Wednesday, September 14, 2016

WAZIRI MKUU ACHANGISHA ZAIDI YA BILIONI 1.4 KWENYE HARAMBEE YA KUSAIDIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akizungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na jumuia ya wafanyabiashara kwenye harambee ya kuchangisha michango kusaidia walioathirika na tetemeko .
 
Na Nassir Bakari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechangisha na kupokea michango ya zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao jana Jumanne, 13 Septemba, 2016 Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
 
Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz Mlima.

Alisema tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko hilo.

“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema.

Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Alisema Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.
 
Pia Waziri Mkuu aliwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za kikao cha jana kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.

Wakati huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.