HABARI MPYA

Your Ad Spot

Sep 20, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA-ULINZI UIMARISHWE KWENYE MAENEO YA VIWANDA NA UWEKEZAJI

Waziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,wakati alipowasili katika kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Pichandege Kibaha Mjini.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkurugenzi wa viwanda vya kutengeneza sabuni cha KEDS Pichandege Kibaha Mjini ambae pia ni mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze,Jack Feng.Picha na Mwamvua Mwinyi



Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

WAZIRI mkuu,Kassim Majaliwa amezitaka serikali za vijiji na ngazi nyingine mkoani Pwani,kujikita kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kulinda mali na usalama wa wawekezaji na watanzania kijumla.

Amesema haijajulikana hadi sasa nia na dhamira ya watu wasiojulikana wanaojihusisha kupoteza maisha ya watu ,na ni hatari endapo watajiingiza katika maeneo ya uwekezaji kwani hakuna mwenye uhakika wa azma yao.

Aidha Majaliwa ,ametoa wiki mbili kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa WAMI ,ili kutoa utaratibu na kama sheria inaruhusu kuvunja mkataba ikiwa mkandarasi ameshafikia kiwango cha asimilia 50 ya utekelezaji.

Waziri huyo ,pia ameziagiza halmashauri nchini kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto yatakayosaidia kudhibiti majanga ya moto yanapotokea hususan kwenye maeneo ya uzalishaji na viwanda.

Katika hatua nyingine amelitaka shirika la umeme Tanesco,Dawasco kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme na maji katika maeneo yenye uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.

Alitoa rai hiyo,wakati wa ziara yake ya siku moja ,aliyoifanya mkoani Pwani kutembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Kibaha,na cha kutengeneza vigae Twyford Ceramics Ltd/Pingo,Chalinze ,Bagamoyo.

Majaliwa ,alieleza kuwa ni lazima raia mmoja mmoja na jukumu la kila mmoja kusimamia kulinda nchi kuanzia maeneo wanayoishi .

Alisema serikali imejipanga kuendelea kusimamia amani na utulivu,ambapo amewataka wananchi waiunge mkono serikali kupambana na wahalifu wasio na nia njema na serikali.

“Hatuna uhakika kwa watu hawa wanaofanya vitendo vya ovyo,watanzan ia waungane na serikali,kupambana ili wasije kuingia kwa wawekezaji na kupoteza ndoto za serikali za kupata wawekezaji “alisema Majaliwa.

Akizungumzia tatizo la uhaba wa maji ,alisema mradi wa WAMI ulikuwa ukamilike tangu mwezi July mwaka huu.

Alisema alitembelea mradi huo mwezi juni mwaka huu ukiwa chini ya asilimia 38 na kusema mkandarasi akiendelea kusuasua watamfukuza na kutoa agizo ikifika mwezi huu wafikie asimilia 80.

“Nilitaka kuja mwezi huu lakini nikaambiwa speed ni ndogo na bado hali hairidhishi,na mkandarasi hajamaliza”mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amekuwa akiuliza juu ya kukwama kwa mradi huo” ;”Nimetoa wiki mbili kwa waziri aangalie dhamana ya kampuni kwenye ubalozi wao wa India na kuangalia sheria namna ya kufanya ama kukamilisha mradi kwa muda mfupi uliobaki”alifafanua.

Kuhusu nishati ya umeme Majaliwa,alisema serikali ipo mbioni kutekeleza mradi mkubwa wa umeme stiegler’s gorge katika chanzo cha mto Rufiji, utakaozalisha megawatts 2,100 zitakazoondoa kama si kumaliza upungufu wa umeme uliopo.

Aliitaka halmashauri ya Chalinze,ijipange kwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji.

Kuhusu suala la zimamoto ,Majaliwa alisema mkoa huo kwasasa una viwanda vikubwa hivyo wakati serikali ikipokea changamoto ya uhaba wa vifaa na magari ya zimamoto ,halmashauri ijipange kupitia bajeti zao.

“Viwanda hivi ni vikubwa vinajengwa ,kiwanda hiki cha KEDS kina jengo hilo hapo lenye urefu wa mita 30 juu,tuombe mungu moto usitokee ,unawezaje kuzima moto kwa maji ya kwenye ndoo ,ipo haja ya kuangalia namna ya kutatua changamoto hii”

“Dar es salaam ambako ni mji wa kibiashara serikali itasaidia katika kununua mitambo ya kusaidia kuzima moto kutegemea ukubwa wa majengo yaliyopo”aliongeza Majaliwa.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara,alitoa rai kwa halmashauri ya Mji wa Kibaha kuboresha barabara zilizopita mitaani na kuhakikisha mitaa yote iwe na barabara bora kwa kufumua zisizofaa na kuchonga barabara zenye viwango.

Pamoja na hayo ,Majaliwa alibainisha uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.

Aliwasihi vijana ambao tayari wana ajira kwenye viwanda hivyo kutumia nafasi walizozipata kwa kuchapa kazi .

Majaliwa aliwaomba vijana hao kuchapa kazi na kuwathibitishia wawekezaji kuwa watanzania ni wachapazi na wana uwezo wa kufanyakazi viwandani na hakuna haja ya kuleta watumishi nje ya nchi.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,alimwambia waziri mkuu ,kwamba mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyo ya kuridhisha kwa wawekezaji.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa nishati ya umeme isiyokidhi mahitaji kwani kwasasa mahitaji ni megawatts 73.2 na uliopo ni megawatts 40 ambao bado hautoshelezi.

Mhandisi Ndikilo,alieleza tatizo la uhaba wa vifaa,vitendea kazi na magari kwa idara ya zimamoto na kuhofia endapo janga la moto likitokea kushindwa kuzima moto kwa wakati na kusababisha athari kubwa.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,alilalamikia uzembe na uvivu uliokubuhu katika utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze (CHALIWASA).

Alielezea kuwa,tatizo la maji limedumu kwa takribani miaka 13 sasa hali inayosababisha adha kwa wawekezaji na wananchi kijumla.

Ridhiwani alisema ,haridhishwi na mwenendo wa mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi huo kutokana na kasi yake kuwa ni ndogo na haiendani na maagizo aliyoyatoa waziri mkuu hapo awali.

Akiwa kiwanda cha KEDS ,mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka ,alimuomba Majaliwa kuangalia kwa jicho la tatu kero ya miundombinu isiyo rafiki kwa wawekezaji.

Koka alisema wawekezaji wengi wanakimbilia kuwekeza mji wa Kibaha na mji huo upo usoni mwa barabara kuu ya Morogoro-Dar es salaam lakini bado kuna tatizo la barabara mbovu.

Wakati huo huo ,mkurugenzi mkuu wa kiwanda cha KEDS na Twyford ,Jack Feng alisema asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka hapa nchini .

Alisema katika kiwanda cha KEDS wameshaajiri watu 200 huku wakitarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 katika kiwanda hicho .

‘Ndani ya ujenzi huu kuna kiwanda kingine kikubwa ambacho tutazalisha bidhaa ya pempars na kiwanda kingine tutatengeneza misumali”alieleza Feng.

Alisema hatua ya ujenzi ni nzuri imefikia asilimia 90 na wanategemea kuanza uzalishaji mwezi ujao,na utagharimu dola mil.200 hadi utakapokamilika.

Feng alifafanua,kwenye kiwanda cha Twyford watarajia kuajiri wafanyakazi 4,000 hadi 6,000 mara watakapoanza kuzalisha mwezi Nov mwaka huu,sasa kuna wafanyakazi 1,200.

Mkurugenzi huyo ,alieleza gharama ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Twyford ni dola mil. 56 sawa na bilioni 120 na watauza vigae ndani ya nchi hadi nje ya nchi Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages