Sunday, May 7, 2017

BULEMBO: MASALIA YA WALIOKISALITI CHAMA DAR WATAENDELEA KUSHUGHULIKIWA

DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hali ya kisiasa ndani ya Chama mkoani Dar es Salaam si shwari kutokana na kugubikwa na masalia ya wanachama na viongozi walioisaliti CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kilisema masalia hayo ni shida ndani ya CCM na kwamba lazima yaondolewe ili kukiacha Chama katika mikono salama wakati kikiendelea na mchakato wa uchaguzi mkuu ndani ya Chama.

Kauli hiyo nzito ilitolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, wakati akizungumza na Wajumbe wa Mabaraza ya Jumuia za CCM na Halimashauri Kuu ya CCM wilayani Ilala, Temeke, Kigamboni, Kinondoni na Ubungo, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Bulembo, CCM ni Chama kikongwe cha siasa hapa nchini ambacho kiko makini na kina mkono mrefu wa kufahamu mambo, ikiwemo waliokisaliti wakati huo wa uchaguzi mkuu.

Alisema kuwa tayari kimebaini kuwepo kwa kundi hilo la wasaliti likiwa limeweka kambi nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Ilala, Asaa Simba kwa nia ya kupanga safu ya uongozi ndani ya CCM.

Kutokana na kubainika kwa kundi hilo, Bulembo alitoa agizo kwa viongozi wa CCM na jumuia zake kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kuhakikisha haipitishi majina ya wagombea hao ambao ni wasaliti.

Alionya kuwa ikibainika kwa kiongozi yeyote kuwa alipitisha jina la mgombea ambaye ni msaliti, atawajibishwa haraka iwezekanavyo.

Mwenyekiti huyo alisema kamwe, CCM haiwezi kukubali kambi ya wasaliti iwapangie safu ya uongozi ndani ya Chama.

“CCM ina mkono mrefu na iko makini, hivyo inaona mbali kuliko wanavyofikiri watu wengine. Tunajua kinachofanywa sasa na masalia ya wasaliti ambao waliachwa katika mchujo wa kutimuliwa na Halmashauri Kuu iliyopita.

“Katika maamuzi ya Halmashauri Kuu iliyopita kwa mkoa wa Dar es Salaam tuliwafukuza Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huu Ramadhani Madabida, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kinondoni Salumu Madende na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala Asaa Simba,” alisema Bulembo.

Alisema licha ya kuwafukuza viongozi hao, bado kuna kuna wengine ambao waliisaliti CCM kwa namna moja au nyingine katika uchaguzi mkuu uliopita na hivyo kuchangia Chama kushindwa vibaya katika baadhi ya maeneo.

Bulembo alisema atafanya kila njia ili kupata kibali kutoka kwa vikao husika kwa ajili ya kuwashughulikia wasaliti walionakia katika mkoa wa Dar es Salaam.

“Ndani ya CCM naitwa “mnoko” kutokana na msimamo wangu wa kutetea maslahi ya Chama. Sasa nasema acha niendelee kuitwa “Mnoko” kuliko kukubali makapi ya wasaliti hawa waendelee kuitesa CCM. Nitapambana nao hadi dakika za mwisho…hiyo ndio ahadi yangu yangu kwenu wanachama wenzangu.

“Hivi, kama tumeweza “kukata vichwa vya wasaliti” akina Madabida je, tutashindwa “kukata miguu” ya masalia ya wasaliti katika mkoa huu?,” alihoji Bulembo na kuongeza kuwa lazima waondoke haraka.

Alisisitiza kuwa watu hao lazima waondoke ndani ya CCM kabla ya kumalizika kwa uchaguzi na badala yake waende kwenye nyumba yao ya wasaliti kwa Edward Lowassa.
“Waondoke waende kwenye nyumba yao ya wasaliti kwa Lowassa na Mahanga. Hapa si mahali pa wao kuishi au kufanyakazi tena,” alisema.

Alisema CCM lazima ijipange kwa kukabiliana na hali hiyo kwa kupitia upya majina ya wasaliti hao kutoka ngazi ya mkoa hadi shina na watakao bainika wachukuliwe hatua kali bila kuangalia sura zao.

“Mtoto wa nyoka ni nyoka. Hatuwezi kulala kwa wasi wasi ndani ya nyumba yetu eti kwa ajili ya kuhofia mtoto wa nyoka.

“Kama tumeua nyoka tena baba na mama kwanini tuogope mtoto wa nyoka. Haiwezekani na haitawezekana kama waliingia salama katika Chama hiki basi sasa waondoke salama,” alisema.

Alisema wana-CCM lazima watambue kwamba katika kipindi hiki cha uongozi wa CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais, Dk. John Magufuli, hakuna mchezo mchafu utakaoachwa.
Alisema Magufuli amedhamilia kukisafisha Chama na kukiweka kwenye mazingira mazuri ili kiwe kimbilio la wanyonge na hivyo kuwataka wamuunge mkono katika kutimiza azma hiyo.


Bulembo alisema hakuna maana yoyote kwa wasaliti hao kuendelea kubaki ndani ya CCM kwa sababu ya kujuana na kuvumiliana.
------------------------------------
MATUKIO KATIKA PICHA KUHUSU ZIARA HIYOYA BULEMBO MKOANI DAR, LEO

PICHA ZOTE NA BASHIR NKOROMO
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.