Tuesday, October 28, 2014

UFAFANUZI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUHUSU TUHUMA ZILIZOTOLEWA NA GAZETI LA JAMHURI DHIDI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII NA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHE. LAZARO NYALANDU

 TAARIFA RASMI
Katika gazeti la Jamhuri la Jumanne Agosti 19 – 25, 2014 ISSN No. 1821-8156 Toleo No. 150, zilichapishwa taarifa potofu zenye  kichwa cha habari;
  KASHFA IKULU;
·    Nyalandu atumia Leseni ya Rais kuua wanyamapori 704 bure,
·    Watakaouawa wamo pia tembo 8, chui 8, Simba 8, ndege,
·    Wauaji ni Wamarekani marafiki wa Waziri wa Maliasili.
I.   
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuwafahamisha Umma kuwa, tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu  na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na  kasi ya kupambana na ujangili.

Ukweli ni kwamba Familia ya Freidkin ilipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais (Special License/President’s License) ya kuwinda kwa mujibu wa Kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori baada kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya Wanyamapori kutoa kibali maalum kwa malipo au bure. Aidha, kibali hicho hutolewa baada ya Waziri kuridhika kwamba kibali hicho kina maslahi kwa taifa na hakikinzani na sheria na mikataba ya kimataifa kama CITES. 

Kufuatana na Kifungu hicho cha 58 (1) Leseni Maalum hutolewa kwa mtu yeyote kwa masilahi ya kitaifa ikiwemo:-
1.    Utafiti wa kisayansi
2.    Makumbusho
3.    Elimu
4.    Utamaduni na
5.    Chakula wakati wa dharura

Maslahi ya taifa ni pamoja na leseni kutolewa kwa watu mashuhuri kama vile Wakuu wa nchi,  Wafalme, Malkia, Wakuu wa dini pamoja na watu ambao katika utendaji wao wametoa michango yenye manufaa maalum kitaifa au michango mikubwa katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.

Katika utaratibu huu, kwa mwaka 2013 hadi sasa, Leseni ya Rais zimetolwa kwa watu wafuatao:-

Na.    Jina    Kibali Na.    Kampuni iliyowindisha    Bure/Malipo      
1    H.H. Sheikh Abdullah Mohamed Buli Al Hamed    000000657 cha 22/8-6/09/2013    Kilombero North Safaris/Green Mile Safaris    Bure      
2    H. H Sheikh Mohamed Rashid Al Maktoum    0000676 cha 16/01 – 26/01/2014    Ortello Business Corporation (OBC)    Bure      
3    Familia ya Freidkin ya Watu wanane     00006678-85 za 1-21/08/2014    Tanzania Game Trackers Safaris Ltd    Kwa malipo        
4    Kiongozi wa Bohora Duniani            Bure   

Familia ya  Freidkin imekuwa na sifa ya kupewa Leseni ya Rais kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa katika shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori kwa kipindi cha zaidi ya  miaka ishirini iliyopita bila kukoma.

Familia ya Freidkin imekuwa ikitoa mchango huo kupitia Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii iitwayo Tanzania Game Trackers Safaris Ltd. Pamoja na Asasi yake iitwayo Freidkin Conservation Fund (FCF tangu miaka ya 1990).

FCF imekuwa ikitoa michango mikubwa hususan ya kukabiliana na ujangili.
Bw. Freidkin kwa kupitia Taasisi hii amekuwa akichangia na hata kushiriki katika shughuli za kuzuia ujangili na shughuli za kijamii kwa kufanya yafuatayo:-

a.    Kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Wanyamapori katika kazi za kuzuia ujangili amekuwa akichangia mafuta ya doria katika Mapori ya Akiba ya Kizigo, Maswa, Moyowosi, Ugalla na Pori Tengefu la Lake Natron
b.    Kutoa magari ambayo hutumika kwenye kuzuia ujangili
c.    Kutoa helikopta kwa ajili ya kufanya doria kwenye mapori husika
d.    Kuchangia  malipo ya doria kwa askari wa Idara.
e.    Kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii kama vile kujenga vituo vya doria (outposts) na ujenzi wa shule mpya (kwa mfano Kizigo Sekondari/Manyoni)

Vibali vilivyotajwa na Gazeti la Jamhuri la tarehe 19/08/2014, Toleo la 150 vilitolewa kwa familia ya Freidkin ya watu wanane (8) kwa ajili ya uwindaji kuanzia tarehe 1 hadi 21 Agosti 2014 kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kupitia kampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris Ltd

Maeneo hayo yaliyowindwa hayahusiani na ugawaji wa vitalu kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri ya kuwa Waziri Nyalandu amegawa vitalu zaidi ya vitano kwa kampuni moja.. Leseni ya Rais inatuma kuwinda katika sehemu yoyote ile itakayoonekana inafaa kisheria bila kujali idadi ya vitalu husika kwa vile ni shughuli ya mara moja tu.

Uchambuzi wa makala ya gazeti hili ulitaja vipengele kama:-

a)    Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu yenye kicha cha habari;  KASHFA IKULU
Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ametumia Leseni ya Rais kuwaruhusu marafiki zake Wamarekani wanane kuua wanyamapori 704 bila kulipa hata shilingi moja serikalini.

Tuhuma hizi si za kweli.
Ukweli ni kuwa, Pamoja na leseni hii kuitwa Leseni ya Rais kwa Mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974, leseni hiyo haitolewi na Ikulu bali hutolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Maliasili na Utalii na leseni hiyo haikutolewa bure.

b)    Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni ya Rais kwa rafiki zake Freidkin na familia yake pia si za kweli.

Leseni ya Rais ilitolewa kwa familia ya Freidkin na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kwa kuzingatia utaratibu kama walivyopewa watu wengine ambao wamekidhi vigezo kama ilivyoelezwa hapo juu.

Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni la kuwinda wanyamapori 704 bila malipo pia si za kweli.

Ukweli ni kuwa, si kweli kwamba familia ya Freidkin ilipewa leseni bila malipo kwani familia hiyo  ilipewa Leseni ya Rais baada ya kulipia ada ya vibali (permit fee), ada ya nyara (trophy handling fee) na ada ya uhifadhi (conservation fee) na ada ya wanyamapori watakaowindwa ambayo ingelipwa baada ya uwindaji kufanyika kama ilivyo kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (GN No. 243 Kanuni 21 (1),

Utaratibu huu unatumika kwa wawindaji wote wa kitalii.

Idadi ya wanyamapori wanaotolewa kwenye leseni yoyote kupitia kampuni za uwindaji wa kitalii hutolewa kwa kufuata “Safari Package” na siyo wote wanaowindwa kwa kuwa uwindaji ni wa kuchagua kwa kuzingatia ukubwa na ubora wa nyara, umri, jinsia na iwapo wamepatikana eneo husika. Hivyo kama mwindaji anashindwa kupata mnyama mwenye sifa hizo ni kwamba hatawinda mnyama husika hata kama ameandikwa  kwenye leseni. Hii ndiyo tasfiri ya kisheria ya kulipia wanyama watakaowindwa tu na siyo wanaoandikwa kwenye leseni/kibali.

 Aidha, kulingana na sheria, mwindaji anatakiwa kuandika kila mnyama anayewindwa nyuma ya leseni mara tu baada ya kuwinda kwa kuonesha tarehe mnyama alipowindwa, aina ya mnyama, idadi, jinsia, umri na mahali alipowindwa. Kazi hii huhakikiwa na Afisa Wanyamapori na Mwindaji Bingwa (Profesional Hunter) wa eneo husika kwa mujibu wa Kanuni za Uwindaji wa Kitalii.

c)    Tuhuma kuhusu idadi ya wanyama walioruhusiwa kuwindwa ikiwemo kuuwa tembo wanane (8)

Pamoja na familia ya Freidkin kupewa leseni ya Rais kuwindia, hakuna tembo yeyote wala Simba aliyewindwa. Tuhuma kwa Familia ya  Freidkin kuwinda Tembo wanane na simba si za Kweli. Tuhuma hizo zilikuwa na nia ovu ya kumchafua, kumdhalilisha Mheshimiwa Waziri Nyalandu pamoja na familia ya Freidkin.

Ukweli ni kwamba pamoja na kuwa idadi ya wanyama hao walikuwa wameandikwa kwenye leseni iliyotolewa, lakini wanyama hao hawakuwindwa kwa sababu hawakuwa wamefikia ubora wa Nyara inayotakiwa kuwindwa kisheria.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za uwindaji nchini, mnyama tembo anaruhusiwa kuwindwa kwa ajili ya matumizi binafsi na siyo ya kibiashara. Kufuatana na Mkataba wa CITES, Tanzania imekuwa ikiwinda tembo 50 kwa miaka ya 1990 na baadaye kwenye miaka 2000 tembo 200 idadi ya tembo ilipoongezeka.

Hata hivyo, mwezi Juni 2014 Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii alipunguza idadi hiyo kwa asilimia 50% kutokana na kupungua kwa idadi ya tembo wenye ubora wa  kuwindwa. Aidha, uwindaji huo unazingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Uwindaji wa Kitalii. Endapo tembo aliyeandikwa kwenye kibali au leseni hajafikisha viwango stahiki hatawindwa.

d)    Tuhuma ya  Kuruhusu wageni kuwinda katika vitalu ambavyo siyo vya kampuni husika

Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizi zina nia ovu ya kudhoofisha kasi ya kupambana na ujangili.

Ukweli nu kuwa, Freidkin na familia yake waliruhusiwa kuwinda kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kwa sababu hii ndiyo maana Freidkin na familia yake walipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 243 la mwaka 2010 Kanuni ya 19(2) ambalo linaeleza kuwa mwenye Leseni ya Rais anaruhusiwa kuwinda eneo lolote kama atakavyoelekeza Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mantiki hii, si kweli kwamba Mheshimiwa Waziri Nyalandu alikiuka sheria na kugawa zaidi ya vitalu vitano vya kuwindia kwa familia ya Freidkin.

Hivyo, tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambavyo ni vitalu vitano kwa kampuni  si za kweli.

Kwa kuzingatia maelezo hayo hapo juu, kutolewa kwa leseni ya Rais kwa familia ya Freidkin kulizingatia sheria, kanuni na taratibu zote za uwindaji.

Tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Mheshimiwa Waziri Nyalandu kuhusu utoaji wa Leseni ya Rais ya kuwindia kwa familia ya Freidkin, zilikuwa na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na kushusha heshima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri Nyalandu na familia ya Freidkin

e)    Tuhuma kuwa Waziri Nyalandu ameruhusu Tanzania Game Trackers Safari (TGTS) kumilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka kifungu cha 38(7) cha sheria ya wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 pia si za kweli.

Ukweli ni kuwa kampuni ya Tanzania Game Trackers Safari (TGTS) ndiyo iliyotumika kuwindisha familia ya Freidkin kwenye maeneo matano yaliyotajwa juu na si vitalu vinane kama ilivyoandikwa na gazeti la Jamhuri.
Vilevile kama ilivyoelezwa hapo juu kisheria, mtu mwenye leseni ya Rais ya uwindaji anaruhusiwa kuwinda eneo lolote linalofaa kuwinda kisheria bila kujali ukomo wa idadi ya vitalu.
Tuhuma hizi zilikuwa na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na kushusha heshima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri Nyalandu na familia ya Freidkin

f)    Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu ameruhusu uwindaji wa kitalii kufanyika eneo la Makao, sehemu ambayo haijatengwa kama kitalu pia si za kweli.

Tuhuma hizi zinalenga kuchafua jina zuri la Mheshimiwa Waziri na kumpunguzia dhamira, Hari na kasi ya kupambana na ujangili.

Ukweli ni kuwa, eneo la Makao pamoja na kwamba halijatengwa rasmi kama kitalu cha uwindaji, lakini kisheria linaruhusiwa kufanyika shughuli za uwindaji (yaani kwa lugha iliyozoeleka – kuwindwa) kama ilivyo kwa maeneo mengine ya mapori tengefu na mapori ya wazi. Hii ndiyo maana familia ya Freidkin haikugawiwa vitalu bali ilipewa kibali cha kuwinda katika maeneo yaliyotajwa.

2.    Katika gazeti Jamhuri la tarehe 30 machi 2014 toleo namba 129 ilichapishwa taarifa potofu  yenye kichwa cha habari NYALANDU ’ AUZA’ HIFADHI
·    Yeye na lembeli waenda afrika kusini kukamilisha mpango
·    Katibu mkuu njia panda alazimishwa kuidhinisha safari, posho
·    Hifadhi nyingine nazo mbioni kutolewa kwa wawekezaji
    Taarifa hiyo potofu ilielezea kuwa Waziri Nyalandu alikwenda nchini Afrika ya Kusini na kufanya mazungumzo na kampuni ya African Parks Network (APN) kwa ajili ya kuikabidhi uendeshaji wa Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ikiwemo kuuza hifadhi ya Katavi.
    Tuhuma hizi si za kweli.

    Tuhuma hizi zililenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii.

Ukweli ni kuwa  Safari ya Waziri Nyalandu kwenda Africa kusini ilikuwa rasmi na ilifuatia maagizo ya Serikali kuhudhuria mkutano wa African Parks Network (APN) wa uhifadhi ulioandaliwa na  asasi hiyo kwa lengo pia la kuhakiki uwepo, utendaji halisi wa taasisi hiyo na kufanya majadiliano kuhusiana na mapendekezo yao.

Huu ni utaratibu wa kawaida wa utendaji serikalini ambapo taarifa ya safari hiyo iliwasilishwa Serikalini kwa hatua zaidi.

Katika mkutano huo, hakukuwa na mikataba yoyote iliyowekwa na Waziri Nyalandu au maamuzi yoyote ya kukabidhi hifadhi za Taifa kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri.

Tuhuma hizo zilizolenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na Mhe. Nyalandu.

3     Gazeti la Dira jumatatu, Machi 31 – April 6, 2014, liliandika habari yenye kichwa cha habari “Kashfa za Nyalandu zatikisa. Na vichwa vidogo vya habari vilivyosomeka, Adaiwa kumiliki vitalu, kampuni ya “tours”, Aificha chini ya mwamvuli wa Wachina.

Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizo zina nia ovu ya kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Nyalandu na   kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.

4    Taarifa ya kuwa Waziri Nyalandu anatuhumiwa kurefusha msimu wa muda wa uwindaji kuanzia Julai Mosi hadi Machi 30 ambapo ni sawa na muda wa miezi tisa kila mwaka tofauti na muda wa kisheria ambao ni kuanzia Julai Mosi hadi Decemba 31 sawa na miezi 6 kwa mwaka si za kweli.
Ukweli ni kwamba Waziri Nyalandu alitangaza kusudio la kuongeza msimu wa uwindaji kutoka miezi sita kwenda tisa na hii iko ndani ya mamlaka ya waziri kisheria kama ilivyo kwenye Sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake.

Hii siyo mara ya kwanza kwa mawaziri wenye dhamana ya Maliasili na Utalii kurefusha au kufupisha msimu wa uwindaji.

5    Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu ni mmoja wa wafanyabiashara wa Uwindaji na yuko karibu kabisa na wawindaji wenye vitalu nchini hazina ukweli wowote.

Waziri Nyalandu ni waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya Maliasili na Utalii na anapaswa kuwa karibu na wadau wote wa maliasili na Utalii ili kuweza kusimamia vema sekta hiyo. Huwezi kuisimamia vema Sekta husika kwa kuwakwepa wadau husika.

6    Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu anakabiliwa na kashfa ya kujihusisha na ujangili mkoani Singida pia si za kweli

       Ukweli ni kuwa tuhuma hizo zina nia ovu ya kuchafua jina la Waziri Nzyalandu, kumshushia heshima na hadhi yake kwa lengo la kupunguza na kukwamisha jitihada zake za kukabiliana na ujangili uliokithiri hususan mauaji ya tembo na faru.

     Jitihada zilizofanywa na Waziri Nyalandu hadi sasa ni pamoja na kutafuta fedha na vifaa ndani na nje ya nchi ikiwemo helikopta moja na kuwezesha kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kukusanya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo chini ya uratibu wa shirikal a Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ofisi ya Tanzania.

7    Kashfa za kumhusisha Waziri Nyalandu na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye, Rehema Manji kudai kuwa alitishiwa bastola ni kosa kisheria kwani. Waziri Nyalandu hakuwahi kutenda kosa hilo.

Kutajwa kwa mmiliki wa gari namba T 505 BKM kuwa ni la ndugu Lazaro Samwel Nyalandu, mwenye utambulisho wa mlipa kodi (Tin: 105-059-701) si uthibitisho ya kuwa Waziri Nyalandu alihusika kumtishia bastola Rehema Manji. Kashfa hizo zililenga kumchafua, kumshushiaa hadhi  Waziri Nyalandu.
8    Katika gazeti la Jamhuri la Jumanne October 07 – 13, 2014 ISSN No. 1821-8156 Toleo No. 157, zilichapishwa taarifa zenye kichwa cha habari AUNTIE EZEKIEL ATANUA NA NYALANDU MAREKANI.

 Tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu  na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na  kasi ya kupambana na ujangili.

Ukweli ni kuwa, Waziri Nyalandu hakuhusika kwa namna yoyote ile na kile kilichoelezwa na gazeti la Jamhuri “Aunty Ezekiel atanua na Nyalandu Marekani” kichwa cha habari hiyo na vichwa vidogo vya habari vilivyoandikwa vililenga kutoa picha potofu kwa umma ili kumchafua, kumdhalilisha, na kuvuruga amani kwa Waziri Nyalandu na familia yake.

Waziri wa Maliasili na Utalii, akiwa nchini Marekani kikazi, alialikwa kuhudhuria shughuli ya kutimiza miaka minne ya blog ya Vijimambo ambayo inamilikiwa na Watanzania waishio Marekani.

Waandaaji wa shughuli hiyo iliyolenga kutangaza Utalii wa Tanzania nchini Marekani walimwalika Waziri Nyalandu kuwa mgeni rasmi. Mwaka jana kwenye sherehe kama hizo alialikwa Rais mstafu Ali Hassan Mwinyi

Wizara ya Maliasili na Utalii haikuhusika na uratibu wa safari ya Msanii Auntie Ezekiel.

Tarifa hizo zimelenga kuchafua Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu.

Tuhuma za ufisadi, ujangili na matumizi mabaya ya madaraka hazina ukweli wowote. Tuhuma hizo zinalenga kudhoofisha kasi ya Waziri Nyalandu katika kupambana na ujangili.

9    Hoja ya kuwa waandishi wa habari wameshinda na kuwa wameokoa mamilioni ya fedha za umma ambazo zingetumika kulipia mkutano na badala yake mkutano huo ulifanyikia wizarani hazina msingi.
Hoja hizo si za kweli kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Nyalandu anatumia kumbi za wizara kufanya mikutano na wadau.

Mikutano ya wizara ya Maliasili na Utalii inayofanyikia kwenye kumbi za mikutano nje ya wizara, inafuata taratibu zote za Serikali na inategemeana na idadi ya washiriki wa mikutano hiyo na aina ya mkutano husika.

Utaratibu huu ni wa kawaida na hutumiwa na watendaji na viongozi mbalimbali wa Serikali na si upotevu wa fedha za umma kama inavyodaiwa na magazeti husika bila kujua uhalisia wa mikutano, idadi ya watu watakaohudhuria mkutano , na wadau wa mkutano husika.

Mikutano hii imekuwa na manufaa makubwa kwa taifa katika swala zima la kupambana na ujangili

10    Tuhuma ya kuwa waziri anafanyia kazi hotelini si za kweli kwa sababu kiongozi wa serikali wa ngazi za juu anakuwa kazini muda wote bila kujali yuko wizarani ama nje ya wizara.

Tuhuma hizo zinalenga kuchafua jina zuri la Waziri Nyalandu, kumkatisha tamaa na kumpunguzia heshima yake kwa umma ili kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.

Hadi sasa kuna mafanikio makubwa yaliyojitokeza katika suala zima la kupambana na ujangili ikiwemo Kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauaji ya tembo. Idadi ya tembo katika ikolojia ya Serengeti - Maasai Mara imeongezeka, kupungua kwa matukio ya ujangili katika Pori la Akiba  Selous kuanzia mwezi machi 2014 hadi sasa, wadau wengi kujitokeza katika kusaidia suala zima la kupambana na ujangili wa wanyamapori nchi kama Marekani, Ujerumani, China, Uingereza.

Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kwa umma kwamba tuhuma zote zilizotolewa na hata zitakazoendelea kutolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu zinalenga kulichafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na pia kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya gazeti la Jamhuri na chombo chochote cha habari kitakachotoa taarifa za kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu.

TAARIFA HII IMETOLEWA NA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.