LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 11, 2022

KANISA HALISI LASIMIKA HATMA YA BABA HALISI NA MAMA HALISI, LATUMA SALAMU ZA HERI NA BARAKA KWA RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kazini.


Na Bashir Nkoromo, Tegeta
Kanisa Halisi la Mungu Baba limemtumia salam za heri, baraka na upendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ili Mungu Baba amlinde asijikwae kwenye korongo au kikwazo chochote kibaya katika maisha yake na katika kazi zake.

Salam hizo zimetumwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi, wakati wa Sherehe ya kusisimua na ya kihistoria ya Kusimika Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi, iliyofanyika jana Jumapili, 12 Adari,1(Aprili 10, 2022), Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Namanga jijini Dar es Salaam.

Baba Halisi alituma salam hizo kupitia kwa Katibu wa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kinondoni Godwin Gondwe, Anold Kinyaiya ambaye alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha DC huyo kwenye sherehe hiyo iliyohudhuriwa na Viongozi mbalimbali na maelfu ya Uzao (waumini) na Makuhani wa Kanisa hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania.

"Tunajua, japo uliyemuwakilisha hakuweza kufika kutokana na kuwa na majukumu mengine, lakini tunaamini wewe ndiye yeye. Basi tunakuomba utufikishie salam zetu za heri, baraka na upendo kwa Rais wa Taifa letu Samia Suluhu Hassan, kwamba tunamuinua (kumuombea) kila siku asijikwae kwenye kikwazo chochote kibaya katika maisha yake na katika kazi zake.

Kwamba tunawainua pia viongozi wa ngazi zote walio chini yake, nao wasijikwae kwenye korongo au kikwazo chochote kibaya katika maisha yao na kazi zao", akasema Baba Halisi, wakati akimuaga Mwakilishi wa DC Gondwe, mwishoni mwa sherehe hiyo na kuongeza:

"Mwambie Rais sisi kila siku asubuhi mapema huwa tunamuombea yeye na hao walio chini yake katika kutimiza majukumu ya kuliongoza Taifa letu".

Mapema, kabla ya kuanza hotuba yake ya kufanya Shukrani katika Sherehe hiyo ya kusimika Hatma yake na ya Mama Halisi, Baba Halisi aliwaongoza Uzao na Makuhani wa Kanisa hilo kufanya shukurani (maombi) ya kumuinua Rais Samia na wasaidizi wake wote kwa zaidi ya dakika kumi.

"Kabla sijaanza Shukurani ya kusimika Hatma yangu na ya Mama Halisi, kwanza kama mnavyojua kawaida yetu huwa tunamwinua (kumuombea) Kiongozi wa Taifa letu na Wasaidizi wake wote, kama tunavyoagizwa na Mungu Baba, kwamba kabla ya kufanya lolote tunapaswa kufanya kwanza shukrani kwa ajili ya kuwainua wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.

Hili mnalijua au hamlijui?", Baba Halisi akasema, na kuwauliza Uzao na Makuhani waliokuwa wamefurika ukumbini kwenye Sherehe hiyo.

Baada ya Baba Halisi kuwauliza na kutorishwa na sauti ndogo waliyotumia kujibu, akawauliza tena, kama wanajua au hawalijui agizo hilo, Uzao wakalipuka kwa sauti za juu, wakamjibu tunajuaa! basi akamuomba mgeni Rasmi kusogea mbele yake, akaanza Shukrani ya Kumwinua Rais Samia na Wasaidizi wake wote.

Baada ya hatua hiyo Baba Halisi alimwita Mama Halisi kisha akamshika mkono akiwa upande wake wa kuume, na Minara (watoto) wake wanne nao wakasimama naye safu moja, akaanza kutoa Hotuba yake hiyo ya kusisimua, akisema;

"Kwanza kabisa tunamshukuru Chanzo cha Mema na Mazuri yote, ambaye ndiye Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana (Kolosai 1:16-17), kwa kutusimika yeye mwenyewe kuwa Baba Halisi na Mama Halisi.

Mimi Baba Halisi, nilipoonekana kwa mara ya kwanza kwenye familia niliyopitia, sikujua kuwa mimi ndiye Baba Halisi! Hata familia hiyo niliyopitia walikuwa hawajui kuwa mimi ni Baba Halisi. Hata hivyo, kuna Sauti (mwito wa Mungu), nilipokea nilipoanza kukua iliyonikataza kumpiga kofi yeyote, kumtukana yeyote na kumlaani yeyote.

Hivyo, ndivyo nilivyokuwa shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu. Wale waliosoma na kufanya kazi pamoja nami, wanaweza kushuhudia kuwa ndivyo au sivyo", akasema Baba Halisi na kisha akaendelea;

"Nilipokuwa Chuo Kikuu, nilipata sauti ya kuapa kuwa, Sitakosana na mtu yeyote kwa sababu ya gari, fedha au mwanamke katika Maisha yangu. Hivyo ndivyo nilivyokuwa kila mahali nilipopitia. Sikumbuki mtu yeyote ambaye nimewahi kukosana naye.

Katika mataifa yote niliyowahi kwenda, walipenda kuniita Apologetic Man (Mtu wa Toba). Hadi sasa bado naishi Maisha hayo ya toba na shukrani! Kwa sababu hiyo mnisamehe bure, Uzao, Makuhani, Jamii, Taifa, Uumbaji na Uhalisia wotekila mahali nilipowakwaza kwa sababu ya kuleta Sauti ya Chanzo Halisi ambayo kwa mara ya kwanza hamkuielewa. Hata mimi nimewasamehe bura bila kubagua yeyote." akasema Baba Halisi.

Baba Halisi akaendelea kueleza alikotoka ikiwemo namna alivyokutana na Mama Halisi hadi kuoana kuwa Kanisa (mke wake), maelezo ambayo yaliwafanya maelfu waliokuwa katika sherehe hiyo kuonekana watulivu na kumsikiliza kwa makini.

"Nilimuona Mama Halisi miaka karibu 30 iliyopita kwenye basi kubwa Kibaoni-Tegeta, nikiwa naenda mjini Dar es Salaam. Kesho yake alipokuja kusali mahali nilipokuwa nasali, wote kwa pamoja katika nyumba niliyopitia walisema ‘‘leo tumemuona atakayekuwa Mama Halisi’’.  

Baada ya miezi mitatu ikawa Harusi kubwa. Hatujawahi kutofautiana wala kupigana hata siku moja kwa jambo lolote! Namshukuru Chanzo Halisi kunipa Kanisa (mke) ambaye siyo mtata kwa jambo lolote.
 
Tukiwa kwenye kazi ya Sekta ya Umma, tulipata watoto watatu na baada ya kuingia kwenye Kazi ya Kanisa tukapata mtoto wa Wanne, ambaye ni mlango na muhuri wa nyie wote kuwa wanangu walioumbwa kwa sauti.

Napenda pia mjue kuwa watoto hao hawakwenda Chuo Kikuu, ingawa walikuwa na sifa ya kwenda, kwasababu ya gharama ambayo ilibidi tuilipe ya kuwa Baba Halisi na Mama Halisi na wao kuwa Mnara Mmoja Halisi ili leo tusimikwe rasmi kuwa familia ya kuvusha Kanisa, jamii na Taifa mpaka kufika Bustani Mpya, mahali anapoishi Chanzo Halisi, aliye Chanzo cha Mema na mazuri peke yake", alisema Baba Halisi na kuongeza;

"Leo, kwa sababu ya Mnara Mmoja Halisi kukubali kufuatana na mimi bila maswali, nawakabidhi zawadi ya duka la vitambaa vya kushona vazi jeupe. Huu ni uhalisia wa kupata Hatma ya Baraka na Utajiri Udumuo kwenu nyote mlioumbwa kwa sauti, umilele wote bila mauti.
 
Hatuwezi kusema mengi leo, tunashukuru tu Chanzo cha Mema na Mazuri kutupa kibali cha kuwa Baba Halisi, Mama Halisi na Mnara Mmoja Halisi.

Katika kutimiza shukrani hii, leo tunatoa shukrani kwa wote waliokuja kushuhudia jambo hili. Aidha,tunatoa shukrani kwa Serikali iliyokubali kusajili hatma hii. Pia, tunatoa shukrani kwa uzao na Makuhani Halisi waliokubali kufuatana nasi katika safari hii ambayo haijawahi kuwepo katika majira saba zilizopita.

Zaidi sana, napenda kumtukuza Chanzo Halisi kwa kuwa sijawahi kufanya chochote kwa kutumia akili ya mtu, wala akili ya shule bali akili yake Yeye. Ningetumia akili ya mtu au ya shule tusingefika mahali palipokusudiwa kama ilivyotokea leo. Nyote Mbarikiwe kupita Kawaida", Baba Halisi akahitimisha Shurani yake.

Hadi sasa majina ya Baba Halisi na Mama Halisi yanatambuliwa kuwa ni majina yao rasmi kwa kuwa tayari yameshasajiliwa na Mamlaka inayohusika na utoaji Vitambulisho vya Taifa. 

Habari kwa picha👇

Baba Halisi na Mama Halisi wakiwa katika furaha wakati Kwanya ya Nyimbo za kumtukuza Mungu Baba ya Kanisa Halisi la Mungu Baba, ilizpokuwa ikiimba wakati wa Sherehe kubwa ya Kusimika Hatima yao, iliyofanyika jana Jumapili, Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam.
Mama Halisi akionyesha furaha hiyo.
Mama Halisi akiendelea kuonyesha furaha hiyo kwa kuimba na kushangilia.
Baadhi ya Makuhani na Uzao wa Kanisa Halisi la Mungu Baba wakishangilia wakati wimbo wa kumtukuza Mungu Baba ulipokuwa ukiimbwa wakati wa Sherehe hiyo.
Baadhi ya Makuhani na Uzao wa Kanisa Halisi la Mungu Baba wakishangilia wakati wimbo wa kumtukuza Mungu Baba ulipokuwa ukiimbwa wakati wa Sherehe hiyo.
Baadhi ya Makuhani na Uzao wa Kanisa Halisi la Mungu Baba wakishangilia wakati wimbo wa kumtukuza Mungu Baba ulipokuwa ukiimbwa wakati wa Sherehe hiyo.
Kuhani Faida Halisi akieleza jambo fulani, wakati wa sherehe hiyo.
'Mpapasa' Kinanda wa Kwaya ya Kanisa Halisi la Mungu Baba akikiungurumisha kinanda wakati wa Sherehe hiyo.
Wanakwaya wa wakiimba wimbo wa kumtukuza Mungu Baba wakati wa sherehe hiyo.
Mpiga gita zito la Bass, akiungurumisha chombo hicho, wakati wa sherehe hiyo.
Mpulizaji mahiri wa 'Domo la Bata' King Maluu, akiwajibika kunogesha Wimbo wa kumtukuza Mungu Baba, wakati wa Sherehe hiyo.
Mwimbaji wa Kwaya ya Kanisa Halisi la Mungu Baba akiimba wimbo wa kumtukuza Mungu.
Mwimbaji wa Kwaya  hiyo, akiimba wimbo wa kumtukuza Mungu.
Baadhi ya Makuhani wakiwa kwenye Sherehe hiyo.
Baadhi ya Makuhani wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Makuhani na Uzao wakifurahia wimbo wa kumtukuza Mungu Baba wakati wa Sherehe hiyo.
Uzao na Makuhani wakiwa wamefurika ukumbini wakati wa sherehe hiyo.

Baadhi ya uzao wakifuatilia sherehe hiyo wakiwa kwenye hema maalum nje ya ukumbi. 

Mgeni Rasmi Kuwasili👇

Kuhani Moja Halisi akitambulisha Makuhani wa Kanisa Halisi kwa Mgeni Rasmi Katibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Anold Kinyaiya (Mwenyekiti), baada ya mgeni huyo Rasmi kuwasili kwenye Sherehe hiyo kumwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe.
Kuhani Moja Halisi akiendelea kutambulisha Makuhani kwa Mgeni Rasmi.
"Hawa pia ni Makuhani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba", akasema Kuhani Moja Halisi kumweleza Mgeni Rasmi.
Mgeni Rasmi Anold Kinyaiya akiwa tayari ukumbini. Kulia ni Baba Halisi na Mama Halisi.
Mama Halisi na Huduma Moja Halisi wakimsaidia jambo Baba Halisi.
Makuhani wakiwa kwenye Ibada ya Sherehe hiyo wakati ikianza kupamba moto.
Baba Halisi akisoma Hotuba ya Kusimika rasmi Baba Halisi na Mama Halisi wakati wa sherehe hiyo. Pamoja naye ni Mama Halisi na Kushoto ni Mnara Udhihirisho Halisi, Mnara Huduma Moja Halisi na Kulia ni Mnara Mwaminifu Halisi na Mnara Utimilifu Halisi.
Mgeni Rasmi (Mwenye suti), akipokea shukurani iliyokuwa ikifaywa na Kuhani Moja Halisi wakati wa Ibada hiyo. Kulia ni Baba Halisi na Mama Halisi.
Mgeni Rasmi akisikiliza wakati Kuhani Moja Halisi akimwalika kwenda altareni kuzungumza.
Kuhani Moja Halisi akimwalika mgeni Rasmi kupanda Altareni kuzungumza.
Mgeni Rasmi Katibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Anold Kinyaiya akizungumza mbele ya Baba na Mama Halisi, Makuhani na uzao wa Kanisa Halisi kufungua rasmi Sherehe hiyo.
Baba Halisi akimpongeza mgeni Rasmi kwa maneno murua aliyotoa kwenye Hotuba yake.
Mama Halisi pia akampongeza Mgeni Rasmi kwa maneno yake Murua aliyotoa wakati wa Sherehe hiyo.
Baada ya kuzungumza Mgeni rasmi akaketi kuendelea kufuatilia yaliyokuwa yanajiri.
Baba Halisi na Mama Halisi wakiwa wametulia kusikiliza wakati Wawakilishi wa Kampuni Moja ya kutengeneza vifaa vya Kisasa vya kusafisha maji, wakitambulishwa.
Waendeshaji wa Kampuni hiyo wakijitambulisha.
Baadhi ya Vifaa vya kusafisha Maji vya kisasa kabisa vinavyotengenezwa na Kampuni hiyi ni hiki ambacho kimenunuliwa na Kanisa Halisi la Mungu Baba kutoka kampuni hiyo.
Kuhani Moja Halisi akifanya Shukurani ili kumpa nafasi tena Baba Halisi kuja altareni kufanya Shukurani ya Kusimika Hatma Baba Halisi na Mama Halisi.
Mgeni Rasmi akiwa amesimama katika eneo Maalum aliloelekezwa na Baba Halisi kwa ajili ya kupokea Shukurani ya kumwinua Rais Samia Suluhu Hassan na Wasaidizi wake kabla ya Shukurani ya Kusimika Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi.
Baba Halisi akifanya Shukurani ya Kumuinua Rais Samia na wasaidizi wake wote, alipokuwa hajafanya Shukurani ya Kusimika Hatma ya yeye na ya Mama Halisi.
Mgeni Rasmi akiwa amesimama kwa unyeyekevu kupokea Shukrani hiyo ya kuinuliwa Rais Samia.
Baada ya Baba Halisi kumuinua Rais Samia akaelekeza Mgeni Rasmi kukabidhiwa zawadi za vitabu vya machapisho ya Sauti alizopokea kwa nyakati tofauti na kuziandika, ili zawadi hiyo akampelekee Rais Samia.
Kisha Baba Halisi akafanya shukurani ya Kusimika Baba Halisi na Mama Halisi (kushoto).
Akaendelea kutoka maelezo kufafanua Kusimika Hatma Baba Halisi na Mama Halisi imekujaje. "Kuna watu nimesikia wanauliza nani amesimika Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi. iko hivi, wapo waliotangulia wengi akiwemo Adam ambao walisimikwa lakini aliyewasimika hakuonekana! hii ni kwa sababu walisimikwa kwa sauti kutoka kwa Mungu mwenyewe", akasema Baba Halisi, kisha uzao na Makuhani wakashangilia na kupiga viganja kwa furaha.
Baadhi ya Makuhani kutoka Burundi, Congo DRC na Kenye wakitambulishwa.
Kuhani kutoka Houston Marekani akijitambulisha.
Padre ambaye alihudhuria Sherehe hiyo akijitambulisha.
Baadhi ya Makuhani na Uzao wakamshangilia Padre huyo.
Mgeni mmoja mwingine akajimbulisha.
Na huyu mgeni akajitambulisha.
Makuhani na Uzao wakiwa wamefurika ukumbini.
Makuhani na Uzao wakiwa ukumbini.
Baba Halisi akitoa zawadi kwa mtoto mchanga wa Uzao aliyefika kwenyefika kwenye Sherehe hiyo Kushoto ni Mama Halisi.
Makuhani wakipeleka kutoa zawadi yao ya pamoja kwa Baba na Mama Halisi mwishoni mwishoni wa sherehe hiy.
Zawadi zikiendelea kutolewa.
Baba Halisi akionyesha Vitambu vya Safari ya Uzao wa Mungu Baba, ambavyo ni machapisho ya Sauti alizopokea kwa nyakati tofauti na kuziandika. Alihimiza Uzao, Makuhani wa Kanisa Halisi na watu wengine kuvinunua kwa kuwa vinayo mambo makubwa yanayotakiwa kila mtu ayajue. Bei ya vitabu hivyo kwa pamoja kuanzia Vol. 1 hadi Vol. 5  ni sh. 70,000 na Vinapatikana Makao Makao Makuu ya Kanisa hilo (Moyo Mmoja), Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam.
Watoto wa Kuhani wa Kanisa Halisi la Mugu Baba kutoka Houston, Marekani wakiwa wamesimama mbele, walipokuwa wamepewa nafasi ya Kumsalimia Baba Halisi.
Mgeni Rasmi wa Anold Kinyaiya akiondoka ukumbini mwishoni mwa Sherehe hiyo.
Kuhani Ushindi Halisi na Kuhani Moja Halisi wakiwa wamesimama imara wakati mgeni rasmi akiondoka.
Baadhi ya Uzao na Makuhani wakizungmza nje ya ukumbi baada ya sherehe hiyo.
"Kuhani umeionaje Sherehe, naona imefana sana". inaelekea ndivyo makuhani hawa walivyokuwa wakisemezana nje ya ukumbi baada ya sherehe hiyo.
Baadhi ya uzao wakiondoka mmoja baada ya mwingine baada ya sherehe hiyo.
Uzao hawa wakiwa mbele ya basi lao ili kurudi Kigamboni baada ya sherehe hiyo.

Basi la lililotela Makuhani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba Kituo cha Mafinga, likiwa tayari kuondoka na abiria kurejea huko baada ya sherehe hiyo

 ©2022 CCM Blog/Bashir Nkoromo

 

6 comments:

  1. IMEKUWA, ainuliwe CHANZO HALISI
    Muweza wa yote.

    ReplyDelete
  2. IMEKUWA ainuliwe CHANZO HALISI muweza wa yote, na awafungue macho mataifa yajue na yasikie sauti ya CHANZO HALISI ( Mungu Baba)

    ReplyDelete
  3. Namshukuru CHANZO Halisi cha Mema na mazuri kwa ajili ya Baba Halisi, Mama Halisi, Minara na Taifa baba kwa ujumla. Aliyetupa maono haya na kulichagua Taifa hili kuwa Taifa baba
    azidi kutulinda,Amani itawale ndani ya taifa.

    ReplyDelete
  4. Tunamshukuru Mungu baba Chanzo halisi, anaye wawezesha kuandika habari hizi njema, wote mbarikiwe sana na CHANZO HALISI Muumba wa vyote wote na yote, tunawapenda mno,....

    ReplyDelete
  5. Nina mshukuru CHANZO HALISI,kwaajili ya kutupatia Tanzania,Afrika na mataifa yote yaliyompokea CHANZO HALISI,kukubali kufuatana naye na kumpenda Baba Halisi na Mama Halisi wanaotubariki kwa baraka za Uhalisia

    ReplyDelete
  6. Tunamshukuru mno MUUMBAJI WA YOTE,WOTE na VYOTE vilivyo vyema na vizuri,SIFA,HESHIMA NA UTUKUFU kwa hakika anastahili yeye kwa kuifanikisha sherehe hii.
    Hakika tumepokea Baraka na Utajiri Udumuo.IMEKUWA.

    ReplyDelete

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages