LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 11, 2015

TANZANIA: UVUVI ENDELEVU UTAWASAIDIA WAVUVI KUONDOKANA NA UMASKINI DUNIANI

Na  Mwandishi Maalum, New York
 Tanzania, kupitia  Mwakilishi wake wa Kudumu  katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi,   imeelezea  kuridhishwa kwake na namna ambavyo  Mashirika ya Kimataifa naTaasisi binafsi  zinavyoshirikiana na  kwa karibu  na  serikali  na taasisi zake kuimarisha sekta ya uvuvi.

Ushirikiano huo  umeifanya sekta ya uvuvi nchini kuwa wenye tija na hivyo kuchangia katika ongezeko la kupato na kuwaondoa katika umaskini jamii ya watanzania ambao maisha yao  ya kila siku yanategemea sana uvuvi, na pia kuimarisha  utuzaji wa mazingira ya pwani na viumbe hai.

Balozi Tuvako Manongi  ameyasema hayo  wakati  wa mkutano wa pembezoni ( side event) uliokuwa umeandaliwa na Mpango wa Chakula Dunia ( FAO). Mkutano huo umefanyika sambamba na mkutano  usio rasmi ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakutana ana kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya bahari na uwiano wake katika utekelezaji wa  Malengo  Mapya ya Maendeleo  Endelevu baada ya 2015.

Balozi Manongi alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano huo ambapo  majadiliano yalilenga  zaidi katika suala zima la  uwezeshwaji wa wataalamu wa sekta ya uvuvi na  wavuvi   wadogo na wakati kwa kuwapatia  mbinu na maarifa ya kisasa ya uvuvi endelevu na unaozigatia utuzaji wa  mazingira ya  bahari na viumbe hai.

Katika mchango wake,  Balozi ameeleza kuwa  uchumi na ustawi wa   wavuvi wengi wanaoishi pembezoni mwa bahari (pwani) nchini tanzania  unategemea sana shughuli za uvuvi na kutoka na  ukweli  huo, Serikali ya Tanzania,  licha ya kukaribisha wabia katika kuiendeleza sekta ya  uvivu  pia inawashukuru wale wote ambao  hadi sasa wametoa mchango wao wa hali na mali katika eneo hilo.
 Akaongeza kuwa mafunzo na utaalamu ambao wadau hao wamekuwa wakiwapatia wataalam wa kitanzania  kwa kuwashirikisha pia wavuvi ambao ndio wahusika wakuu,  umesaidia sana katika kuwainua kiuchumi lakini pia  kuwapatia mbinu endelevu za uvuvi na utunzaji wa mazingira.
Wadau  ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia maendeleo  endelevu ya sekta ya  Uvuvi ikiwamo misaada ya kiufundi ni  FAO na  EAF- Nansen  Project ya  Norway.

Tanzania  ni kati ya  nchi 32 ambazo zinashirikiana  kwa karibu na  EAF –Nansen Project katika miradi  mbalimbali   inayohusu uwezeshwaji wa wavuvi wadogo na wakati. Aidha Tanzania ni kati ya nchi 10 za mwanzo zilizochaguliwa   kutekeleza  mpango huo.

Amesema Balozi Manongi,    uvuvi endelevu na matumizi salama ya  Bahari ni  moja  ya  ajenda  za Malengo Mpya ya Maendeleo Endelevu baada ya 2015 (SDGs).  Ajenda ambayo    kwayo   inasisitiza  usimamizi endelevu  na  ulinzi wa bahari na mazingira ya pwani na viumbe hai ili kuepusha athari mbalibmali.

Vile vile ajenda hiyo ambayo ni  namba 14 inasisitiza pia uwepo kwa kanuni bora zinazosimamia uvuvi ikiwa ni pamoja na  kudhibiti uvuvi wa kupita kiasi na uvuvi haramu,   na utoaji wa huduma za kisasa kwa wavuvi wadogo na fursa za masoko. 

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzani katika Umoja wa Mataifa  ameeleza zaidi kwamba, zao la samaki  pamoja na  kuwa kuchanzo cha kipato kwa watanzania wengine na taifa kwa ujumla,  lakini pia   samaki   wanachangia katika kuwapatia lishe bora watanzania na  kwa sababu hiyo  matumizi endelevu ya mazao ya  bahari  na bahari ni jambo  muhimu sana.

Katika majadiliano hayo,  Dr. Gabriella Bianchi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utafiti wa samaki  kutoka  ofisi za FAO yeye katika mchango wake, ameelezea baadhi ya  mambo ambayo wanatarajia kuyafanya katika kuzisaidia nchi za Afrika  Mashariki  Tanzania ikiwamo na kwingineko Afrika    katika masuala ya  usimamizi, mafunzo na utaalamu  zaidi  kwenye masuala ya  samaki na bahari kwa ujumla.

Akasema  mabadiliko ya tabia nchi, shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, na uchafuzi wa  bahari  ni baadhi ya changamoto ambazo wataalamu na watafiri wa masuala ya  bahari na viumbe hai wa baharini  kuamua  kupanua wigo wa kazi zao za utafiti ikiwa ni pamoja na  mafunzo na uwezeshaji.

Naye   Dr. Alf Hakon Hoel ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya utafiti,  amesema  Norway inakamilisha  ujenzi wa  meli mpya  na ya kisasa  ya masuala ya utafiti inayotarajia kuanza shughuli zake mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Dr.  Hoel meli hiyo itakuwa na vyumba vya kufundishia,  maabara za picha na maabara ya tabia nchi.
--------------
PICHA ZAIDI
 Balozi Manongi akibadilishna  mawazo na Dr. Alf Hakon Hoel ambaye ni mtaalamu wa masuala ya  utaifiti na ambaye alieleza kwamba Norway iko katika maandalizi ya mwisho ya kukamilisha meli mpya  na ya kisasa zaidi ya utafiti itakayoanza kazi mwakani.
 Balozi  akibadilishana mawazo na Dr. Gabriella Bianchi ambaye pia ni  mtaalamu wa masuala ya  utafiti wa samaki,  Dr   Gabriella na Dr, Hoel wamefanya kazi kwa karibu sana na wataalamu wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya  uvuvi.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa Pembezoni

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages