Wednesday, May 3, 2017

POLEPOLE: KUWA MWANACCM NI KUKUBALI KUWA DARAJA LA KUWAUNGANISHA WATU NA SERIKALI YAO

“Sisi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni wajamaa, wakati wote tunazungumza kijamaa, hata tunapokosea hukosoana kijamaa. 

Kama wajamaa hatupaswi kwa namna yoyote ile kubakisha chembe ya kutokuelewana wala kutokufahamiana kwa sababu tunayo nafasi ya kuzungumza, kurekebishana, kuonyana na kukaripiana. Na kijamaa mtu lazima abadilike, mwenendo wake usiokuwa mwema kwa maslahi mapana ya Chama Cha Mapinduzi”. 

Hayo yalisemwa na liyekuwa mgeni rasmi Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi alipokuwa akihutubia Mkutano wa Viongozi wa ngazi zote wakiwemo mabalozi (Wenyeviti wa mashina) katika wilaya za Bukoba mjini na Vijijini mnamo tarehe 28/04/2017 huko Bukoba Mjini Kagera. 

Akiendelea kueleza juu ya historia ya Chama Cha Mapinduzi, Ndg. Humphrey Polepole alisema,
Chama Cha Mapinduzi kina historia ndefu, kwanza ni Chama kikongwe Afrika nzima (kimekuwa chama kiongozi Afrika nzima). Ndiyo Chama pekee Afrika kinachoongoza kwa idadi ya wanachama (takribani mil.8 mpaka sasa), kinachotufuatia ni Chama tawala kinachotoa uongozi kule Afrika Kusini ANC, lakini vyama vyote kusini mwa Afrika (kimoja kimeshaanguka kabisa hakipo madarakani Zambia), vinavyobaki vyote vimeishi na kunufaika kwa ulezi wa Chama Cha Mapinduzi ikiwemo kuwasaidia katika harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika kama vile Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Msumbiji, Zimbabwe na Angola.

Ukitoa Chama Cha Kikomunist cha Uchina CPC, Chama kinachofatia kwa ukubwa na utajiri wa maarifa duniani ni Chama Cha Mapinduzi. Chama Cha Mapinduzi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977 kutoka kwa wazazi wake TANU na ASP, msingi wa kuanzishwa kwake ulikuwa ni kuwa Chama Cha Wanachama na kinachoshughulika na shida za watu. Chama ambacho mtu yeyote akiona mwanachama wake au kiongozi au mtumishi wake anasema wakiwepo hawa niko salama. Nikiwa na matatizo yangu nikiona mtu ana nguo za kijani naweza nikampa shida yangu ikafanyiwa kazi. Wakulima wanapopata changamoto kimbilio lao kabla ya kufika Serikalini ni kwenye Chama Cha Mapinduzi.

Mwaka 1964, kulifanyika jaribio la Mapinduzi hapa Tanzania, kipindi hicho nchi ilikuwa imerithi Jeshi kutoka kwa wakoloni liliotambulika kama “African Care” kwa Kiswahili cha zamani. Jeshi hili Lilikuwa na nidhamu ya kikoloni, lilifundishwa kushughulika na watu kwa fikra na muelekeo wa kikoloni na nidhamu yake ilikuwa ni kutii Serikali ya kikoloni. Mwaka 1964 kwa nidhamu ile ile ya kikoloni jeshi hili likafanya jaribio la uasi la kutaka kupindua nchi. kwa utaratibu mzuri uliokuwepo kipindi hicho katika nchi, jaribio lile lilishindikana. Na ndipo kuanzia hapo mpango wa kulikataa jeshi hilo ulianza. Chama Cha Mapinduzi kwenye Jumuiya yake ya Umoja wa Vijana kote nchini Tanzania kiliandikisha vijana madhubuti na imara hao walikwenda kuanzisha hili tunaloliita JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA. Leo hii Mtu kwa matendo yake, kwa mwenendo wake akifanya Chama Cha Mapinduzi kikose heshma mbele ya watu, kipoteze heshima ambayo kimejijengea katika Taifa hili tangu mwanzo, atakuwa amekikosea sana Chama hiki.

Chama Cha Mapinduzi kimetutolea viongozi madhubuti ambao walitoa maisha yao kwa ajili ya watanzania. Wapo akina mzee Karume, Mwl Nyerere, mzee Kawawa, mzee Kahama na wengine wengi, walitoa maisha yao wakajikana kwa ajili ya Tanzania, wakajenga Chama kikawa imara na wakaiimarisha nchi leo tunajivuna sisi ni Raia wa JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA na kwa sasa tunaongoza kuwa nchi imara na madhubuti Afrika, isingalikuwa CCM haya yote tusingelikuwa tunajivuna. 

Akiendelea kuhutubia hadhara Ndg. Humphrey Polepole(pichani) alisema, Kiongozi hupaswi kujisahau. Kiongozi unaposhindwa kutambua shida za watu, ukajiona wewe ni bora zaidi kuliko wale waliokupa dhamana ni makosa makubwa. wakati mwingine ni vizuri kufahamiana na wanachama na wananchi ili kujua shida zao na changamoto zao kwa sababu wao hujua pia majawabu ya changamoto na shida zao. Tukiwasikiliza tutawaelewa na tutatafuta namna nzuri ya kuwasaidia. Lakini kama tukijifungia kwenye kuta zetu tukakaa juu sana, ama kwenye Serikali, ama kwenye Chama, tukawapuuza, TUTAHARIBIKIWA. 

ITIKADI maana yake ni ujumla wa mawazo yetu, malengo yetu, misingi, tamaduni na desturi zetu kama Chama. Pamoja na mambo mengine, Itikadi ya Chama Cha Mapinduzi inajumuisha IMANI yake. Ujumla wa mawazo yetu ndio hutaarifu namna ambavyo tunapaswa kuenenda na ujumla wa fikra na mawazo yetu ndio unatuambia ni namna gani tuielekeze Serikali kutenda. 

Chama Cha Mapinduzi kinaamini Binadamu wote ni sawa. Haijalishi una kipato cha juu, cha chini, au cha kati kwa maana ya fedha mbele ya Chama Cha Mapinduzi sisi sote ni sawa. Haijalishi ni mtoto wa maskini ama tajiri, atakapofika kwenye huduma za umma sisi sote ni sawa. Na imani hii tunaielekeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutenda sawasawa nayo.

Imani nyingine ya Chama Cha Mapinduzi, Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. UTU tafsiri yake ni kuwapenda wenzetu, kutokuwabagua wenzetu, kutokudhulumu haki za watu wetu, UTU ni kutetea haki za watu wetu, ni kusimamia vizuri kabisa mipango na miradi ya maendeleo ili watu wetu kutoka maeneo mbalimbali wapate maendeleo kama ambavyo inawapasa wapate.

Imani nyingine ya Chama Cha Mapinduzi inasema “Ujamaa na kujitegemea ndio njia pekee ya kujenga Jamii ya watu walio sawa na huru”. Ujamaa ni Udugu, Umoja na mshikamano. Penye ujamaa hakuna utengano, kuna Umoja tu hakuna udhaifu, lakini kuna watu huru, wanaojitambua, wanaoweza kusema kwa uwazi na kusimamia kweli na wanazingatia misingi ya usawa.

Kwenye Chama Cha Mapinduzi, Sisi sote ni wamoja, ni ndugu, tunagawana rasilimali katika nyumba yetu kwa faida yetu. Hata kwenye uchaguzi aje tajiri na maskini kwetu sisi wote ni sawa. Tutawapima kwa hoja zao, maono yao ya wapi wanataka kututoa na wapi wanataka kutupeleka halafu sisi kama Chama tutawatafakari tena na tena kwa maslahi mapana ya Chama Cha Mapinduzi hapo tutasema huyo ndiye anafaa kutuongoza na huyo tutakaye mchagua hata wasio WANACCM watamkubali kwa sababu tumemchukua mtu ambaye kwa viwango na vigezo vyote ANAFAA na ANATOSHA.

Kama unathamini utu wa mtu huwezi kumtukana mtu, kumkosea heshima, wala kumdhulumu mtu mali yake na wale wenye shida kama watakuwepo utawasaidia, na wale usiokuwa na uwezo wa kuwasaidia utawaunganisha na wahusika ili wapate msaada.

Huwezi kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakati unasambaza chuki, fitina unazungumza watu, unasengenya watu na unajipenda wewe mwenyewe tu badala ya kuwaweka wanachama kwanza unajiweka wewe kwanza. Wewe unaona ndio mtu bora kuliko watu wengine ukisema wewe imekwisha na ukienda wewe wakufuate. Mwana CCM wa kweli anaamini CCM kwanza na mengine baadae. Na anaamini Chama hiki kikiimarika faida yake si kwetu tu ni kwa umma mzima wa watanzania. Ndio maana mwl nyerere alituambia ”Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba” .

Tangu kuundwa kwa Taifa letu, Chama pekee chenye mizizi, Itikadi, kilichojengwa katika utamaduni wa kuwaheshimu watu, kuwapenda watu, kuwaweka watu kwanza, na kutetea masilahi yao ni Chama Cha Mapinduzi. 

Ili uwe muumini kwenye Chama Cha Mapinduzi, lazima ukubali kuziishi ahadi zake kwa mwenendo wako kama mwanachama au kiongozi. Kwenye katiba ya Chama Cha Mapinduzi inasema mtu huwezi kuwa mwanachama sharti umekubaliana na ahadi za mwananchama kisha ukaapa mbele yetu kwamba utaishi ahadi hizo ambazo ndio ishara kwamba hakika unaamini katika imani yetu.

Mojawapo ya ahadi ya mwanachama ya 4 inasema RUSHWA NI ADUI WA HAKI, SITAPOKEA WALA KUTOA RUSHWA”. kutoa au kupokea rushwa hupelekea kufanya uamuzi isivyopasa na kwa upendeleo na hatimaye kukiuka msingi wa imani kwamba binadanu wote ni sawa. Hii ni marufuku kwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Mtu anayenunua uongozi kwa fedha yake hawezi kuwatumikia wananchi na wanachama badala yake atautumia kwa kadri anavyoona inaafaa na sio kulinda wala kusimamia maslahi mapana ya Chama Cha Mapinduzi na UMMA wa watanzania.

1968 Mwl. Nyerere aliandika, “kazi ya Chama cha Siasa kilichoimara ni kuwa kama DARAJA la kuwaunganisha watu na Serikali waliyoichagua na kuiunganisha Serikali na watu inayotaka kuwahudumia, ni wajibu wa Chama kuwasaidia watu kuelewa Serikali yao inafanya nini na kwa nini”. Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mnapaswa muwe daraja, katika ya Wananchi na Serikali yao. 

Mwenyekiti wetu wa Chama na Rais wetu wa JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA anatupenda kwelikweli. Nataka niwahakikishie kuwa Jembe tulilonalo sasa si la kilimo cha kawaida, ni la mashamba makubwa makubwa ambalo hakuna mtu mwingine aliyelitengeneza isipokuwa sisi wenyewe. Kama daraja, tunapaswa kuisaidia Serikali kusemea mazuri  yake kwa wananchi waelewe kuhusu nini serikali inafanya na kwa nini. 

Ndg. Humphrey Polepole aliendelea kuwakumbusha Viongozi wa Chama juu ya kufuatilia fedha za Halmashauri 10% kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. “Maendeleo yetu kama Taifa ni Sera za CCM, Viongozi wa CCM Mkoa na Wilaya mnapaswa mkayafatilie haya,  mnapaswa kujua pesa ziko wapi, zinatolewa na nani na kwa watu gani kwa lengo la kuhakikisha pesa hizo zinawafikia wananchi wa maeneo yenu kwa wakati na kwa haki na usawa”.

Mkutano huu uliwahusisha Wenyeviti na Makatibu wa Chama katika Wilaya za Bukoba Mjini na Vijijini pamoja na wenyeviti na makatibu wa Jumuiya za Chama Mkoa na Wilaya zote za Bukoba mjini na vijijini, kamati za uongozi, kamati za siasa, Sekretarieti, wajumbe wa Halmashauri kuu za wilaya zote mbili, mkoa, wajumbe kutoka vikao vya maamuzi kata pamoja na matawi na mabalozi. 

Ndg. Humphrey Polepole alipata fursa ya kusiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa hadhara hiyo na kuzipatia ufumbuzi palipo na uwezekano. Ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika mkoani humo tangu litokee tetemeko la ardhi, Ndg. Humphrey Polepole alipata wasaa wa kuwapa pole wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kwa maafa makubwa yaliyotokea kwenye janga hilo.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.