LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 23, 2019

MAKAMU WA RAIS AZIAGIZA HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUTOA ASILIMIA 10 YA MAPATO YAKE KWA WANAWAKE, VIJANA NA WALEMAVU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa asilimia 10% ya mapato yake kwa Wanawake, Vijana na Walemavu kwa mujibu wa sheria.


Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika Viwanja vya TASAF wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

“Niagize Halmashauri zote kuhakikisha zinatoa fedha hizo kama ilivyopangwa bila riba yeyote kwani fedha hizi zipo kisheria na kwa kutozitoa ni kuvunja sheria”alisema Makamu wa Rais.

Aidha, amesisitiza Halmashauri kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha fedha zinazokopeswa kwa vikundi zinarejeshwa kwa kuwa lengo la fedha hizo ni kuwanufaishwa walengwa zaidi huku akishauri kuwepo na makundi yenye mradi unaoleta tija kwa manufaa ya wengi.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kutoharibu mazingira kwa kukata miti kwani hasara ya kukata mti ni kubwa kulikoni faida wanayoipata hivyo amewashauri kutumia teknolojia mpya ya Solar na Umeme kama ilivyoshauriwa na wataalamu.

Wakati huohuo Mbunge wa Jimbo la Sikonge ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph Kakunda amesema mpaka 2021 kwa mara ya kwanza vijiji vyote wilayani Sikonge vitapata umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Kakunda ameleeza namna wananchi wa Jimbo lake walivyoridhishwa na kasi ya maendeleo ambapo Serikali imetoa pesa katika miradi ya afya, miradi ya elimu na kuboresha miundombinu ya barabara.

Pia alielezea Vipaumbele ambavyo wamejiwekea jimboni kwake katika kukuza fursa za kimaendeleo, vipaumbele hivyo ni kuanzisha viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo, pili viwanda vya vifaa vya majumbani na ujenzi na tatu ni viwanda vitakavyoajiri watu wengi kwa wakati mmoja.

Kwa upande mwingine Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kurudisha uchumi wa madini kwa Watanzania.

“Wananchi changamkieni kuwekeza kwenye uchumi wa madini, lipeni kodi kwa maendeleo ya Taifa letu”.  alisema Waziri huyo.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya hiyo,alikabidhi hundi ya shilingi milioni 40 kwa vikundi 11 vya ujasiriamali  na kuzungumza na wananchi.

Makamu wa Rais ameongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Naibu Waziri Maji Mhe. Juma Aweso, Naibu Waziri Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelline Mabula na Naibu Waziri TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages