Monday, June 19, 2017

MAKATIBU JUMUIA YA WAZAZI BARA NA ZANZIBAR WAMG'ANG'ANIA BULEMBO

NA HAPPINES MTWEVE, DODOMA
MAKATIBU wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania wamepinga  kwa kauli moja azma ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Alhaj Abdallah Bulembo kutogombea tena nafasi hiyo na kumtaka kubadilisha azma yake hiyo.

Alhaji Bulembo aliweka wazi azma ya kutogombea tena Uenyekiti wa Jumuia ya Wazazi katika kikao cha Baraza Kuu Maalum la Jumuia hiyo hivi karibuni mjini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Makatibu wa Jumuia hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar waliokuwa katika semina ya Siku mbili mjini hapa, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Shinyanga Masanja Salu,  kwa pamoja wanamuomba Bulembo abadilishe uamuzi wake wa kutogombea tena nafasi yake, akisema wanachama wa Jumuia hiyo bado wanahitaji uongozi wake.

“Kwa niaba ya makatibu wa mkoa kabla hujatamka neno sisi tunasema fomu tunakuchukulia, tunakuomba usiwe na shaka, wewe ndio jemedari wetu wewe ndio jembe, wewe ndio Mwenyekiti wetu, wache wachukue fomu uje uone maajabu, hapa tunakukabidhi fedha hizi kila katibu amechanga hela ya fomu wewe usihangaike fomu tunakuchukulia sisi,”alisema Salu.

Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Oganaizesheni ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka Makao Makuu ya Jumuia ya Wazazi Tanzania Daniel Mgaya alisema kupitia watendaji hao wanamuomba afikirie upya uamuzi wake huo, naye kama Mkurugenzi wa uchaguzi atahakikisha anachukua fomu na kuijaza hata kama kiongozi huyo atakuwa nje ya nchi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nikuombe kwa heshima kabisa kupitia kikao hiki cha watendaji ufikirie mara mbili au mara tatu juu ya uamuzi wako, unamuacha nani, kuna miradi ambayo umeanzisha na haijaisha sasa unataka kuicha ni kama umejenga nyumba haijaisha unaondoka kwenye nyumba hiyo,  sasa tunasema angalau uingie kidogo ulale kidogo ndipo uondoke,”alisema Mgaya.

Akifungua semina hiyo, Alhaj Bulembo aliwataka viongozi na wale wote waliomsihi kubadili uamuzi wake, kuvuta subira huku akiahidi kwenda kukaa na wazee kujadiliana nao ili kupata jibu kama agombee au asigombee.

“Hoja ya kugombea au kutokugombea nimeshasema sigombei lakini nasukumwa sana na maneno ya watu wakiniomba nigombee, tulikuja Dodoma hapa mzee wetu Lusinde alisema maneno makubwa sana yaani unakaa kwenye kiti unatamani kulia, napata tabu sana na neno linaloitwa kugombea.

Mtu mzima ukishaaga sigombei kesho unasemaje unagombea, linataka busara kubwa kidogo na sio kwamba kama tafasiri inavyosema kwamba mimi sigombei kwa sababu nasusa, hapanaa,”alisema Bulembo.

Aliwapongeza kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha kufanya kazi pamoja ambapo wamerudisha thamani ya Jumuiya ya Wazazi na kuonekana bora miongoni mwa jumuiya nyingine.

“Tunaelekea kumaliza miaka mitano lakini nitumie nafasi hii kuwapongeza huko mikoani leo jumuiya ya wazazi inaonekana na kuheshimika, katika mikoa tunayopita unakuta jumuiya ya wazazi ndio nguzo ya katibu wa mkoa katika chama, kwa hiyo tunaweza kusema na nyinyi sasa mmetusaidia, mmesimamia nafasi yenu na hiyo hatuwezi kusema ni juhudi ya mtu mmoja bali ni juhudi zetu wote,” aliongeza Bulembo.

Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Seif Shaban Mohamed aliwataka Makatibu kusimamia mikoa yao na kutofanya makosa ya kupata viongozi wabovu.

Katibu huyo alisena, hivi sasa wanakwenda kwenye uchaguzi, uchaguzi ni fitna, hivyo akawasihi waende kusimamia vizuri uchaguzi ili kuepuka kufanya makosa na kujikuta wakipata viongozi ambao hawafai.

Aliwaonya kutojiingiza katika makundi ambao  yanaweza kuwasababishia ambao ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi kufanya maamuzi ambayo si sahihi.

"Wewe ni mwamuzi na kocha angalia sana kabla hujajiingiza uelewe hapa ndipo CCM inapataka na wewe uingie hapo hapo,”alisema Mohammed.

Katika semina hiyo wajumbe walijadili mada mbalimbali ikiwemo kuhusiana na uchaguzi wa Jumuiya hiyo ambao umeanza katika ngazi mbalimbali.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.