LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 23, 2019

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 16 KWA MKURUGENZI ROMBO


Na Mwandishi Maalum, Rombo
 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa (pichani) ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John awe amepeleka kwenye kijiji cha Holili mgawo wa asilimia 20 sawa na sh. milioni 114 zinazotokana na mauzo ya madini ya pozolana.

Kulingana na agizo hilo Mkurugenzi huyo wa wilaya anatakiwa awe amewasilisha fedha hizo kabla ya Machi 10, mwaka huu.

Ametoa maagizo hayo leo Februari 23, 2019,  wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Maagizo hayo ameyatoa baada ya wananchi wa kijiji hicho cha Holili kuwasilisha malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili Halmashauri hiyo iweze kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo ya madini hayo yanayochimbwa kijijini kwao.

 “Mkuu wa wilaya, simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dk. Anna Mgwira) nataka nipate taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.” amesema Waziri Mkuu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi kutenga muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini kusikiliza ili kuzupatia ufumbuzi kero zinazowakabili.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema hali ulinzi na usalama katika mpaka huo si nzuri, Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo, hivyo ni muhimu kwa wananchi washirikiane katika kuulinda mpaka huo.

Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaokamatwa wakipita au kuingiza mizigo kupitia njia zisizo rasmi kwa sababu hao ndio wanaopitisha silaha.

Waziri Mkuu amesema wananchi wa Tanzania na Kenya hawajazuiwa kufanya biashara upande wowote bali wanatakiwa wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika nchi husika ikiwa ni pamoja na kutumia njia rasmi.

Amewataka viongozi na watendaji waliopo maeneo ya mipaka huo wa Holili wawe makini kwa sababu mpaka huo hauko salama na kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yapo kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages