LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 8, 2020

WAZIRI MPANGO: PPRA WANAFANYA KAZI NZURI, WAELIMISHE UMMA ZAIDI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, leo Agosti 8,2020 ametembelea banda la Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwenye Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane, yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Waziri Mpango amesema kuwa anatambua kazi nzuri inayofanywa na PPRA na amewataka kuongeza wigo wa kutoa elimu ya ununuzi wa umma kupitia vyombo vya habari. 

Aidha, Mheshimiwa Waziri amesema kuwa anasoma Ripoti za ukaguzi unaofanywa na PPRA, na amewataka kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo wanayoyaibua.

“Mnafanya kazi nzuri sana, Ripoti zenu nimezisoma vizuri sana na mnaniandikia vizuri. Lakini, msiishie kwenye kuibua matatizo tu, muwe pia sehemu ya kuyatatua,” amesema Waziri Mpango.

Akizungumzia maagizo ya Waziri Mpango, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Mahusiano kwa Umma, Bi. Winifrida Samba, alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa pongezi alizozitoa kwa Mamlaka hiyo na kuahidi kufanyia kazi maagizo yake. 

Agosti 7, 2020, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga alitembelea banda hilo na kueleza kuwa anatambua kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka hiyo. Aliwataka kuendelea kufanya kazi nzuri na wasipunguze kasi kutokana na kufisiwa. 

“Kweli kazi yenu tunaiona, mnafanya kazi nzuri. Zamani kidogo kulikuwa na changamoto, lakini kwa sasa kazi yenu tunaiona na tunaitambua, kwa hilo we commend you (tunawapongeza),” alisema Profesa Luoga. 

Viongozi wengine waliotembelea banda la PPRA na kuwapongeza ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani, Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagin, Katibu Tawala wa Wilaya ya Busega, R. Rutagumirwa, Katibu Tawala wa Meatu, A. Rutaihwa. 

Wadau na wananchi mbalimbali walipewa elimu na kuhamasishwa kuwa sehemu ya usimamizi wa ununuzi wa umma, kwa kutoa taarifa PPRA pale ambapo wataona kuna dalili za uvunjifu wa sheria.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages