HABARI MPYA

Your Ad Spot

Nov 21, 2018

DK. ABBAS AWATAKA WAANDISHI KUZINGATIA KIKAMILIFU SHERIA YA HABARI

Na Grace Semfuko-MAELEZO 
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi (Pichani), amewataka waandishi wa habari kutumia haki na wajibu wao katika kulinda maadili yao ya uandishi na kutotumia taaluma yao kukejeli na kuchafua watu wengine.

 Amesema sheria mpya namba 12 ya mwaka 2016 ya huduma za vyombo vya habari kifungu cha 7 ingawa inawapa Waandishi wa Habari kukusanya, kuhariri na kusambaza habari lakini haiwapi fursa waandishi hao kuandika habari ambazo zinachafua wengine.

Dkt Abbasi aliyasema hayo katika mahojiano na kipindi cha Hallow Tanzania kinachorushwa na radio ya Uhuru FM ya Jijini Dar es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali Nchini.

 “Sheria Mpya ya Habari inawapa fursa Waandishi kufanya kazi zao za kukusanya,kuhariri na kusambaza habari,sheria hii haijamnyima Mwandishi wa Habari kupata habari, lakini pia haijatoa fursa za kusambaza habari za kukejeli na kuchafua wengine, sheria itachukua nafasi yake kwa atakaebainika kufanya hivyo” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali. 

 Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilichukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni sehemu ya kulinda maadili ya uandishi wa habari na kuvitaka vyombo vingine kuendelea kuheshimu, kulinda na kutetea maslahi ya Taifa.

Akihojiwa na Mtangazaji wa kipindi hicho Aggrey Manzi kuhusiana na baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii katika kuchafua wengine, Dkt Abbasi alisema sio sahihi kutumia mitandao hiyo katika kuona wengine hawafai, bali mitandao itumike kutangaza habari za Maendeleo. 

Kuhusu wanaobeza maendeleo ya nchi yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli swali lililoulizwa na Mkuu wa Vipindi wa radio hiyo Abdallah Hussein, Dk. Hassan Abbasi alisema Serikali itaendelea kufanya Maendeleo na kwamba wanaobeza hawazuii utekelezaji huo.

 “Walisema hakuna ndege, ziliponunuliwa pia walisema kuwa nani atapanda, wakasema hakuna miundombinu ya barabara inajengwa bado wanasema, pia daraja la Mfugale limejengwa, Mradi Mkubwa wa umeme wa Stiglers Gorge unajengwa, Reli ya Kisasa ya standard Gauge inajengwa lakini bado wanasema, waache waseme tu, hawatuzuii kufanya miradi ya Maendeleo kwa ajili ya wananchi”

 Akizungumzia kuhusu ukuaji wa uchumi kwa wananchi mmoja mmoja swali lililoulizwa kwa njia ya simu na Abdallah Athumani Mkazi wa Chalinze Dkt Abbasi alisema ukuaji wa uchumi unatokana na kuimarisha miradi ya Maendeleo na kwamba wakazi wanaponufaika na miradi hiyo uchumi unakua kwa mtu mmpja mmoja. 

 “Unapoenda kutibiwa kwa gharama nafuu katika Hospitali ambazo zimejengwa na Serikali unakuwa umehifadhi fedha zako ambazo zitatumiwa kwa matumizi mengine hii ina maana umeepukana na matumizi makubwa ya gharama za hospitali, tunaposema elimu bure ina maana Mzazi halipii gharama za elimu na fedha hizo zinafanya kazi nyingine, kwa ujumla uchumi umekua kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages