LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 24, 2024

BALOZI DK. NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA WAKASUVI MKOANI TABORA, LEO, ASEMA ALIKUWA KIONGOZI SHUPAVU, AWASILISHA SALAM ZA RAIS DK. SAMIA

Uyui, Tabora
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi ni pigo kubwa siyo kwa mkoa huo tu bali kwa Chama, Serikali na taifa zima kwa ujumla.

Amesema, Wakasuvi ambaye amefikwa na mauti akiwa pia Mwenyekiti wa Kamati Ndogo, iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha Chama Cha Mapinduzi, alikuwa mmoja wa viongozi shupavu wa CCM, kuanzia mkoani kwake, hadi ngazi ya taifa.

Balozi Dk. Nchimbi amesema kutokana na uwezo na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na ushirikiano tangu mwaka 2002 Wakasuvi alipochanguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo wa Tabora, aliendelea kuaminiwa hadi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, nafasi aliyokuwa nayo hadi mauti yanamfika.

Amesema hayo akitoa salaam za pole na rambirambi kwenye msiba wa hayati Wakasuvi, kabla ya mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.

Msimba huo uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Kassim Majaliwa akimuwakilisha Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo nchini Namibia kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Dk. Hage Geingob.

“Kiwango cha kuaminiwa Mzee Wakasuvi kilikuwa ni kikubwa sana. Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Mkoa na Mjumbe wa NEC ya CCM Taifa, pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Lakini pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha chetu. Makamu wake alikuwa ni Mzee Wassira (Steven).

Watu wanauliza maswali mbalimbali. Mimi ilikuwa imepangwa niwatembelee na kuonana nao Jumatatu (keshokutwa). Wakaniulize maswali waliyopanga kuniuliza nami nilikuwa nimejiandaa kwenda kujibu maswali hayo,” akasema Balozi Dk. Nchimbi na kuongeza;

“Mzee Wakasuvi ameanza uongozi muda mrefu sana tangu, Umoja wa Vijana. Wenzake wengine wako hapa kina Mzee Lukuvi (William), Mzee Luhavi (Rajabu) na wengine. Muda wote alikuwa anahamasisha maendeleo ya nchi yetu na kuchochea uimara wa CCM.

Chama kimepoteza, Serikali imepoteza na Wananchi kwa ujumla wamepoteza kiongozi mahiri na shupavu. Tuna kila sababu ya kulinda na kuenzi kazi zake, kwa kuendelea umoja, kushikamana, amani na utulivu thabiti bila kujali tofauti zetu za kisiasa, dini, kabila wala maeneo.”

Mbali ya salaam hizo, Balozi Dk. Nchimbi pia aliwasilisha salam za Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia akisema msiba huo umemgusa moja kwa moja lakini hakuweza kuhuduria kutokana na ratiba ya majukumu mengine ya kikazi, nje ya nchi.

“Kama ambavyo imekuwa kawaida kwa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kila kunapojitokeza jambo kama hili, hapa pia amejitoa kwa uzito mkubwa tangu tu zilipotokea taarifa za msiba huu. Washauri wake wa siasa wote wako hapa.

Pia ametutuma sisi wasaidizi wake, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali na mimi kwa upande wa Chama kuleta salaam zake za pole kwa wana CCM wote na Tabora kwa ujumla wenu. Nasi pia tutafikisha salaam na shukrani zenu mlizompatia yeye kwa jinsi alivyojitoa kushiriki katika msiba huu,” akasema Balozi Dk. Nchimbi.

Wakasuvi alifikwa na mauti juzi, Februari 22, 2024, baada ya kuugua kwa muda mfupi, ambapo pia alikuwa katika maandalizi ya kusafiri kikazi kwenda mkoa wa Pwani, Jumapili, Februari 25, 2024 kwa ratiba ya majukumu mengine ya kazi za Chama.

Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiweka udongo katika kaburi lenye mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi, wakati wa maziko ya kiongozi huyo yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akishiriki katika mziko ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi, yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora. Kulia kwake ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiifariji familia ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi, wakati wa maziko ya kiongozi huyo yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
Waombolezaji wakisali 'salat jeneiza' kabla ya kwenda kumpumzisha katika nyumba yake ya milele, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi, wakati wa maziko ya kiongozi huyo yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakiwa na waombolezaji wengine kwenye msiba huo.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akitoa pole na rambirambi kwa ndugu, jamaa, Marafiki na Wana CCM wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi,  yaliyofanyika leo Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
Baadhi ya viongozi na waombolezaji mbalimbali wakiwa kwenye msiba huo. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM mstaafu Daniel Chongolo.
Waombolezaji wakiwa kwenye msiba huo. (Picha na Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM)

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages