HABARI MPYA

Your Ad Spot

May 21, 2018

MWENYEKITI WA CCM RAIS DK MAGUFULI APOKEA RIPOTI YA TUME YA KUTATHMINI NA KUHAKIKI MALI ZA CHAMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Mei, 2018 amepokea ripoti ya tume aliyoiunda kuhakiki mali za chama, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Bashiru Ally Kakurwa katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam.TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati hiyo imefanya kazi kwa miezi 5 ambapo imekusanya taarifa, imehakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama, imeangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.
Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema uhakiki huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo.
Ameongeza kuwa uhakiki huo umefanyika katika mali za chama zilizo chini ya baraza kuu, jumuiya za chama na kampuni za chama.
Katika ripoti hiyo Dkt. Bashiri Ally Kakurwa amesema tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhilifu, wizi, usimamizi mbaya wa maliutapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.
Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara Ndg. Philip Mangula ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na kusisitiza kuwa ripoti iliyotolewa imedhihirisha kuwa baadhi ya watu waliooneka kukisaidia chama, hawakuwa wanakisaidia bali kujinufaisha.
Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“Nilipokuwa nateua tume hii nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria wakati wa uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya chama.
Kabla ya kuondoka katika ofisi ndogo za CCM Lumumba, Mhe. Dkt. Magufuli amesalimiana na wananchi waliokuwa nje ya ofisi hiyo na kuwahakikishia kuwa CCM imeamua kuhakiki mali zake ili kukiwezesha chama hicho kulinda mali zake na kunufaika na mali hizo.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa CCM imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa dhamira yake ya kupiga vita rushwa na ufisadi na amewaeleza kuwa tume ya Dkt. Bashiru Ally Kakurwa imefanya kazi nzuri.
“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri, ndio maana tumeunda tume ya Dkt. Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana, na ripoti hii tutaipeleka Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na viongozi watoe maelekezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Mei, 2018

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages