LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 22, 2018

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHATEKELEZA AHADI YA KUBORESHA NA KUSOGEZA HUDUMA ZA AFYA KARIBU NA WANANCHI KWA KUFANIKISHA UPATIKANAJI WA GARI LA KUBEBEA WAGONJWA KATA YA LANG'ATA - WILAYA YA MWANGA.

1 Julai 2018
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetekeleza ahadi ya kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na  wananchi kwa kufanikisha upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa Kata ya  Lang'ata - Wilaya ya Mwanga.

Gari la kubebea wagonjwa limekabidhiwa katika kituo cha afya cha Kagongo na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi kwa niaba ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli ambaye ndiye aliyetoa gari hilo baada ya kupokea kilio cha wananchi kupitia kwa Ndg. Jumanne Abdallah Maghembe Mbunge wa Jimbo la Mwanga.

Akiwa katika tukio la kukabidhi gari Ndg. Polepole amesema Rais Magufuli anawapenda sana wananchi wote bila kubagua vyama vyao na CCM nayo inahimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020 hata katika maeneo yanayoongozwa na upinzani ndio maana gari la kubebea wagonjwa limetolewa katika Kata yenye Diwani wa upinzani ili kuendeleza dhana ya CCM kuwa maendeleo yanayotolewa na Serikali ya CCM hayana Chama. 

Wakati uo huo Ndg. Polepole ametolea ufafanuzi wa masuala, changamoto na fursa za Serikali ya CCM kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga ikiwemo;
Changamoto ya upatikanaji wa mtandao wa simu, ambapo Chama kimeahidi kufuatilia na kupatikana kwa mtandao wa simu katika maeneo ambayo yanayo changamoto hiyo ya mtandao wa simu ikiwepo Kata ya Lang'ata.

Katika masuala ya uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu napo Chama kimekemea vitendo vya baadhi ya   kuwanyanyasa wananchi, kupokea rushwa na kutosimamia haki katika zoezi la kudhibiti uvuvi haramu, Chama pia kimewataka wananchi nao kufuata utaratibu na kutii sheria katika matumizi ya Bwawa hilo kwa faida yao na vizazi vyao.

Aidha Ndg. Polepole ameielekeza Halmashauri ya Mwanga kujenga maeneo maalumu ya kupokelea samaki ambapo Serikali itapata mapato na wananchi watafaida kibiashara na kiuchumi, Halmashauri itoe mikopo ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake na itumie ulinzi shirikishi katika kukabiliana na uvuvi haramu katika Bwawa la nyumba ya Mungu. 

"Chama chetu kinahimiza haki na usawa, Halmashauri hamuwezi kutaka kukusanya fedha kwa wananchi bila kuweka fedha, jengeni maeneo maalumu ya kupokelea samaki, mtapata mapato, mtawawezesha wananchi kiuchumi na kibiashara na wekeni utaratibu mzuri wa ulinzi shirikishi katika kupambana na uvuvi haramu kwenye Bwawa  la nyumba ya Mungu", amesema Ndg. Polepole

Huu ni muendelezo wa ziara za kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages