LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 5, 2017

WAUAJI RUFIJI WAUA TENA, HALI SIO SHWARI

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, akizungumza (picha na Mwamvua Mwinyi) 

Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji 
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Amiri Chanjale (60)mgambo,mkazi wa Umwe ,tarafa ya Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani ,amefariki dunia kwa kupigwa risasi kichwani na watu wasiojulikaa. 

Tukio hilo ni la sita kutokea wilayani hapo likihusisha wenyeviti wa vijiji, vitongoji ,mgambo na wanachama wa CCM,ambapo wanne wamekufa na wawili walinusurika kifo . 

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo, alisema tukio hilo limetokea majira ya saa mbili usiku may 4 ,wakati marehemu alipokuwa amejipumzisha nyumbani kwake. 

Alisema wauaji hao,  walifika nyumbani kwa Chanjale ,kitongoji cha Makarafati kijiji cha Umwe Kusini ,kata ya Umwe  na kumkuta kajipumzisha ndani kwake ndipo walipompiga risasi na kutokomea kusikojulikana kwa kutembea kwa mguu. 

Njwayo alieleza kuwa, wauaji hao wamekuja na staili mpya ya kutotumia pikipiki baada ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo, kupiga marufuku usafiri wa pikipiki kuanzia saa 12 jioni. 

Alifafanua kwamba,april 29 mwaka huu, Hamad Malinda, mkazi wa kijiji cha Mgomba Kaskazini, kata ya Mgomba,Ikwiriri,aliuawa kwa kupigwa risasi,na watu ambao hawakutumia usafiri huo. 

 Njwayo, alisema wauaji hao wanasoma alama za nyakati kwa kusoma doria za askari polisi hivyo kutimiza malengo yao. 

"Jeshi la polisi bado linaendelea na kazi yake ya kuwasaka wauaji na mtandao wao wote, hivyo niwatoe hofu wananchi kuwa kila kitu kinaanza taratibu, na serikali itashinda kwani hakuna linaloshindikana "alisema. 

Kwa upande wa wananchi akiwemo Yusuph Kipe, Zainab Kelo walibainisha kuwa, tatizo lililopo ni doria kutofika maeneo ya pembezoni mwa miji na vijijini ambako ndiko matukio yanatokea.

Walisema, CCM taifa inapaswa kuliona hilo na kuiomba kuangalia namna ya kusaidia wanachama wake ambao ndio wanaokumbwa na matukio hayo. 

Kuhusu jeshi la polisi walipongeza kwa kutolala masaa 24 kulinda raia na mali zao licha ya kulitaka jeshi hilo lisome mbinu mpya wanazotumia watu hao. 

"Kwa matukio haya ya ndani ya wiki moja,napata somo kuwa hawa watu bado tunao kwenye jamii yetu, haiwezekani mtu aue kisha atembee tu inawezekana ni watu tunaoishi nao humu humu vijijini "alisema Kipe. 

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, alisema polisi bado inaendelea na kazi yake usiku na mchana. 

Lyanga aliiomba jamii kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuacha kuficha taarifa za wahalifu kwenye maeneo yao. 

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Ndikilo, alisema hali sio shwari kwasasa wilaya ya Rufiji. 

Aliwataka wananchi washirikiane na polisi kwa kusema watu wageni wanaoingia kwenye maeneo yao, na wanaowatilia shaka. 

Mhandisi Ndikilo, alisema inspector general (IGP) Enerst Mangu, ametangaza bingo ya kiasi cha sh. mil tano kwa mwananchi atakaesaidia kuwafichua wauaji. 

Mkuu huyo wa mkoa, alisema hakuna haja ya kuogopa kutaja wahalifu wasiolitakia mema taifa na mkoa kijumla na kuchafua amani iliyopo. 

Mhandisi Ndikilo, aliitaka jamii iendelee kuwa na imani na serikali na vyombo vyake vya dola wakati vikiendelea kupambana katika maeneo ya Rufiji na Kibiti. 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages