LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 23, 2018

RAIS DK. MAGUFULI MGENI RASMI KILELE CHA SIKU YA SHERIA


Na Jacquiline Mrisho MAELEZO.
Rais Dk. John Magufuli (Pichani) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Februari Mosi mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yenye maudhui ya ‘Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili’.

“Kila mwaka Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria ambayo huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama, kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi na Rais Magufuli katika viwanja vya Mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar es Salaam,” amesema Jaji Mkuu Juma.

Jaji Mkuu amesema kuwa kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau muhimu katika Sekta ya Sheria watatumia siku tano kuanzia tarehe 27 hadi 31 Januari mwaka huu kwa ajili ya kufanya maonesho yatakayotoa elimu kwa wananchi watakaopata nafasi ya kuhudhuria katika viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyopo jijini humo.

Maonesho hayo yatatanguliwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria yatakayofanyika Januari, 28 mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yatakayoanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Rais Mstaafu Kikwete atazindua rasmi Wiki ya Sheria.

Aliongeza kuwa Wiki ya Sheria inatoa nafasi nzuri kwa wananchi kuzifahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wa sekta ya sheria ili kufanikisha maboresho endelevu ya Mahakama.

Aidha, Jaji Mkuu Juma amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama itaendelea kupokea malalamiko na mawazo kutoka kwa wananchi na kuyafanyia kazi hata baada ya Wiki ya Sheria kuisha.

Wiki hiyo ya Sheria itaenda sambamba na uzinduzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama yaliyokamilika yakiwemo ya Mahakama ya Mwanzo Kawe, Kituo cha kisasa cha mafunzo Kisutu pamoja na Mahakama ya WIlaya ya Bagamoyo, Mkuranga na Kigamboni.

Wadau wengine watakaoshiriki katika wiki ya sharia pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Mafunzo ya Uanansheria kwa Vitendo Tanzania, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
----
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Sheria hapa nchini yanayotarajiwa kufanyika kwa siku tano katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, kuanzia Januari 27, 2018.  Kushoto ni Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Hussein Kattanga.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages