LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 1, 2017

RAIS DK. MAGUFULI ATAKA TAASISI ZA SERIKALI NA BINAFSI KUJIUNGA NA MFUMO WA UKUSANYAJI KODI KIELEKTRONIKI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza taasisi za Serikali na taasisi binafsi zinazotumia mifumo ya kielektroniki kujiunga na mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System {e-RCS}) ili kupata taarifa za uhakika na kulinda usalama wake pamoja na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato yote stahiki.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 01 Juni, 2017 alipotembelea Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu (National Internet Data Center) kilichopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam na kisha kuzindua mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki uliotengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa kutumia wataalamu wa ndani.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Tanzania Bara na Zanzibar na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka benki mbalimbali, kampuni za simu na viongozi wa dini.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere kuwa mpaka sasa ni kampuni tatu za simu ambazo ni TTCL, Halotel na Smart ndizo zimejiunga kutumia Mfumo huu na kwamba TRA na ZRB zinatarajia kampuni zote za simu, mabenki na taasisi mbalimbali kujiunga na mfumo wa e-RCS kabla ya mwisho wa mwaka 2017.

“Wanaokusanya mapato wanalalamika kuwa kumekuwa na udanganyifu kwenye utoaji taarifa za wafanyabiashara na wafanyabiashara nao wanalalamika kuwa wamekuwa wakibambikizwa kodi, sasa dawa ya haya yote ni Kituo hiki cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu, jiungeni na mfumo huu kwa sababu sasa kila kitu kinafanywa na mashine, hakuna kuonea mtu, na Mhe. Makamu wa Rais naomba usimamie suala hili” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Pamoja na kutoa agizo hilo Mhe. Dkt. Magufuli ametaka taasisi zote za Serikali zenye vituo vya kumbukumbu (Data Centers) kuoanisha vituo hivyo na amepiga marufuku kuendelea kuanzisha vituo vingine, na badala yake zitumie Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzibana kampuni zote za simu ambazo hazijajiunga na soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) kujiunga haraka ili kuwepo uwazi katika uendeshaji wake huku akisisitiza kuwa Serikali inawapenda wawekezaji lakini ni lazima walipe kodi inavyostahili kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ameungana na Rais Magufuli kuzipongeza TRA na ZRB kwa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki na amewataka Watanzania wote kulipa kodi ili kuinua uchumi.

“Natoa pongezi kwa kuanzishwa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu, kituo hiki ni ‘State of the Art’ nakupongeza pia Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa tangu uingie madarakani umetia msisitizo mkubwa katika kuongeza ukusanyaji wa kodi, na kwa kweli ukusanyaji wa kodi umeongeza” amesema Mhe. Rais Shein.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

01 Juni, 2017 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages