LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 3, 2018

MARAIS WA IRAN NA USWISI WATAKA KUDUMISHWA MAKUBALIANO NYUKLIA YA JCPOA

Marais wa Iran an Uswisi wametilia mkazo udharura wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama matunda makubwa ya kisiasa na kusema, kulindwa kwa makubaliano hayo kuna manufaa kwa usalama na amani ya kimataifa.
Rais Hassan Rouhani ambaye alasiri ya leo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Bern akiwa pamoja na mwenyeji wake wa Uswisi, Alain Berset, ameashiria kwamba miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa kati ya pande hizo mbili ni kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na udharura wa nchi zote kulinda na kuheshimiwa makubaliano ya kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hususan azimio nambari 2231 na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuheshimu makubaliano ya JCPOA maadamu maslahi yake yanadhaminiwa na maadamu itapewa dhamana inayohitajika katika uwanja huo. 
Katika kikao hicho ambacho kimefanyika baada ya Iran na Uswisi kutia saini hati tatu za ushirikiano katika nyanja za sayansi, afya na uchumi, Dakta Hassan Rouhani amesema ana matumaini kwamba, uhusiano wa kifedha, kibenki, kibiashara, kiutamaduni, uwekezaji na utalii wa baina ya pande hizo mbili utapanuliwa zaidi.
Rais Rouhani amesema kuwa, matamshi yanayotolewa na viongozi wa Marekani dhidi ya Iran ni bwabwaja  tupu na kusisitiza kuwa: Ni makosa na ufinyu wa mantiki kufikiria kwamba nchi zote zitauza mafuta isipokuwa Iran. 
Rouhani na Alain Berset
Kwa upande wake, Rais wa Uswisi amezungumzia suala la kubuniwa ramani ya njia ya kustawisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika masuala ya kiuchumi, kifedha, kielimu, kiufundi na sekta ya uhajiri na kusema: Mazungumzo yake na mwenzake wa Iran yamegusia masuala mbalimbali hususan makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na matokeo ya kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano hayo. Alain Berset amesema kuwa, Uswisi itaendelea kuhesiemu na kutekeleza makubaliano hayo na kwamba mapatano ya JCPOA yalitiwa saini na nchi kadhaa na kupasishwa na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages