Rais Magufuli ametumia mamlaka yake kwa mujibu wa Ibara ya 148 (2)(a) ya Katiba na kifungu cha 29 (5) cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa.
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Luteni Jenerali Paul Massau amesema kati ya waliohitimu mafunzo hayo, 115 ni wanaume na 6 ni wanawake.
Amesema watano kati yao wametoka nchi za Rwanda, Uganda na Eswatin.
Massau amesema wanafunzi 87 waliachishwa mafunzo kwa sababu mbalimbali ikiwamo magonjwa, kutofikia viwango vya ufaulu, kukimbia mafunzo na utovu wa nidhamu.
“Maofisa waliotunukiwa kamisheni leo wana viwango tofauti vya elimu; shahada ya uzamili yupo mmoja, shahada ya awali 79, stashahada ya juu 4, stashahada 8 na kidato cha sita 31,” amebainisha mkuu huyo wa chuo.
Rais Magufuli ametoa zawadi kwa maofisa waliofanya vizuri kwenye mafunzo ambao ambao ni aliyefanya vizuri kwenye mafunzo, Daniel Meshack; aliyefanya vizuri darasani, Emmanuel Kakuba na aliyefanya vizuri kwenye medani, Ramadhan Kakombe.
Wengine ni aliyefanya vizuri kutoka nchi jirani, Armstrong Mwesige kutoka Uganda na ofisa mwanamke aliyefanya vizuri, Beatrice Kipinge.
Hadi sasa Rais Magufuli amefanya zoezi hilo kwa mara nne la kuwatunuku kamisheni maofisa wa jeshi, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waliohudhuria hafla hiyo ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, katibu mkuu wa wizara hiyo, Florence Turuka na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo.