LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 9, 2017

JPM ATOA MAGAZRI MATATU YA WAGONJWA KWA WABUNGE

Na Mwadishi Wetu
Rais Dk. John Pombe Magufuli ametoa magari mapya matatu ya kubebea wagonjwa kwa Wabunge watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao ya ubunge.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam mchana huu, imesema, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amekabidhi magari hayo aina ya Land Cruiser Hardtop kwa niaba ya Rais Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mkoa wa Rukwa Ally Keissy, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Munde Tambwe na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Balozi Kijazi amesema Rais Magufuli ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha Wabunge hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.

“Mhe. Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Mhe. Keissy umekuwa hata ukitafuta miadi ya kuja kumuona Mhe. Rais kwa suala hili, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu. 

“Tunafahamu kila Mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii, na huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro.” Amesema Balozi Kijazi.

Balozi Kijazi amewapongeza Wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao za kisiasa wala makundi.

Kwa upande wao Ally Keissy, Munde Tambwe na Lucy Mayenga wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitikia kilio chao cha kuwasaidia wananchi magari ya kubebea wagonjwa, na wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuwapigania Watanzania wote hasa wenye shida na pia kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages