LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 28, 2018

JAPAN YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SH. BILIONI 77.3 KUJENGA NEW BAGAMOYO ROAD DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale. baada ya tukio la kusaini mkataba wa msaada wa Shilingi bilioni 77.3 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya njia ya nne ya New Bagamoyo Road kutoka Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam, Februari 28, 2018 
Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania ruzuku ya Yen bilioni 3.78 sawa na Shilingi bilioni 77.3 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.

Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Februari 28, 2018, Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na kushuhudiwa na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Toshio Nagase na Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Barabara nchini-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale.

Mradi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa awamu ya nne ya ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).

Akizungumza baada ya kutiwa saini wa makubaliano hayo, Bw. Doto James amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika itasaidia  kutatua changamoto ya msongamano wa magari yanayotoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

"Upanuzi wa Barabara ya New Bagamoyo si tu kwamba utaondoa msongamano wa magari, bali pia ni kiungo muhimu cha Bandari ya Bagamoyo ambayo itarahisisha usafirishaji wa abiria, mizigo na huduma kutoka Jiji la Dar es Salaam, mkoa wa Pwani na mikoa mingine nchini" Alisema Bw. Doto James.

Ameishukuru Japan kwa msaada mwingine uliotolewa mwezi Septemba, 2017 wa kiasi cha fedha za Japan (Yen) milioni 69 sawa na shilingi bilioni 1.4 ambazo zimetumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hiyo itakayoanza kujengwa

Bw. James ameeleza kuwa  awamu ya kwanza, Japan ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara ya Mwenge pamoja na kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Mlalakuwa, Lugalo na Tegeta.

“Si mara ya kwanza kwa Japan kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km 188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi Dodoma (259.9)” alisisitiza Bw. Doto James.

Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu Yoshida ameeleza kuwa kutolewa kwa msada huo ili kuwezesha awamu ya pili ya ujenzi wa barabara kuanza kutayafanya matokeo ya kujenga barabara hiyo kuanza kuonekana dhahiri ikiwemo kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa ili kuokoa fedha nyingi zinazotokana na changamoto za msongamano huo.

"Ili kukamilisha usanifu wa kina wa mradi huu, nilisaini mkataba wa usanifu wa kina wa mradi wa upanuzi wa barabara ya new Bagamoyo  (Awamu ya Pili) miezi mitano iliyopita, hatimaye sasa ninasaini mkataba wa sehemu kuu ambayo ni ujenzi wenyewe" Alisema Balozi Yoshida.

Balozi huyo wa Japan hapa nchini, amesema mradi huo utasaidia kuboresha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini nchini na kwamba msaada huo ni mwendelezo wa kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania.

Utafiti uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari  yanayokadiriwa 52,000 yanayopita kila siku katika barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages