LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 1, 2018

MPINA AJA NA MIKAKATI 15 YA MAPINDUZI MAKUBWA KWENYE SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiwaonyesha Mkakati  wa kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake baada ya kuuzindua katiika ukumbi wa VETA Dodoma.
Kikosi kazi  kilichoandaa  mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ( aliyekaa katikati)kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Bi Selina  Lyimo, kushoto Kaimu Katibu Mkuu Uvuvi Bwana Julius Mairi. (Picha  na John Mapepele) .

Na John Mapepele
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua mikakati 15 itakayotumika kama nyenzo ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo na kuleta mageuzi makubwa na ya muda mfupi kwenye sekta za mifugo na uvuvi kabla ya kumalizika awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano mwaka 2020.
Mikakati hiyo ni pamoja nakudhibiti magonjwa ya mifugo chanjo na viatilifu, mpango kazi wa kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake, mkakati wa usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini, mkakati wa upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo pamoja na mkakati wa kuboresha na kuzalisha kwa wingi ng’ombe wa nyama na maziwa kwa njia ya uhimilishaji.
Mwingine ni mkakati wa kudhibiti na kuondoa migogoro baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, mkakati wa kuboresha uzalishaji wa kuku,mkakati wa kuanzisha na kuwezesha ushirika wa wafugaji, mkakati wa kuendeleza ukuzaji wa viumbe kwenye maji pamoja mkakati wa kufufua Shirika la Uvuvi nchini TAFICO
Akizungumza jijini Dodoma mara baada ya kuzindua mikakati hiyo, Waziri Mpina ameiagiza wizara hiyo kuunda kikosi kazi kitakachosimamia utekelezaji wake na kwamba kila baada ya miezi mitatu kufanyike tathmini na kwa watumishi wataoshindwa au kukwamisha utekelezaji wa mikakati hiyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na taratibu. 
Alisema mikakati hiyo ikikamilika Serikali itaweza kukusanya zaidi ya sh bilioni 100 kwa mwaka zitokanazo na sekta za mifugo na uvuvi tofauti na sh bilioni 30 zilizokusanywa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 ambapo kwa mwaka 2017/2018 Serikali imeweza kukusanya sh bilioni 46 baada kufanyika Operesheni Sangara na Nzagamba.
Hivyo Waziri Mpina alisisitiza kuwa utoroshaji wa mazao ya mifugo nje ya nchi, uvuvi haramu,mifugo kufa kwa kukosa tiba sahihi za magonjwa kwa wakati havitapata tena nafasi chini ya uongozi wake huku ulinzi wa rasilimali za mifugo na uvuvi ukiimarishwa kwa kuweka vizuizi katika njia zote zilizobainika kuhusika na utoroshwaji huo.
Alisema udhibiti wa magonjwa ya mifugo utawezesha kuongeza uzalishaji kuanzia ndege wafugwao, mbuzi, kondoo,ng’ombe na kuchochea uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo hapa nchini na kuwezesha upatikanaji wa ajira,kodi na upatikanaji wa bidhaa za mifugo kwa gharama nafuu.
Waziri Mpina alisema ni aibu kwa Taifa ambalo asilimia 37 ya nchi yake ni maji na yenye uoto wa asili mzuri lakini tunashuhudia mifugo ikidhoofika na mingine hata kufa kwa kukosa maji na malisho hivyo mkakati huo utatoa majawabu ya changamoto hiyo.
Pia alishangazwa na kitendo cha baadhi ya watu wakihodhi mashamba ya mifugo ya Serikali waliobinafsishiwa na kubadilishiwa matumizi na kwamba kwa miaka mingi wameshindwa kuendeleza mashamba hayo hivyo Serikali itayataifisha yote na kurejeshwa serikalini ili yatumike kulishia mifugo.
Pia mikakati hiyo itamaliza kabisa tatizo la wafugaji kukosa haki ya kupata malisho kutokana na migogoro ya ardhi huku akitolea mfano mnada wa Pugu wenye ukubwa wa ekari 1,900 lakini sasa zimebaki ekari 108 tu baada ya wananchi wengi kuvamia eneo la mnada na kugeuza makazi.
Waziri Mpina alisema mikakati hiyo ndio itakuwa mwarobaini wa matatizo yote yaliyokuwa yanakabili sekta ya mifugo na uvuvi , na kuziagiza halmashauri zote nchini nazo zishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati ili kuiwezesha sekta ya mifugo na uvuvi kutoa mchango unaostahili katika pato la taifa.
Hivyo Wizara itaandaa mafunzo kwa maofisa Mifugo na Uvuvi kutoka katika halmashauri zote nchini mwezi Agosti ili kuwawezesha kuufahamu mkakati huo na kuutekeleza kwa umakini na kwa wakati.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu-Mifugo, Celina Lyimo alisema kuandaliwa kwa mikakati hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mpina alilolitoa Julai 6 mwaka huu la kutaka kuandaliwa mikakati ya kuwezesha kuwepo mageuzi katika sekta hizo na kuwataka watumishi wa wizara hiyo kuifanyia kazi kwa wakati weledi na uadilifu ili kupata matokeo chanya katika kipindi kifupi.
Naye Kaimu Katibu Mkuu-Uvuvi, Julius Mairi alisema mikakati hiyo itawezesha sekta za mifugo na uvuvi kuwezesha kuongeza pato la Taifa na mtu mmoja mmoja na kumshukuru Waziri Mpina kwa uongozi wake thabiti uliolenga kuona kunakuwepo mageuzi ya haraka kwenye sekta hizo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages