LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 23, 2019

MKUCHIKA AWASHAURI MAOFISA UTUMISHI KUINGIZA TAARIFA SAHIHI ZA WATUMISHI KWENYE MFUMO SHIRIKISHI WA TAARIFA ZA KIUTUMISHI NA MISHAHARA (HCMIS)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika amewakumbusha Maafisa Utumishi kuingiza taarifa sahihi za watumishi kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ili kutozalisha watumishi hewa na kupunguza kero kwa wastaafu katika kupata haki zao kama inavyostahili.

Mhe. Mkuchika ameyasema hayo wilayani Ruangwa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, kabla ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, endapo maafisa utumishi watashindwa kuingiza taarifa sahihi za watumishi kwenye mfumo wa HCMIS itasababisha kupoteza taarifa na ikitokea mtumishi kufariki au kustaafu itapelekea Ofisi ya Rais Utumishi kukosa taarifa sahihi za mtumishi huyo wanapotaka kuandaa stahili zake.

“Niwakumbushe maafisa utumishi nchini kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu kwa kuwahudumia ipasavyo watumishi wa umma walio katika maeneo yenu ya kazi na wananchi kwa kutoa huduma bora kwa wakati na bila upendeleo,” Mhe. Mkuchika amesema.

Aidha, Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, endapo maafisa utumishi watatekeleza wajibu wao ipasavyo, watumishi wastaafu watapata haki yao ya kulipwa mafao kwa wakati kama inavyostahili na kuwahimiza maafisa utumishi kufuatilia mafao ya watumishi wastaafu kwa moyo bila kulazimishwa wala kutaka rushwa.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa, ili Serikali iweze kufanikisha zoezi la ulipaji mafao kwa mtumishi mstaafu kwa wakati na kwa usahihi, ni wajibu wa Afisa Utumishi kuhakikisha taarifa zilizopo kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ni sahihi.

“Si jambo zuri kwa mtumishi kusafiri kutoka kituo chake cha kazi kwenda Ofisi ya Rais Utumishi, Dodoma kufuata huduma ambayo Afisa Utumishi anaweza kuitatua,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa, endapo mtumishi atafuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi, atamrudisha mtumishi huyo kwenye kituo chake cha kazi ili jambo lake lifanyiwe kazi na Afisa Utumishi husika.

Ameongeza kuwa, Serikali imetoa mafunzo ya matumizi ya mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kwa maafisa utumishi lakini mpaka sasa, Ofisi ya Rais Utumishi imekuwa ikipokea malalamiko ya watumishi wanaosafiri kutoka vituo vyao vya kazi kwenda Dodoma kuangalia taarifa zao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) yuko katika ziara ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages