeshi kuanzia usiku wa kuamkia Januari
Mosi, 1984, alipomwangusha Rais Shehu Shagari aliyetarajiwa kuapishwa kwa
muhula wa pili wa utawala wake, siku hiyohiyo.
Buhari
aliiongoza Nigeria kwa miezi 19 na siku 26 kamili kuanzia siku hiyo hadi usiku
wa kuamkia Agosti 27, 1985, wakati naye alipong’olewa kijeshi na Jenerali
Ibrahim Badamasi Babangida.
Katika
hali hiyo, wapiga kura wa nchi hiyo wamemchagua rais huyo wa zamani kwa sababu
wanaujua uongozi wake, lakini pia wamefikia uamuzi huo baada ya awali kumkataa
katika chaguzi tatu za mwaka 2003, 2007 na 2011 na sasa alikuwa akigombea nafasi
hiyo kwa mara ya nne mfululizo.
Walichagua
kile kinachoitwa kwamba “zimwi likujualo halikuli likakwisha”, lakini Jenerali
huyo wa jeshi pia ‘amebebwa’ na utekaji, utesaji na mauaji yanayofanywa mara
kwa mara na kundi la kigaidi la Boko Haram likiongozwa na Abubakar Shekau.
‘Amebebwa’
pia na rushwa iliyokithiri nchini humo ambapo wananchi wanaamini kuwa atatumia mpaka
uzoefu wa kijeshi, ili kupambana na mtandao wa uhalifu huo ambao umekuwa ni
sugu kwa Nigeria kushinda nchi zote barani Afrika. Hizo ndizo sababu kubwa
zaidi na mbili zilizompa ushindi huo mwembamba.
Wanigeria
hatimaye wamechoka kutekwa, kuteswa ama kuuawa kikatili na kundi hilo la
kigaidi kila kunapokucha. Walifika mahali wakaamini kwamba jeshi la nchi hiyo ambalo
Rais Goodluck Jonathan anayemaliza muda wake wa kutawala Mei 29, mwaka huu akiwa
ni Amiri Jeshi Mkuu wa sasa limeshindwa kabisa kudhibiti vitendo hivyo.
Mbaya
zaidi ni habari zinazodai kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali yake wakiwemo
Mawaziri, Magavana wa Majimbo na Majenerali wa Jeshi hilohilo ni sehemu ya
kikundi hicho, hivyo mara zote wamekuwa wakivujisha siri muhimu za mashambulizi
ya kijeshi yanayopangwa ili kukitokomezea mbali.
Wanafanya
kama aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Msumbiji na Naibu Waziri wa Ulinzi,
Jenerali Sebastiao Mabote alivyokuwa pia ni sehemu ya kikundi cha waasi cha
Resistance Nacional de Mozambique (RENAMO), katika miaka ya 1980 kabla
hajagunduliwa na majeshi ya Tanzania yalipokwenda huko kuvisaidia vikosi vya
serikali ya nchi hiyo mwaka 1987!
Ndiyo
maana ili kuondokana na hali hiyo, wananchi wa Nigeria walimnyima kura za
kutosha Rais Jonathan na kumpa Jenerali Buhari.
Walifanya
hivyo pia kwa sababu katika hotuba zake zote wakati wote wa kampeni zake, Buhari
alikuwa akiahidi kwamba kazi yake kubwa ya kwanza akiapishwa tu itakuwa ni kuweka
mikakati madhubuti ya kijeshi ya kuwatokomezea mbali Boko Haram.
Wakiangalia
uzoefu alionao kama Kamanda na Kiongozi Mwandamizi wa Kijeshi, wapiga kura walio
wengi waliona wamchague kusudi awe tena Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya nchi
hiyo, lengo likiwa kumkabidhi jukumu la kuokoa maisha yao yanayozidi kunyemelewa
kila kunapokucha na genge hilo la kigaidi.
Ndiyo
maana ninasema ushindi huo wa Jenerali Muhammadu Buhari kamwe hauwezi ukafananishwa
kwa namna yoyote ile na juhudi zinazofanywa iwe na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Civic United Front (CUF), National League for Democracy (NLD), NCCR
– Mageuzi ama kwa ‘nguvu’ ya pamoja waliyoipa jina la Ukawa.
Hauwezi
ukafananishwa kwa namna yoyote ile na kivuli cha kwamba eti chama kilichopo
madarakani kimeshindwa na wapinzani, hivyo CCM nayo ianze kutia maji ‘kichwani’
kwake.
Haiwezi
kuwa namna hiyo kwa vile kiuhalisi, uchaguzi huo mkuu wa Nigeria kamwe haukuwa
wa kisiasa zaidi isipokuwa wa kutafuta amani ‘iliyoporwa’ na Boko Haram.
Mbali na amani, rushwa iliyopo nchini humo
nayo kamwe haiwezi ikafananishwa angalau tu kwa asilimia 15 na ile iliyopo
Tanzania, Kenya, Liberia, Ethiopia, Togo, Mauritania au Benin na kadhalika!
Kama taifa tajiri zaidi kwa mafuta
Afrika, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu kushinda nchi zote katika bara
hili, mamilioni ya wasomi na kuongoza kwa vitendo vya utapeli duniani; Nigeria ndiyo
pia inaongoza kwa uhalifu huo wa jinai unaoitwa rushwa barani Afrika.
Pamoja
na kuwepo katika viwango tofauti kwa miaka mingi, rushwa nchini humo ilishamiri
kiasi cha kuota mizizi hasa wakati wa utawala wa Jenerali Sani Abacha.
Katika miaka yake mitano ya kuwepo
madarakani kuanzia mwaka 1993 hadi 1998 alipokufa ghafla mno, Abacha mwenyewe alikuwa
kinara wa rushwa akijilimbikizia mabilioni ya fedha nje na ndani na nchi hiyo.
Alikuwa rais ambaye kwake uhalifu huo wa jinai ulikuwa ni ujanja wa maisha!
Aliporudi tena madarakani Mei 29,1999 baada
ya awali kuwa Kiongozi wa Kijeshi kuanzia mwaka 1975 hadi Januari Mosi, 1980,
Jenerali Olusegun George Obasanjo alijitajidi kupambana na hali hiyo katika
miaka yake minane mipya ya utawala wake wa kiraia, lakini kwa vile hali ilishakuwa
mbaya mno katika kipindi cha Jenerali Abacha kamwe hakuweza kuitokomeza mara
moja.
Kustaafu kwake na hasa katika miaka mitano
ya utawala wa Jonathan, kwanza akiwa ni rais wa kurithi na hata alipochaguliwa
kushika nafasi hiyo mwaka 2011, tatizo hilo la rushwa lilirejea tena na hali
ikawa mbaya kupindukia pale kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kilichoundwa
mwaka 2009 kilipozidi kuimarisha ukatili wake.
Ilifika mahali ambapo rushwa ilikuwa
kama sehemu ya maisha ya kila siku nchini humo. Ilifika mahali kuwa vitendo
hivyo viligeuzwa na kuwa sehemu ya lazima ya maisha ya watu na kuenea kila
sehemu kuanzia mijini mpaka vijijini.
Ndiyo maana ulipofika uchaguzi mkuu wa
Machi 28, mwaka huu, wapiga kura wa Nigeria waliona wamchague Jenerali Buhari
na kumwangusha Jonathan.
Walifanya hivyo kwa sababu aliahidi kupambana
kwa nguvu zake zote na kikundi hicho cha kigaidi, kile ambacho kimeongeza
vitendo hivyo vya rushwa huku Rais Jonathan akishindwa kukikabili na kutaka eti
achaguliwe tena ili aifanye kazi hiyo, ahadi ambayo hata wendawazimu wa
kufikiri wasingeikubali!
Mbali kutoka Nigeria, ushindi wa Chiluba
nchini Zambia, Methieu Kerekou (Benin), Kibaki (Kenya), Michael Satta (Zambia)
ama Profesa Peter Mutharika kule Malawi mwaka jana pia hauwezi kufananisha kwa
namna yoyote ile na nguvu za Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi, NLD wala Ukawa hapa
nchini.
Chiluba kwa mfano alishinda kwa vile
UNIP ilikuwa imeshakufa miaka mingi kama chama cha siasa. Kaunda aliyekuwa
madarakani tangu mwaka 1964 alikuwa gizani kuhusu ukweli huo.
UNIP ilikuwa imebaki tu ofisini kwake au
makao makuu bila kuwepo tena popote au kwa namna yoyote, lakini yeye alikuwa
hafahamu kitu chochote!
Alikuwa hajui kwa sababu alikitumia
chama hicho kama alama ya kugombea tu urais ili kukidhi matakwa ya kisheria,
lakini siku zote alishiriki kinyang’anyiro hicho kama “KK” akidhani kwamba ni
maarufu kuliko taasisi hiyo yenyewe.
Hakujua kabisa kuwa chama hicho hakina
mashina popote, hakina matawi wala ofisi za kata ila kipo kwa wastani kwenye
majimbo, wilaya pamoja na mikoani tu.
Kilikuwa kimeshakuwa sawa na jinsi vyama
kama Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP) au NCCR –
Mageuzi vilivyo hapa nchini au Civic United Front ilivyo katika upande wa
Tanzania Bara huku yeye akiwa hajui!
Aidha, ushindi wa Satta uliokuja
kutokana na kifo cha Rais Levy Mwanawasa au wa Profesa Peter Mutharika dhidi ya
Joyce Banda kule Malawi pia una sura zake.
Satta alichaguliwa kutokana na chuki za
Wazambia baada ya Mwanawasa kumtia misukosuko Chiluba na kuonekana kutokuwa na
shukurani kwake.
Ni Chiluba ambaye alimwibua Levy Mwanawasa
na kushinikiza ateuliwe kuwa mgombea urais wa chama cha MMD wakati yeye alipokuwa
akistaafu mwaka 2001.
Lakini aliposhika wadhifa huo na hasa
kipindi kile cha pili akamshtaki kwa makosa ya rushwa, ufisadi na matumizi
mabaya ya madaraka huku watu wakiamini kwamba alifanya hivyo ili kutaka
umaarufu kwamba ni kiongozi anayetetea maslahi yao.
Ndiyo maana alipokufa chama chake
kiliondoshwa madarakani katika uchaguzi mkuu uliokuja kufanyika ili kukidhi
matakwa ya Katiba. Kiliadhibiwa kwa vile kilionekana kuwa cha kisasi, kile ambacho pia
uwepo wake ulitegemea zaidi nguvu ya rais aliyepo madarakani na siyo wanachama waliopo
mijini na vijijini.
Mwanawasa mwenyewe alidhani akimtia
gerezani Chiluba angekijenga kwa sababu tu wote wanatoka chama kimoja, jambo
ambalo wapiga kura walio wengi waliliona na kuamua vinginevyo bila ya kujali kwamba
alishakufa.
Katika kuhitimisha makala hii, sasa
ninaomba nigusie angalau kidogo sana kuhusu nafasi ya 159 ya Tanzania kati ya
nchi 187 ambazo ni masikini duniani.
Jambo ambalo halieleweki hapa ni je;
hivi mtu akiwa ni wa 159 kati ya 187 maana yake ni kutoka chini au kutoka juu?
Hata kwa akili ndogo tu ya kawaida ni
kwamba, jumla ya nchi ambazo ni masikini duniani ziko 187, halafu kuna ya kwanza kwa
kuwa ni masikini zaidi, ya pili, ya tatu, ya nne, ya tano, ya sita, ya saba…ya
100, ya 150 na kisha Tanzania kuwa ni ya 157.
Hivi ubaya wake hapo uko wapi kama
inatanguliwa na nchi masikini 156 huku yenyewe ikiwa mbele ya mataifa 28 tu?
Kama ingekuwa inashika nafasi ya 157 kwa
utajiri kati ya nchi hizo 187 hapo wote tungesema iko mbali sana, lakini kuwa
kwake ya 29 kutoka mwisho katika orodha ya masikini na kutanguliwa na nchi 156,
mtu anayesema vinginevyo huyo ana chuki zake mwenyewe au pengine hafahamu
kabisa kanuni za kuhesabu.
Ndiyo maana ninasema bila mashaka yoyote
kuwa wote wanaosubiri kuiona CCM nayo inashindwa kama PDP kule Nigeria, UNIP na
MMD vya Zambia, KANU ya Kenya ama UPP ya Malawi kwa hakika wanaota!
Mwandishi
wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM katika
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Upanga jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu
Na. 0659 220 220 na 0762 633 244
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇