LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 6, 2015

UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA BIOMETRIC VOTER REGISTRATION (BVR) KATIKA KATA TISA (9) ZA HALMASHAURI YA MJI WA MAKAMBAKO KUANZIA TAREHE 23/2/2015 HADI 3/3/2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza rasmi zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu ya Uboreshaji wa Daftari, ikiwemo manunuzi ya vifaa na upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, tofauti na Uboreshaji wa Daftari hilo kwa Awamu zote za Chaguzi zilizopita, linafanyika kwa kutumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR). Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lilianza kufanyika katika Kata tisa (9) za Halmashauri ya Mji wa Makambako katika Vituo 54 vilivyowekwa katika Mitaa na Vitongoji, kuanzia tarehe 23/2/2015 katika Kata za Kitisi, Kivavi, Lyamkena, Maguvani, Majengo, Makambako, Mji Mwema, Mlowa na Mwembetogwa.
Tume ililenga kuandikisha Wapiga Kura 32,370 kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Takwimu za Sensa ya Idadi ya watu ya mwaka 2012.  Tume ililenga kuandikisha kwa siku jumla ya watu 1,850. Hata hivyo mara baada ya uandikishaji kuanza idadi ya Wapiga Kura waliokuwa wanajitokeza iliendelea kuwa kubwa na kuongezeka kila siku ambapo kulikuwa na misururu mirefu ya watu waliojitokeza kujiandisha katika Vituo vyote vya Uandikishaji. Tume ilivuka malengo yaliyowekwa ya Uandikishaji kutokana na kujitokeza kwa wingi kwa Wapiga Kura waliofika katika Vituo vya Uandikishaji kila siku kwa Kata zote tisa (9) za Mji wa Makambako ambazo zilikuwa zinaandikisha Wapiga Kura.
Idadi ya Wapiga Kura waliojitokeza na kuandikishwa kwa kila siku katika Kata tisa (9) za Mji wa Makambako ilikuwa kama ifuatavyo:-
 i.Tarehe 23/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 3,014;
ii.Tarehe 24/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 4,727;
iii.Tarehe 25/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 5,301;
iv. Tarehe 26/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 6,354;
v. Tarehe 27/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 6,731;
vi.Tarehe 28/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 6,545;
vii.Tarehe 1/3/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 6,906;
viii.Tarehe 2/3/2015 kutokana na Watu waliokuwa wanajitokeza kujiandikisha kuendelea kupungua, Tume iliandikisha Wapiga Kura 4,662; na
ix.  Tarehe 3/3/2015 ambayo ndio ilikuwa siku ya mwisho ya uandikishaji, Tume iliandikisha Wapiga Kura 2,469.
Hivyo, jumla ya Wapiga Kura wote walioandikishwa katika Kata tisa (9) za Mji wa Makambako ni 46,709. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari katika Kata tisa (9) za Halmashauri ya Mji wa Makambako limefanyika kwa ufanisi na mafanikio makubwa ambapo Tume imevuka lengo lililowekwa la Uandikishaji kwa kuandikisha jumla ya Wapiga Kura 46,709 na kuvuka  lengo lililowekwa la  kuandikisha Wapiga Kura 32,370 waliolengwa kuandikishwa kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Takwimu za Sensa ya idadi ya Watu ya mwaka 2012.
Mashine nyingi za BVR zimeonyesha ufanisi mkubwa kwa kuwa zimekuwa zikiandikisha idadi ya Wapiga Kura kuanzia 80 kwa siku hadi watu 160. Pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na changamoto chache zilizojitokeza ikiwemo ya watu wengi zaidi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kusababisha kuwepo kwa misururu mirefu ya watu waliojitokeza katika Vituo kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Changamoto hiyo ilishughulikiwa na Tume kwa kuongeza muda wa ziada wa siku mbili za kuandikisha Wapiga Kura baada ya muda wa siku saba za uandikishaji kumalizika. Lengo la kuongeza siku mbili zaidi za uandikishaji lilikuwa ni  kutoa fursa kwa Wapiga Kura wote ambao walikuwa bado hawajajiandikisha kujiandikisha. Vilevile, katika kushughulikia changamoto hizo, Tume iliongeza idadi ya BVR Kits katika baadhi ya Vituo vilivyokuwa na idadi kubwa na misururu mirefu ya Wapiga Kura waliojitokeza kujiandikisha. Wapiga Kura wote waliojitokeza kujiandikisha waliandikishwa pasipo kuachwa. Kwa ujumla changamoto zote zilizojitokeza zilishughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi.
Tume inaendelea na Ratiba ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata nyingine za Halmashauri ya Mji wa Makambako ambapo Ratiba ya zoezi la Uboreshaji litafanyika kama ifuatavyo:-
                              i. Katika Kata ya Kitandililo Uboreshaji umeanza kufanyika kuanzia tarehe 3/3/2015 na utamalizika tarehe 9/3/2015.
                           ii. Kata ya Mahongole, Uboreshaji utaanza kufanyika tarehe 11/3/2015 na kumalizika tarehe 17/3/2015.
                        iii.  Kata ya Utengule, Uboreshaji utaanza kufanyika tarehe 11/3/2015 na kumalizika tarehe 17/3/2015. 
Tume itaendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Njombe katika Wilaya za Njombe, Makete, Ludewa na Wanging’ombe kuanzia tarehe 16/3/2015 hadi 12/04/2015.
Tangu zoezi hili lianze katika Halmashauri ya Mji wa Makambako na kumalizika, Wananchi wameonyesha mwamko mkubwa sana wa kujiandikisha. Ni matumaini ya Tume kuwa Viongozi wote, Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari vitahamasisha Wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha katika Wilaya za Njombe, Makete, Ludewa na Wangingo’mbe kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Baada ya kukamilisha Ratiba ya Uboreshaji katika Mkoa wa Njombe, Tume itatoa Ratiba ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa mingine.
Tangazo hili limetolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages