Na Lilian Lundo– MAELEZO
Mabadiliko
ya Tabianchi ni moja ya eneo ambalo limekuwa likileta athari kubwa katika nchi
nyingi Duniani.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeweka
mikakati mbalimbali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Moja
ya mikakati hiyo ni pamoja na ujenzi wa kuta kwenye Pwani ya Bahari ya Hindi,
upandaji wa mikoko ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa mifereji ya maji ya mvua na
maji machafu.
Akitoa
taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Mkurugenzi
Idara Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi anasema Mradi wa
kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika Pwani ya
Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam
unatekelezwa katika maeneo manane na unagharimu dola za kimarekani milioni tano.
Bwana
Muyungi anasema maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa kuwa ni eneo la Obama
Ocean Road, Kigamboni kwenye Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Bungoni
Ilala, Miburani Mtoni, Temeke, Salender Bridge, Kunduchi, Mbweni na Ununio
Kinondoni.
Anasema
jumla ya Dola za Marekani 3,489,482 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya ujenzi wa ukuta
eneo la Ocean Road na Kigamboni pamoja
na mitaro iliyopo Bungoni, Ilala na Mtoni Temeke.
Katika
ziara hiyo Bwana Muyungi anazitaja shughuli nyingine zinazotekelezwa katika
mradi huo ni pamoja na kukarabati ukuta wa bahari katika maeneo ya barabara ya
Obama ambayo zamani ilijulikana kama Ocean Road wenye urefu wa mita 820 na Kigamboni eneo la Chuo cha Kumbukumbu cha
Mwalimu Nyerere, urefu wa mita 380, ambapo ukuta huo utadumu kwa zaidi ya miaka
73.
Pamoja
na matengenezo hayo, fedha nyingine zitatumika kutoa mafunzo kuhusu nishati
safi ya kurudisha mikoko ekari 40 ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi katika
maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Sheha
Mjaja anaeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni pamoja na mradi wa kujenga uwezo wa
kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya ukanda wa Pwani
(mradi wa LDCF).
“Mradi huu unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya makamu wa Rais katika maeneo ya
Bagamoyo, Pangani, Rufiji na Zanzibar na unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa
Mazingira (The Global Environmental Facility- GEF) kupitia dirisha la Mfuko wa
Nchi Masikini Duniani (The Least Developed Countries Fund – LDCF) la Mkataba wa
Mabadiliko ya Tabianchi – UNFCCC,” anafafanua Sheha Mjaja.
Anafafanua
kuwa fedha za Mradi huo zinapitia Shirika la Usimamizi wa Mazingira la Umoja wa
Mataifa (UNEP) ambalo pia lina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu na usimamizi
wa fedha na Jumla ya Dola za Kimarekani milioni
3,356,300 zimepangwa kutumika katika mradi huu zikijumuisha fedha za
usimamizi na ufuatiliaji za UNEP ambapo Utekelezaji wa Mradi huu ulianza mwaka
2013 na unategemewa kumalizika mwaka 2017.
Mkurugenzi mkuu huyo wa ZEMA amezitaja
shughuli zitakazofanyika katika mradi huo ni upandaji wa mikoko/mikandaa na
miti ya ukanda wa pwani katika maeneo 6 ya Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa
kuta za bahari katika eneo la Kilimani mjini Unguja na Kisiwa Panza, wilaya
ya Mkoani Pemba.
Anafafanua
kuwa, eneo la Kilimani ambalo ufukwe wake una urefu wa mita 538 litajengwa kuta
mbili (2) za aina ya “gyrones”,ambapo kila ukuta utakuwa na urefu wa mita 100 kutoka kwenye
fukwe kuelekea baharini na ukuta
mwingine utajengwa eneo la Kisiwa Panza ambao utakuwa na urefu wa mita 75.
Kuhusu mradi wa LDCF kwa upande wa
Zanzibar, Bwana Muyungi anasema fedha zote za mradi huko, zimegawanyika katika
maeneo matatu ambayo ni upande wa mikoko na miti ya ukanda wa Pwani ambapo
jumla ya Shilingi 163,895,500 zimepangwa kutumika.
Eneo
lingine ni fedha za ujenzi wa ukuta wa Kisiwa Panza na Kilimani, ambapo gharama
halisi za kuta hizo bado hazijajulikana, ila zitajulikana baada ya zabuni
zilizoitishwa kutangazwa. Zabuni hizo zitasimamiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa
inayoshughulikia huduma za miradi (The United Nations Office for Project
Services-UNOPS) ambao ndio washauri wa ujenzi wa kuta hizo.
Anasema
eneo la mwisho ni fedha kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa mradi ambapo kila
Taasisi inayotekeleza mradi huo imetengewa jumla ya Dola za Kimarekani 8,600.0
kwa mwaka kwa ajili ya kuwalipa wasimamizi wa mradi na kuendesha shughuli za mradi katika maeneo
ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na mafuta, ununuzi wa shajala (stationery) na
gharama za ufuatiliaji.
Hata hivyo, SMZ imekamilisha Mradi
wa ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua na maji machafu kwa shehia za Msingini na
Kichungwani katika mji wa Chake Chake Pemba kupitia Idara ya Mazingira Zanzibar
kwa kushirikiana na wanajamii kupitia kamati za jamii za Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii Tanzania (TASAF) za Shehia hizo.
Aidha, mradi huo umepata fedha
kutoka Shirika la Umoja la Mpango wa Mazingira (UNEP), TASAF, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Aqua-4-All ya Uholanzi ambapo mradi ulianza mwaka 2009 na
kumalizika mwaka 2013.
Malengo ya SMZ ni kuwepo mtaro wa
maji ya mvua yasiyochanganyika na maji machafu yanayotoka majumbani, kupunguza
uchafuzi wa mazingira ya bahari pamoja na viumbe vyake unaotokana na maji
machafu yanayotoka majumbani kwa kuyasafisha kabla ya kuingia baharini.
Nae,
Abdul Juma mkazi wa Kinondoni Jijini Dar es Salaam anazipongeza Serikali ya
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna zinavyojizatiti
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutunza na kukarabati kuta za Pwani
ya bahari ya Hindi.
Anasema,
Serikali imefanya uamuzi mzuri wa kujenga kuta mpya katika kingo za Bahari ya
Hindi ambapo kama kuta za zamani zingeendelea kuwepo zingeleta athari kwa
nyumba zinazopakana na Bahari kutokana na kuta hizo kuchoka na kuwa na nyufa.
Anatoa
rai kwa Watanzania kuiunga mkono Serikali katika kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi kwa kutunza vyanzo vya maji, kupanda miti pamoja na
kutunza miundombinu ambayo imejengwa kwa ajili ya kuzuia athari za mabadiliko
ya tabianchi.
Kwa
upande wake, Asha Said mkazi wa Chake chake Pemba ameipongeza SMZ kwa
kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua na maji machafu kwa shehia
za Msingini na Kichungwani ambapo kabla ya utekelezaji wa mradi huo wakazi wa maeneo
hayo walikuwa wakipata kero ya
kuingiliwa na maji majumbani mwao katika kipindi cha mvua.
Ameendelea
kwa kusema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeleta ukombozi kwa wananchi wa
maeneo hayo ambapo kuna wakati iliwalazimu kuhama katika makazi yao kutokana na
kero ya kujaa maji katika nyumba zao.
Matarajio
ya SMZ na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kuimarisha
mashirikiano, uzoefu na utaalamu wa kimazingira katika kuhakikisha kuwa
Zanzibar na Tanzania Bara zinaendelea kutekeleza miradi ya kimazingira ya
pamoja kwa faida endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.
No comments:
Post a Comment
ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇