LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 7, 2021

MAJALIWA: RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI

Na Mwandishi Maalum, Kilwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana katika kila kijiji ikiwa ni utekelezaji wa kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani hivyo ni lazima kuchukua hatua ya kuhakikisha pale ambako hakuna maji safi na salama yanapatikana.

Kufuatia dhamira hiyo, Waziri Mkuu, amemwagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina wa maeneo ambayo yatawezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo.,

Amesema na kutoa maagizo hayo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa vijiji vya Nasaya, Chumo na Kipatimu akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi.

“Utafiti lazima ufanyike ili tujue wapi tunapa maji, Rais Samia anatoa pesa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, piteni mpime maeneo yote mtafute vyanzo na mtuambie maji yako kiasi gani, mitambo na wataalam tunao", alisema Waziri Mkuu.

Awali, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chumo, Waziri Mkuu ametoa onyo kwa wafugaji wenye tabia ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kuwataka viongozi kuweka utaratibu wa kukutana na wafugaji na kuwaelimisha ili wafuge kulingana na ukubwa wa maeneo yao.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango wake wa kuunganisha mtandao wa barabara Wilaya kwa Wilaya baada ya kukamilika kwa mpango wa kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami. "Meneja wa TANROADS nimeona ukarabati unaoendelea hakikisha barabara hii inafanyiwa ukarabati wa mara kwa mara na iwe inapitika kipindi chote", alisema.

Akiwa katika kijiji cha Miteja Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa asimamia ujenzi wa Kituo Shikizi cha Masaninga ambacho kimejengwa kwa nguvu ya wananchi hadi kufikia hatua ya upauaji.

Waziri Mkuu amesema hadi kufikia tarehe 4 ya mwezi Novemba shule hiyo iwe imekamilika na kuchangia shilingi milioni tano ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za wananchi wa kijiji hicho.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kusindika vinywaji cha Hopaje kilichopo Nangurukuru Wilayani Kilwa, ambapo amesema Mheshimiwa Rais Samia ameendelea na utekelezaji wa sera ya viwanda na kuvutia wawekezaji ili kukuza uchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Rais Samia Suluhu Hassan

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages