LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 4, 2018

TAHLISO YAWAONYA WANAOTUMIA KIFO CHA AKWILINA KISIASA

DODOMA, Tanzania
Jumuiya ya Taasisi za Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO) imewataka wanaotumia kifo cha Mwanafunzi Akwilina Akwilini kisiasa na kutuia mwamvuli wa Jumuiya hiyo kutoa matamko mbalimbali waache vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, Jumuiya hiyo imewaomba wanafunzi kuendelea kuwa watulivu kusubiri matokeo ya  uchunguzi wa kifo cha Akwilina na kujiepusha na maandamano na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Onyo hilo limetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, George Mnali alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kikao na Kamati Tendaji ya Tahliso iliyohusisha Marais wa Serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo hivyo.

Mnali amesema Tahliso ndio chombo kikuu cha kuwasemea wanafunzi wote nchi nzima na sio kikundi kingine chochote.

“Vipo vikundi vingi vimejitokeza na kutoa matamko mbalimbali baada ya kifo hiki cha Mwanafunzi mwenzetu Akwilina Akwilini kutokea, vikundi vingine vikaenda mbali zaidi kwa kuwataka baadhi ya watendaji wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Kujiuzulu jambo ambalo linaashiria vikundi hivyo kutumika kisiasa,”amesema

Ameeleza kuwa haiwezekani kutaka watendaji wa serikali wajiuzulu wakati uchunguzi bado unafanyika na matokeo ya uchunguzi bado hayajatoka.

“Jambo la kusikitisha zaidi kuna baadhi ya vikundi vimejitangaza kwamba vinaungwa mkono na Marais wa Vyuo Vikuu jambo ambalo sio la kweli,”amesema Mwenyekiti huyo

Ametoa wito kwa vikundi vyote vinavyojihusisha na kutumia mwamvuli wa Marais wa Vyuo Vikuu kama kinga yao ilikuuhadaa umma kwamba wanaungwa mkono, viache tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua.

Hata hivyo amesema Tahliso wanasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanyika juu ya kifo cha Akwilina na wanatumai wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amewaomba wanafunzi waendelee kuwa watulivu wakati wanasubiri matokeo hayo nakujiepusha na maandamano na vitendo vyovyote vinavyosababisha uvunjifu wa amani na kuleta mgawanyo miongoni mwa wanafunzi.

Kadhalika, amesema namna bora ya kufikisha hoja ni kutumia njia ya majadiliano kama wasomi badala ya kutumia nguvu ya maandamano kwa kutofuata taratibu na madhara yake ni kusababisha vurugu zisizotakiwa na hatimaye kuhatarisha usalama na hivyo kuathiri jamii kwa ujumla wake.

Mnali amemshukuru Rais John Magufuli kwa kuingilia kati suala hilo la kifo cha Akwilina na kuagiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kuhusika na kifo hicho

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages