Thursday, August 17, 2017

MWANDISHI WA UHURU FRED MAJALIWA ASHINDA UENYEKITI WA CCM KATA YA MZINGA

Fred Majaliwa
NA MWANDISHI WETU
Kaimu Mhariri wa Habari za Michezo na Burudani wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, Wachapishaji wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo  Fred Majaliwa amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzinga wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Majaliwa ambaye ni kaimu Mhariri wa habari hizo katika magazeti ya Mzalendo na Uhuru Wikiendi, ametwaa nafasi hiyo kwa kuzoa kura 59 dhidi ya kura 28 alizopata Mwenyekiti wa zamani wa Kata hiyo, Ignas Agustino, huku Guruneti akipata kura tatu katika jumla ya kura 90 zilizopigwa,
katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki.
 
Katibu Mwenezi wa CCM wa kata hiyo Paul Kapotele, amesema katika uchaguzi huo pia wajumbe 37 wa Halmashauri Kuu walimchagua kwa kura 24 Emmanuel Ryoba Mkunyi kuwa Katibu wa CCM  wa Kata akimuangusha Twaha Kisogo aliyepata kura 13, wakati Kapotele alirejea madarakani baada ya kuzoa kura 29 dhidi ya nane za Gaudencia Malongo.

Aliwataja waliochaguliwa Wajumbe kwenye Kamati ya Siasa kuwa ni Mayasa Subeya, Said Ndembo na Amos Chandala wanaoungana na wengine kwa nafasi zao katika chama na jumuia zake.

Kapotele amesema, baada ya uchaguzi huo, Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo ya Mzinga wilayani Ilala, Dar es Salaam, utafanyika Jumapili ya mwisho wa wiki hii kwa lengo la kuwatambulisha viongozi wapya pamoja na kuwashukuru wapigakura.

Alisema mkutano huo umepangwa kuanza saa 5:00 asubuhi katika ukumbi wa Mkwabi, ambapo pia viongozi wa zamani wa CCM na makada mbalimbali wamealikwa.

"Viongozi wapya tulichaguliwa Agosti 5 mwaka huu kwa hiyo tumeona ipo haja ya kuita tena Mkutano Mkuu ili kuwashukuru wapigakura kisha hapo tuanze kuchapakazi," alisema Kapotele.

Alisema malengo ya uongozi mpya ni kukipa ushindi Chama katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019 na uchaguzi mkuu.

"Baada ya kumalizika uchaguzi tuliangalia namna ya kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wanachama ndio maana tumeandaa mkutano huu kwa lengo la kujenga," alifafanua Kapotele.

Alisema kuwa ana imani baada ya mkutano huo, CCM Mzinga itakuwa imara kufuatia upendo na umoja utakaojengeka miongoni mwa wanachama, viongozi na wapenzi wa Chama.
Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.