LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 12, 2018

WAZIRI MKUU ATAKA MAAFISA UGANI WAWEZESHWE

Awataka wasimamie mifumo rasmi ya ununuzi wa mazao

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ofisi za maafisa ugani zinapaswa kuwepo walipo wakulima, wafugaji na wavuvi na kwamba maafisa ugani katika ngazi zote lazima wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Julai 12, 2018) wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa maafisa kilimo, mifugo na uvuvi kutoka Tanzania Bara ulioanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma. Mkutano huo unahudhuriwa na washiriki 570.

“Maafisa ugani katika ngazi zote lazima wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu kutekeleza majukumu yao. Wataalam wa Wizara washuke hadi ngazi ya mikoa na Halmashauri kusaidiana na waliopo kwenye ngazi hizo.

“Walioko ngazi ya mkoa washuke mara kwa mara hadi ngazi ya Halmashauri na ngazi ya Halmashauri ishuke na kushirikiana na maafisa ugani wa kata na vijiji kuelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu utaalam na maarifa yanayohitajika katika kuendeleza sekta hizi kibiashara,” amesema.

Amesema wakulima, wafugaji, na wavuvi hawana budi kupatiwa mbinu bora kuanzia hatua ya uzalishaji hadi kupata masoko ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi zenye tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesisitiza kwamba maafisa ugani ni lazima wawe na orodha sahihi ya wakulima, wafugaji na wavuvi wote kuanzia ngazi ya kitongoji na aina ya mazao wanayoshughulikia, malengo ya uzalishaji na utekelezaji.

“Maafisa ugani wawe na takwimu sahihi za aina na kiasi cha mahitaji ya teknolojia na  pembejeo za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yao lakini pia wasaidie kuunganisha vikundi vya wakulima, wafugaji, wavuvi na kuunda ushirika imara ili kuendeleza juhudi za kufufua ushirika kama mkombozi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.”

“Ukiwa na ushirika imara hata kama unataka kuwapatia taarifa ya haraka kuhusu ongezeko la bei, au tarehe ya mnada inakuwa rahisi kwa sababu wana Mwenyekiti wao au Katibu wao na kupitia kwake, wote wanaweza wakaitishwa na kupewa taarifa kwa haraka,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka maafisa ugani waende wakasimamie mifumo rasmi ya ununuzi wa mazao ili kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri za mazao yao.

“Hatutaki kusikia watu wanatumia mifumo isiyo rasmi kama chomachoma (kwenye ufuta), butura(kahawa huko Karagwe), katakichwa(kahawa Moshi), kangomba (korosho) na vishada (tumbaku). Nenda kapambane nao, wewe ni afisa wa Serikali na hupaswi kuacha wananchi wanateseka,” alisema.

“Nenda kahimize mfumo wa kuuza mazo kwa ushirika badala kuruhusu wanunuzi kwenda kwa mkulima mmojammoja. Pia mtusaidie kufafanua dhana ya Stakabadhi za mazao Ghalani kwamba siyo malipo ya papo kwa papo. Muwaeleze wakulima kwamba wanapeleka mazao pake wakati wakisubiria bei iwe nzuri, siyo kwamba wanakopwa,” amesisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Selemani Jafo alisema Aprili mwaka huu, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa agizo la kuwa na viwanda 100 kwa kila mkoa na kubaini kuwa umefikia 49.4 ndani ya miezi mitatu tu.

“Tarehe 20 Aprili, 2018, tulifanya kikao cha kwanza cha utekelezaji wa wa agizo la kila mkoa uhakikishe unajenga viwanda 100 vidogo na vya kati. Kwenye agizo hilo, tulilenga malighafi za viwanda hivyo zitokane na mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo. Agizo hilo lilitaka wakuu wa mikoa wawe wamelitekeleza kati ya Desemba 2017 na Desemba 2018; na kufikia Aprili 2018, viwanda 1,280 vilikuwa vimeshajengwa sawa na asilimia 49.4 ya lengo tulilojiwekea,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages